Mirungi - 3: Fataawa Za 'Ulamaa

 

Mirungi - 3 (Mwisho) - Fataawa Za Wanachuoni

Abuu 'Abdillaah

 

 

Alhidaaya.com

 

 

BismiLlaahi Rahmaani Rahiym

 

Fataawa Za Wanachuoni Kuhusu Mirungi

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾

 

Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashaytwaan, na shaytwaan amekuwa ni mwingi wa kumkufuru Rabb wake. [Al-Israa: 27]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema pia:

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ

 

Wala msijitupe katika maangamizi kwa (kuzuia) mikono yenu (isitoe).  [Al-Baqarah: 195]

 

Pia anasema Aliyetukuka:

وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ

 

Na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu.. [Al-'Araaf: 157]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Allaah Anachukia mambo matatu: kusengenya, kuomba na kupoteza mali.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Mirungi ni mti mchafu mbaya uliongia katika ardhi ya Waislam, na wameingia katika mitihani baadhi ya Waislam, na unasababisha madhara ya kimali, kimwili, kidini na kiwakati. Vilevile, ulimaji wake husababisha hasara kubwa za kiuchumi kwa sababu ya maji mengi yanayotumika katika ardhi ngumu ambayo inaoteshwewa. Na kwa hivyo, ni HARAAM kulimwa katika ardhi za Waislam, na pia kutafunwa.

 

Matumizi ya Mirungi yanaingia moja kwa moja katika vileo kwani vinamtoa mlaji katika hali yake ya kawaida na kumbadilisha na kuingia katika hali ya kuishi kwenye fikra za kuwazika na ndoto za aliye macho, vilevile mtu kuwa juu juu amehandasika (kalewa), kadhalika ndani yake kuna kuidhuru mtu afya yake, ubadhirifu wa mali na wakati.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu vinywaji fulani vinavyotengenezwa na asali, mahindi, au shayiri kwa njia ya kuvundikwa au kuchanganywa hadi kugeuka na kuwa pombe. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ufupi na uwazi alijibu:

 

“Kila chenye kulewesha ni ulevi, na kila ulevi ni Haraam.” [Muslim]

 

Na amesema tena Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Kila chenye kulewesha kikiwa kingi, basi japo kichache ni Haraam.” (Ahmad, Abu Daawuud na At-Tirmidhiy). Na kwengine, “Kinacholewesha japo ni ndoo nzima, basi hata muonjo (kuinywa kidogo) wake ni Haraam.” [Ahmad, Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy]

 

Naye ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akiwa amesimama kwenye Minbar ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatangazia,

 

“Pombe ni chochote chenye kufunika akili” [Al-Bukhaariy Na Muslim]

 

Wanachuoni mbalimbali wametoa fatwa mbalimbali za kuonyesha uharamu wa utumiaji wa Mirungi.

 

Zifuatazo ni Fatawa za Wanachuoni mbalimbali, nimechagua Fatwa mbili hapa chini zitakuwa zinawakilisha fatwa nyingi za Wanachuoni wakubwa wa nchi hizo:

 

 

Mwanachuoni Mkubwa Wa Saudia Allaamah Imaam Ibn Baaz (Rahimahu Allaah), Aliyekuwa Mufti Wa Saudia

 

Alipoulizwa:

 

‘Wengi katika waraibu wa Mirungi, inapofika wakati wa Swalaah basi (kwa wale wanaoswali) hutoa midomoni mwao (Mirungi) na kisha huitema kwenye mifuko ya plastiki kisha huswali. Na baada ya Swalaah huichukua kutoka kwenye mfuko na kuila tena, je, Mirungi ni najisi? Na nini hukmu ya mtu mwenye kuswali na hali imo kwenye mdomo wake? Na je, inajuzu kwa yule mwenye kuila akachelewesha Swalaah hadi amalize kula, kisha aje kulipa Swalaah zake?

 

 

Akajibu:

 

Sina elimu ya chenye kuonyesha kuwa ni najisi, kwani huo ni mti maarufu, na asli kuhusiana na miti na mimea mbalimbali ni kuwa yote ni twahara. Ama utumiaji wake ni HARAAM –kwa kauli sahihi za Wanachuoni- kutokana na madhara yake mengi.

 

Na inawapasa hao wenye kutumia, wasiitumie kabisa wakati wa Swalaah, na wala haijuzu hata kidogo mtu kuchelewesha Swalaah kwa ajili hiyo, bali inampasa Muislam aiswali Swalaah kwa wakati wake katika Jama’ah pamoja na ndugu zake Waislam Misikitini, kwa kauli yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Atakayesikia Wito wa Swalaah (Adhaan) na asiende kuswali, basi hana Swalaah ila kwa udhuru.” [Ibn Maajah, Ad-Daaraqutwniy na Al-Haakim kwa Isnaad sahihi]

 

Na aliulizwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuhusiana na huo ‘udhuru’ ambao umeruhusiwa, akajibu: “Ni khofu au maradhi”’ na matumizi ya Mirungi sio udhuru wa kishari’ah, bali ni jambo la Munkar, na ikiwa mtu atachelewesha Swalaah kwa sababu hiyo, basi hiyo itakuwa ni dhambi kubwa sana. Na haifai vilevile kuunganisha Swalaah mbili kwa sababu ya Mirungi, kwani huo si udhuru wa kishari’ah unaokubalika…”

 

[Kitabu ‘Fataawa Islaamiyah’ kilichokusanywa na Muhammad Al-Musanad, Juz. 3, uk. 445 – Majmu’ Fataawaa wa Maqalaat Mutanawi’ah, Juz. 23]

 

  

 

Shaykh Muqbil bin Haadiy Al-Waadi'iy (Rahimahu Allaah), Aliyekuwa Mwanachuoni Mkubwa Wa Yemen

 

 

Aliulizwa:

 

Ni ipi hukmu ya kishari'ah ya kula Mirungi?

 

 

Akajibu:

 

Mirungi ni mti ambao hauna khayr ndani yake.

Allaah Amewatahini Wayemen na Wahabashi kwa mti huu muovu. Na jambo sahihi ni kuwa (mti huu wa Mirungi) umeleta uharibifu kwa uchumi wetu, umeleta uharibifu kwa afya zetu, na umepoteza wakati wetu, bali umepoteza akili zetu. Wengi vichaa kwa sababu ya Mirungi.

 

Hivyo, ninawanasihi kila ndugu ajiweke mbali na mti huu muovu, ambao umewapotezea Wayemen wakati wao (mkubwa), na umewapotezea umri wao, na umewafanya watu wengi kuwa ni waraibu (wa Mirungi).

 

Huo ni mti muovu wenye kusababisha madhambi, namnasihi kila Muislamu kujiepusha mbali nao.

 

Na ninapenda Allaah Awawafiqishe Wayemen na Awabadilishie kwayo kwa mazao mema yenye kunufaisha nchi yao.

 

Ni waajib kwa 'Ulamaa na Madaktari na Walinganiaji katika njia ya Allaah wawakimbize watu (kuuacha) mti huu muovu ambao umetuacha tukiwa tunasubiri kutoka Marekani na kwengineko nafaka kama Thomu na Shamari.

 

Na hivi ndivyo, kila jambo  sisi tumekuwa tegemezi kwa maadui zetu, pamoja na kuwa Yemen ilikuwa ikijulikana hadi kupachikwa jina 'Yemen ya Kijani' (kwa uzalishaji mazao), lakini sasa kwa sababu ya Mirungi, inapaswa kupachikwa jina 'Yemen ya Vumbi' (kwa ukame)'.

 

[Kutoka katika kanda: 'As-ilah Ba'adhw Al-Akhawaat Min Ta'iz']

 

 

Tunamalizia makala hii ya Mirungi kwa wito kwa walaji wote wamche Allaah na wajiepusha na jambo hilo chafu, baya, lenye madhara makubwa ya kidini, kimwili, kiafya, kimali na kiuchumi, na watumie muda wao huo mkubwa wanaoupoteza kufanya yenye manufaa kwa dunia na Aakhirah yao. Na wakumbuke wataulizwa siku ya masiku kwa muda wao walioupoteza, na kwa mali yao walivyotumia.

 

Na wale wanausuhubiana na walaji, wito kwao wajiepushe kusuhubiana na watu hao wasije nao kuingia kwenye balaa na afa hilo miongoni mwa maafa makubwa yaliyomo katika jamii ya Kiislam, wakumbuke pia mwenye kusuhubiana na mfua vyuma, basi ima akuunguzie nguo yako au akutie harufu mbaya ya moshi wake. Hiyo ni tahadhari tuliyopewa na Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa hiyo tuizingatie sana in shaa Allaah.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ajaalie risala hii iwe khaaliswan Liwajhih na iwe na taathira kwa walaji Mirungi na in shaa Allaah iwe ndio sababu ya kuachana kwao na uraibu huo.

 

 

MWISHO

 

Mirungi - 1

Mirungi - 2

 

Share