Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kuhusiana Na Qur-aan – 02
Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa'ah Kuhusiana Na Qur-aan – 02
Dalili Za Wazi Kuwa Qur-aan Ni Maneno Yake Allaah Na Wala Haijaumbwa
Abuu Rabiy’
Dalili Ya Kwanza:
Kauli yake Allaah (Tabaaraka Wa Ta’aalaa):
وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ۚ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْلَمُونَ﴿٦﴾
6. Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah (Qur-aan), kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hivyo kwa kuwa wao ni watu wasiojua. [At-Tawbah: 06]
Anasema Imaam Al-Qurtubiy (Allaah Amrehemu):
“فنص على أن كلامه مسموع عند قراءة القارئ لكلامه، ويدل عليه إجماع المسلمين، على أن القارئ إذا قرأ فاتحة الكتاب أو سورة قالوا سمعنا كلام الله…”
“Akadalilisha (Allaah) kwamba maneno yake yanasikilizwa wakati wa kusoma msomaji maneno Yake, na inajulisha (jambo hili) makubaliano ya Waislamu kuwa msomaji akisoma Suwratul-Faatihah au Suwrah yoyote wanasema tumeyasikia maneno ya Allaah.”
Dalili Ya Pili:
Kauli yake Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa):
وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ صِدْقًا وَعَدْلًا ۚ لَّا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١١٥﴾
115. Na limetimia neno la Rabb wako kwa kweli na uadilifu. Hakuna mwenye kuyabadilisha maneno Yake. Naye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote. [Al-An’aam: 115]
Kwa maana hakuna maneno yaliyotimia kama maneno ya Allaah na wala hakuna maneno yenye ukweli katika akhbaari zake na maamrisho yake na makatazo yake kama maneno yake Subhaanahu wa Ta’aalaa.
Kabla hatujaendelea mbele zaidi kuna swali la msingi sana ambalo latakikana kuulizwa nalo ni:
Vyenye kutegemezwa kwa Allaah vyagawanyika sehemu kuu ngapi?
Jawabu ni kuwa vyenye kutegemezwa kwa Allaah vyagawanyika katika sehemu kuu mbili na hakuna ya tatu!!
1. Chenye kutegemezwa kwa Allaah halafu chenyewe chaweza kujitegemea au kwa lugha ya kitaalamu chaweza kusimama chenyewe. Kama vile unaposema Ngamia wa Allaah, Nyumba ya Allaah, Mitume wa Allaah, n.k.
Hapa utaona kuwa kile ulichokitegemeza ni dhati na ina uwezo wa kusimama yenyewe kwa sababu tukimtoa ngamia peke yake au Mitume au nyumba hapana Shaka kuwa vina uwezo wa kujitegemea vyenyewe.
2. Vyenye kutegemezwa kwa Allaah ambavyo havina uwezo wa kusimama vyenyewe au kujitegemea vyenyewe kama vile maneno ya Allaah, uwezo wa Allaah, n.k.
Ama ya kwanza, inakuwa kutegemezwa kwake kwa Allaah inajulisha kuwa kitu hicho ni kitukufu, na ni kiumbe na hakijapatapo kutegemezwa kwa Allaah ila kwa sababu ya utukufu wake.
Ama ya pili, ni kutegemeza sifa kwa mwenye sifa yake!!
Sasa inakuwa ni jambo la ajabu sana kusema kuwa ile sifa nayo imeumbwa!!
Mimi ninaposema kuwa Allaah Anacheka au Allaah Anazungumza, hapa nimetegemeza sifa Yake Kwake Yeye mwenyewe.
Sasa hapa ikiwa tunakubaliana kuwa Allaah yupo, na kila kilichopo lazima kiwe na sifa haiwezekani kiwepo kitu halafu hakina sifa, sasa vipi Allaah ajiumbie sifa ya maneno ilhali Yeye ni wa mwanzo na hakuna kabla Yake chochote?
Na ndio Ahlus-Sunnah wal Jamaa’ah wanasema maneno katika dhati Yake Allaah ni sawa sawa na maneno katika sifa Zake.
Kama tunakubaliana wote kwa pamoja kuwa Allaah Anazungumza na hii ni sifa yake thaabit, sasa vipi Ayaumbe maneno Yake ambayo ni Qur-aan??
Ima mseme kuwa Allaah Alikuwepo na Alikuwa hana sifa hata moja, na hii haiwezekani kwa sababu hakuna kilichopo ambacho hakina sifa.
Na ndio maana Ashaa’irah katika mlango huu wamejichanganya sana, mara waseme Allaah maneno Yake ni ya ndani ya nafsi Yake na Jibriyl (‘Alayhis-Salaam) alikuwa anaelezea maneno yaliyomo ndani ya nafsi ya Allaah!!
Ama kuuliza swali la mtego la kutaka kutenganisha kati ya sifa ya Allaah ya kuzungumza hii Qur-aan, ni swali ambalo kimsingi halina faida. Utakuta wanaulizana hivi:
Katika dunia hii kuna vitu viwili tu; kiumbe na muumbaji, na wala hakuna cha tatu sasa je hii Qur-aan ni Allaah? Ukisema hapana si Allaah, watakuambia khalaas Qur-aan ni kiumbe!!
Hili ni swali la bid’ah ambalo wamezusha watu wapotofu ili wawapoteze waja Wake Allaah.
Kwa sababu hauwezi kumtenganisha Allaah na sifa Zake akawa Allaah Yupo pasina kuwa na sifa enyi qaumu...
Je, Qur-aan imeumbwa?
Fuatana na Mimi katika kubainisha uongo wa watu
waliopinda kuhusiana na hili In Shaa Allaah.