Kuswali Katika Miswala Yenye Picha Za Ka’bah Misikiti Na Mapambo Mengineyo

 

Kuswali Katika Miswala Yenye Picha Za Ka’bah  Misikiti Na Mapambo Mengineyo

 

www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Naomba kuuliza kuhusu misala tunayosalia yenye picha za misikiti na Kaaba na mengineyo ina picha za mauwa je inajuzu kusalia?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

 

Miswala hiyo haifai kuswaliwa khasa ile yenye picha za Ka’bah  au picha za Misikiti au picha zozote nyenginezo    ambazo hazina umbo la mtu kwa sababu ni Makruwh (jambo la kuchukiza) kwani humsababisha mtu kupoteza khushuu ya Swalaah.

 

Hata miswala yenye picha za mauwa na mapambo mengineyo ni bora kujiepusha nayo kwa sababu huenda miswala hiyo imetengenezwa na makafiri wanaotumia ujanja kupamba vitu kama hivyo kisha humo humo kuchora picha za misalaba, wanyama na kadhalika bila ya kuidhihirisha wazi, bali kuifichaficha ndani ya mapambo hayo ili  mtu asiweze kujua mpaka afanye uchunguzi wa kina.

 

 

Ama miswala yenye picha za umbo la mtu au kiumbe chenye roho, ni haraam.

 

 

Tunafahamu kuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika nyumba yake mara moja kulikuwa na pazia iliyokuwa na picha. Akawa ni mwenye kushughulishwa na hilo, hivyo akaamuru kuwa pazia hiyo ikatwe vipande vipande na kuondoshwa mlangoni. 

 

 

Pia mara moja Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali katika khamiysah (Nguo ya sufi iliyo na alama) na alipokuwa akiswali alizitazama alama zake. Alipomaliza akasema: ((Ipelekeeni khamiysah hii yangu kwa Abuu Jahm na nileteeni (badala yake) anbijaaniyyah (Nguo ya kukwaruza isiyo na alama) kwani imenipotezea umakini wangu katika Swalaah))

 

Katika riwaayah nyengine amesema:

 

 ((…kwani nimetazama alama zake wakati wa Swalaah ilikaribia kunitia katika mtihani” [Al-Bukhaariy, Muslim] 

 

 

Na ‘Ulamaa wetu wamekataza kuswalia Miswala yenye picha kama hizo na zifuatazo ni fatwa zao:

 

Imaam Ibn Baaz-Haifai Kuswali Kwenye Miswala Au Mazulia Yenye Picha Ya Ka’bah Na Masjid An-Nabawiy

 

Imaam Ibn Baaz-Hukmu Ya Kuswali Kwenye Miswala Au Mazulia Yenye Mapambo

Imaam bin ‘Uthaymiyn-Hukmu Ya Kuswali Juu Ya Mazulia Yenye Picha Za Misikiti

 

Kuswali Juu Ya Mazulia Yenye Nembo Za Misalaba Na Eneo Lenye Msalaba Ndani

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share