Ikhtilaatw (Mchanganyiko Wa Wanaume Na Wanawake)

 

Ikhtilaatw

 

(Mchanganyiko Wa Wanaume Na Wanawake)
 

Imekusanywa na: Alhidaaya.com

 

 

 

 

Maana yake:

 

Ni kuchanganyika kwa mwanamke na mwanamme au kwa wingi wanawake na wanaume.

 

Kuchanganyika huku ni aina tatu:

 

 

1.    Kuchanganyika wanawake na mahaarim wao wa kiume, hili jambo limeruhusiwa katika shari'ah ya Kiislam.

 

 

2.    Kuchanganyika wanawake na wanaume kusababisha ufisadi, hili limeharamishwa katika shariy'ah.

 

 

3.    Kuchanganyika wanawake na wanaume sehemu za kutafuta elimu; mashuleni, vyuoni, au mahospitalini, maofisini na sehemu mbalimbali za kazi. Na katika vyombo vya usafiri kama mabasi, matreni, ndege, n.k. Huenda mtu akaona kuwa hakuna fitna katika michanganyiko ya sehemu hizo, lakini hakika kila sehemu kuna fitna itakayozuka maadam tu hakuna tahadhari za kuepukana nazo.

 

Maasi haya yanadhihirika sana katika Jamii yetu ikiwa ni majumbani mwetu, katika shughuli zetu mbali mbali za furaha na misiba, katika vikao mbali mbali ikiwa ni vya mikusanyiko ya kijamii au ya kifamilia.

 

Pia aghalabu shemeji huwa anaishi nyumba moja na mke wa wa kaka yake bila kuhisi tabu au kuona kuwa hakuna madhara yoyote na hali Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametutahadharisha katika Hadiyth ifuatayo: 

 

 ((إياكم والدخول على النساء، قالوا: يا رسول الله أرأيت الحمو؟ قال: الحمو الموت)) متفق عليه

“Tahadharini kuwaingilia (kuingia majumbani mwao) wanawake” Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: “Shemeji ni mauti”. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ni mazoea ambayo yamekuwa mazito kuyaacha kwa wasiotaka kufuata amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na wasiokhofu adhabu Zake. Ama kwa walio kinyume na hivyo hutahadhari na jambo hili na kuanza kubadilisha nidhamu ya maisha katika nyumba zao; kwa kumzuia shemeji kuishi katika nyumba moja na mwanamke au ikiwa mtu kafanya ziara, mwanamke hubakia katika chumba mbali na kile alicho shemeji yake kama ukumbini, au chumbani mwake hadi atakapoondoka.

 

Ajabu ni kwamba unapokataza, baadhi ya watu huona kwamba ni jambo la kuzidisha tabu katika dini, au hutaka kujua dalili ya makatazo haya kwa kudhani kuwa hakuna makatazo. Swali ni kwamba: "Nani aliyekataza maasi haya?" Jibu ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndio waliokataza kama tunavyoelezea dalili zake hapa chini.

 

Makatazo Ya Ikhtilaatw Katika Qur-aan Na Sunnah

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) 

وَإِذَا سَأَلْتُمُوهُنَّ مَتَاعًا فَاسْأَلُوهُنَّ مِن وَرَاء حِجَابٍۚ 

Na mnapowauliza wake zake haja, waulizeni nyuma ya pazia [Al-Ahzaab: 53].

 

 قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَلِكَ أَزْكَى لَهُمْ

Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao. Hivyo ni utakaso zaidi kwao[An-Nuwr: 30].

 

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا ۖ وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ ۖ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ ۖ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ ۚ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾

Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe khimaar (shungi) zao mpaka vifuani mwao, na wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume wao, au wana wao wa kiume, au wana wa kiume wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kiume wa kaka zao, au wana wa kiume wa dada zao, au wanawake wao (wa Kiislamu), au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio ya jimai miongoni mwa wanaume au watoto ambao hawatambui kitu kuhusu sehemu za siri za wanawake. Na wala wasipige miguu yao yakajulikana yale wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]

 

Ameamrisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah hizo tukufu kuinamisha macho, na kulinda tupu, hivyo bila shaka haya ni kutokana na kuchanganyika baina ya mwanamke na mwanamume ndipo ikatoka amri ya makatazo ya hayo ya Ikhtilaatw.

 

 

Amri ya kuinamisha macho ni kuepusha matamanio ya uzuri atakaouona mmoja kwa mwenzake, kuona, kusikia kote kunampeleka mtu katika zinaa kama anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم قال :) كتب على ابن آدم نصيبه من الزنا مدرك ذلك لا محالة , العينان زناهما النظر , والأذنان زناهما الاستماع , واللسان زناه الكلام , واليد زناها البطش , والرجل زناها الخطا , والقلب يهوى ويتمنى , ويصدق ذلك الفرج أو يكذبه ( أخرج البخاري ومسلم

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Ameandika kila sehemu ya zinaa ambayo humuingiza mtu katika shauku. Hakutokuwa na kuikwepa. Zinaa ya macho ni kutazama, ya masikio ni kusikiliza, ulimi ni kunena maneno, mkono ni kuunyoosha, mguu ni hatua zake na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha (hutenda) au kukadhibisha (huacha)” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Vile vile,

قال صلى الله عليه سلم: ((لا يخلوّنّ أحدكم بامرأة إلا مع ذى محرم )) متفق عليه

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hawi faraagha mmoja wenu pamoja na mwanamke ila awepo Mahram wake”. [Al-Bukhaariy Na Muslim].

 

Kuchanganyika mwanamke na mwanamume katika sehemu moja ndio maana ya Hadiyth hii. Sasa vipi anayesababisha fitna na anayesababishiwa kuingia katika fitna wakakaa pamoja?

 

 

Na Mahram aliyekusudiwa hapo ni; mume au mwanamume ambaye hawezi kumuoa mwanamke huyo anayekusudiwa katika Hadiyth, mfano: kaka, ami, mjomba, mtoto wa dada au kaka, au kaka wa kunyonya ziwa moja. Asichanganyike na mwengine zaidi ya hao kwani.

 

 عن عمر رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم: ((ما خلا رجل بامرأة إلا كان الشيطان ثالثهما)) الترمذي

Kutoka kwa 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao.” [At-Tirmidhiy].

 

Tumeonywa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Aayah nyingi kwamba shaytwaan hutuamrisha maovu na uchafu, huanza kumtia binaadamu katika nafsi yake mawazo ya matamanio mwishowe nafsi humfikisha mtu kufanya maovu kwani Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

إِنَّ النَّفْسَ لأَمَّارَةٌ بِالسُّو

Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu.. [Yuwsuf: 53]

 

Tumeelezewa kisa cha Nabiy Yuwsuf ('Alayhis-salaam) alipokuwa chumbani pekee na mke wa Mfalme au Waziri ambaye alimtamani Yuwsuf japokuwa alikuwa ni mtoto aliyemnunua na kumlea hadi akafikia umri wa kubaleghe:

 

وَرَاوَدَتْهُ الَّتِي هُوَ فِي بَيْتِهَا عَن نَّفْسِهِ وَغَلَّقَتِ الْأَبْوَابَ وَقَالَتْ هَيْتَ لَكَ ۚ قَالَ مَعَاذَ اللَّـهِ ۖ إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ ۖ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ﴿٢٣﴾

Na yule mwanamke ambaye yeye (Yuwsuf) alikuwa katika nyumba yake alimtongoza kinyume na nafsi yake; na akafunga milango, na akasema: Haya njoo! (Yuwsuf) Akasema: Najikinga kwa Allaah! Hakika yeye bwana wangu amenifanyia makazi mazuri. Hakika madhalimu hawafaulu. [Yuwsuf: 23]

 

Tukio hilo lilikuwa baada ya kuweko kuchanganyika pekee mwanamke na mwanamume japokuwa hakudhania Yuwsuf kwamba mke wa Mfalme au Waziri atafikia kumtamani na kutaka kuingia naye katika maovu. Lakini kwa Rahma ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) alimuoka Nabiy Yuwsuf (‘Alayhis-sallam). 

وَلَقَدْ هَمَّتْ بِهِ ۖ وَهَمَّ بِهَا لَوْلَا أَن رَّأَىٰ بُرْهَانَ رَبِّهِ ۚ كَذَٰلِكَ لِنَصْرِفَ عَنْهُ السُّوءَ وَالْفَحْشَاءَ ۚ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُخْلَصِينَ﴿٢٤﴾

Na kwa yakini alimtamani (Yuwsuf) na (Yuwsuf) angelimtamani lau kwamba asingeliona buruhani kutoka kwa Rabb wake. Hivyo ndivyo Tunavyomwepusha na uovu na machafu. Hakika yeye ni miongoni mwa waja Wetu waliokhitariwa kwa ikhlaasw zao. [Yuwsuf: 24].

 

Na mambo ya kukaa mwanamume na mwanamke peke yao yamekatazwa kabisa katika Shariy'ah kwani lazima yataleta mabaya. Wala usiseme: “huyu shemeji yangu”-“ndugu wa mke wangu” au “shemeji yangu” - “mke wa ndugu yangu.” Wote hao hatari kwako na kwao na walio kama hao. Faragha kitu kibaya kabisa.  

وقال عليه الصلاة والسلا: (( المرأة عورة ...))  الترمذي

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwanamke ni uchi…). [At-Tirmidhiy].

 

Maana ya kuwa ni 'uchi' ni kwamba haijuzu kutazama mapambo yake wala sehemu ya mwili wake hivyo kuchanganyika kunaleta maana zote hizo.

 

  وقال عليه الصلاة والسلام: ((ما تركت بعدي فتنة هي أضر على الرجال من النساء)) البخاري

 Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sikuacha baada yangu fitna ambayo ina madhara kwa wanaume kama wanawake” [Al-Bukhaariy].

 

Sehemu Zinazotokea Mchanganyiko

 

Nje kama madukani, sokoni, kazini …

 

Mwanamke ameamrishwa kubakia nyumbani kwake ila kwa dharura tu na akitoka anatakiwa awe amejifunika na kujisitiri vizuri kwa hijaab iliyokamilika kishariy'ah inayopaswa kutimizwa, nayo ni mavazi yanayotakiwa yatimize masharti nane zifuatazo:

 

1.     Mwili wote ufunikwe isipokuwa uso na viganja vya mikono. [‘Ulamaa wengine wameona hata uso na mikono pia ifunikwe].

 

2.     Nguo isiwe yenye mapambo.

 

3.     Lazima iwe nzito kiasi isiwe yenye kuonyesha mwili.

 

4.     Lazima iwe yenye kupwaya na sio ya kubana hata ikaonyesha mwili wake.

 

5.     Asijitie manukato.

 

6.     Isishabihi vazi la kiume.

 

7.     Isishabihi mavazi ya kikafiri.

 

8.     Isiwe ya kujionyesha, maana kwamba isiwe kwa ajili ya kiburi kuwa ni vazi bora kuliko la mwengine.

 

Amri ya kubakia nyumbani ni Anaposema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ 

Na bakieni majumbani mwenu.. [Al-Ahzaab: 33]

 

Kwa jinsi iliyvokuwa ni muhimu mwanamke kubakia nyumbani, hata Swalaah yake tumeambiwa kuwa ni bora kwake kuswali nyumbani kuliko kwenda Msikitini.

 

Na aliporuhusu wanawake kwa kuwakataza Swahaba wasiwazuie kwenda kuswali misikitini, na walipokuwa wakihudhuria, alipendelea mlango mmoja uwe kwa ajili ya kuingia wanawake:

 

 عن ابن عمر رضي الله عنهما قال : قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: (( لو تركنا هذا الباب للنساء)) . قال نافع : فلم يدخل منه ابن عمر حتى مات" أخرجه أبو داود بسند صحيح

Kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Tungeliuacha huu mlango kwa ajili ya wanawake)). Kasema Naafi': "Hakuingia tena Ibn 'Umar mlango huo mpaka kufariki kwake". [Abu Daawuwd kwa isnaad Swahiyh]

 

  وعن أم سلمة رضي الله عنها قالت : "أن النساء في عهد رسول الله صلى الله عليه وسلم كن إذا سلمن من المكتوبة قمن وثبت رسول الله صلى الله عليه وسلم ومن صلى من الرجال ما شاء الله فإذا قام رسول الله صلى الله عليه وسلم قام الرجال"  أخرجه البخاري . قال ابن شهاب (وهو الزهري ): فأرى والله أعلم أن مكثه لكي ينفذ النساء قبل أن يدركهن من انصرف من القوم .

Kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu 'anha) ambaye amesema: "Wanawake katika zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakimaliza kuswali Swalah za fardh waliondoka, na akabaki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wanaume waliojaaliwa kuswali, kisha alipoinuka Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wao waliinuka" [Al-Bukhaariy na Muslim]. Amesema Ibn Shihaab (ambaye ni Az-Zuhriy) naona kuwa na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi kuwa kubaki kwake Nabiy msikitini ni kuachia nafasi ya wanawake kuondoka kwanza kabla ya wanaume.

 

Vile vile, itakapombidi mwanamke kutoka nje kwa dharura basi ahakikishe kuwa anatekeleza maamrisho ya Rabb wake katika hali hiyo, kama tulivyotaja kuhusu hijaab na pia katika maongezi akaze sauti yake. 

فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ﴿٣٢﴾

Basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika. [Al-Ahzaab: 32].

 

Hali Inayoruhusu Kuchanganyika

 

Kuna baadhi ya hali za dharura zinazoruhusika kuchanganyika, na mfano wa hali hizo ni kama imetokea mwanamke kuharibikiwa safarini, kupotea, kutaka kudhuriwa na watu au kuvunjiwa heshima na ikabidi kumuokoa na kumsindikiza hadi penye amani au palipo watu wake, kupatwa na ajali kukawa hakuna wanawake wa kumsaidia ila wanaume tu, na hali nyinginezo mbalimbali za dharura kama za matibabu ikiwa hakuna madaktari wa kike n.k.

 

Katika Haram (Makkah)

 

Baadhi ya watu wanatoa hoja ya Msikiti wa Makkah wanapoona kwenye matelevisheni au kwa waliojaaliwa kufika kuwa kule kuna mchanganyiko wa wanaume na wanawake. Wengi wanashindwa kuelewa kuwa hali ile ya dharura inayosababisha vile si hoja ya kumfanya Muislamu kuruhusika kuchanganyika kwani huko kuna ulazima wa kutekeleza Twawaaf na haiwezekani kuwatenga wanawake katika 'Ibaadah hii kutokana na hali ilivyo, watu kuhitajika kufanya Twawaaf wanapoingia tu Haram, umbali wanaotoka watu nchi kwa nchi, na muda wa 'Ibaadah hiyo na kutowezekana kupangika zamu ya utekelezaji wa 'Ibaadah hiyo kwa wanaume na wanawake ndio kukapatikana dharura hiyo.

 

Pamoja na kuwepo hali hiyo na ugumu huo wa kuwatenganisha wanawake na wanaume kwenye Twawaaf, askari waliomo Msikitini hapo wanajaribu sana kuwatenganisha wanawake na wanaume katika kuswali ingawa wengi huwa wakaidi.

 

Katika Kazi

 

Ikiwa kuna dharura ya kufanya kazi na ikasababisha kuchanganyika, kwani katika kufanya kazi mfano biashara kutakuweko wanawake na wanaume, ila lazima izingatiwa shariy'ah isemavyo na kutekeleza inavyopasa na kuepukana na makatazo.

 

Kuhudumia Wageni

 

Wanapokuja wageni wa mume au jamaa zake mke lakini ambao si mahaarim wake, anaweza kuwahudumia kwa kuwatayarishia chakula kama kuwapelekea hali akiwa katika stara kamili bila kuonekana sehemu zozote za fitnah, na muhimu aweko mumewe. Hii ni kutokana na dalili ifuatayo:

 

 لما عرَّسَ أبو أُسَيد الساعِدِيُّ دعا النبيَّ صلى الله عليه وسلم وأصحابَهُ فما صنَع لهم طعاماً ولا قدم إليهم إلا امرأتُهُ أمُّ أُسيد، بَلَّتْ  (وفي رواية: أنقعت)  تَمَراتٍ في تَوْر من حجارةٍ منَ الليل، فلما فَرَغَ النبيُّ صلى الله عليه وسلم من الطعام أماثَتْه له فسقَتْهُ تتْحِفُه بذلك. (فَكَانَتِ امْرَأَتُهُ يَوْمَئِذٍ خَادِمَهُمْ. وَهْيَ الْعَرُوسُ)

 Abu Asyad As-Saa'idiy alipooa, alimualika Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba zake. Hakuna aliyetayarisha chakula au kuwahudumia isipokuwa mkewe Ummu Asyad. Aliroweka tende katika bakuli la udongo usiku uliopita. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipomaliza kula, alimpakulia na kumtunikia, hivyo mkewe akawa ndiye mwenye kuwahudumia wageni na alikuwa ndiye bi harusi. [Al-Bukhaariy, Muslim na wengineo].

 

Katika Kusaidia Kazi Za Jihaad

 

Inafaa wanawake kusaidia katika kazi kama hizo kama kuwatibu waliojeruhiwa, au kuwapelekea maji n.k. kwani hivyo walifanya wanawake zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na kazi kama hizo kwa ajili ya maslahi wa Waislamu. Swafiyyah bint 'Abdul-Mutwalib, Shangazi yake Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alishiriki katika kuwapiga makafiri na kumkinga Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), pia aliweza kumuua Myahudi kwa kumkata kichwa chake hata wakaingiwa na khofu Mayahudi waliotaka kuvamia kambi waliyoachwa wanawake, watoto na wazee kwa kudhania kwamba kuna mwanamume hivyo hawakuthubutu kuwasogelea.   

 

Vile vile katika kushirikiana kutekeleza kazi za Dini kama kufunza watu, kuwapatia misaada wanayohitaji, kutoa ushauri mbali mbali n.k. maana kuna baadhi ya wanawake wamejaaliwa kuwa na busara na hikma katika mambo haya. Vile vile uwezo kwa kusaidia kwa njia yoyote ile, kama ni wa kifedha, kielimu n.k.  

 

 

Wa Allaahu A’alam

 

Share