058-Asbaabun-Nuzuwl: An-Nisaa Aayah 058: إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
Sababu Za Kuteremshwa (Baadhi Ya Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
An-Nisaa 058-Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe…
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٥٨﴾
58. Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe. Na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Ni uzuri ulioje wa Anayokuwaidhini kwayo Allaah! Hakika Allaah daima ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote.
Sababun-Nuzuwl:
Aayah hii ni ya pekee katika Suwrah hii ya An-Nisaa (4:58) ambayo imeteremka Makkah. Imeteremshwa Siku ya Fat-h Makkah (Ushindi). Ibn Jurayj amehadithia kwamba imeteremshwa kuhusu ‘Uthmaan bin Twalhah pale Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipochukua ufunguo wa Ka’bah kutoka kwake akaingia Ka’bah. Alipotoka nje ya Ka’bah, alitoka huku akiwa anasoma:
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُكُمْ أَن تُؤَدُّوا الْأَمَانَاتِ إِلَىٰ أَهْلِهَا
Hakika Allaah Anakuamrisheni kurudisha amana kwa wenyewe.”
Hapo akamwita ‘Uthmaan bin Twalhah na akampa funguo. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]. Funguo hizo zimeendelea kubakia katika ukoo huo, kizazi baada ya kizazi mpaka sasa, na mpaka Siku ya Qiyaamah ukoo huo umefadhilishwa kuwa ndio wenye amana ya kukamata funguo za Al-Ka’bah.