Bid'ah - Uzushi Katika Dini

 

Abu 'Abdillaah na

 

Muhammad Al-Ma'awy
 

 BismiLlaah Rahman Rahiim

 

Alhidaaya.com

 

 

Maana:

 

Maana ya Bid'ah katika lugha ni kila kitu ambacho kimeanzishwa si katika mfano ule wa mwanzo, sawa kama ni mzuri au mbaya. Na mfano wake ni kama kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَإِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿١١٧

Mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Anapokidhia jambo basi huliambia Kun! Basi nalo huwa. [Al-Baqarah: 117]

 

Yaani ameanzisha tofauti na ule mfano wa kwanza.

 

Al-Badii‘ na al-Bid’ah ni kitu kinachokuwa mwanzo kabisa. Allaah Amesema:

 

قُلْ مَا كُنتُ بِدْعًا مِّنَ الرُّسُلِ وَمَا أَدْرِي مَا يُفْعَلُ بِي وَلَا بِكُمْ ۖ إِنْ أَتَّبِعُ إِلَّا مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ وَمَا أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mimi sikuwa jambo jipya lilozuka miongoni mwa Rasuli na sijui nitakavyofanyiwa mimi wala nyinyi. Sifuati isipokuwa niliyofunuliwa Wahy, nami si chochote isipokuwa ni mwonyaji bayana. [Al Ahqaaf: 9]

 

Hii ina maana kuwa mimi siye Nabiy wa kwanza kuja ulimwenguni bali wameletwa Manabii wengi kabla yangu. Na inasemekana kwamba ameanza fulani bid'ah inamaanisha kuwa ameanzisha fulani njia ambayo haikupitiwa na yeyote.

 

Bid'ah katika istilahi ya kisheria ina maana njia iliyoanzishwa katika dini, inayoshabihiana na ile njia ya kisheria (lakini kwa hakika si hivyo, yaani inakwenda kinyume na sheria), hivyo wanazua bid'ah kwa kusudi ya kuwa na ada ya kujikurubisha kwa Allaah Aliyetukuka (hii ni kuwa haiwatoshelezi yale yaliyokuja katika sheria na hivyo wanataka kuongeza juu yake kama kwamba wanakamilisha yaliyopungua)”. (Imaam Abu Ishaaq ash-Shaatwiby, al-I’tiswaam, Mj.1, uk. 37).

 
Naye Shaykh Abdulla Swaalih Farsy amesema, “Bidaa iliyokusudiwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukatazwa ni kutiwa katika Dini – na kuitakidiwa kuwa ni Ibada jambo ambalo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema litiwe katika Dini wala hakulifanya, na hali ya kuwa anao uweza wa kulifanya”. (Bid-a, Dibaji).

 

Ibn al-Jawzy amesema: “Bid'ah ina maana ya kitendo ambacho hakikuwepo hivyo kukianzisha na mara nyingi katika uanzilishi ni kwamba kinakwenda kinyume na sheria na hivyo kuwajibika kuzidisha au kupunguza” (Talbiys Ibliys, uk. 16 – 17).

 

Imaam Maalik amesema: “Yeyote atakayeanzisha katika Uislamu bid'ah akiona kuwa ni nzuri amedai ya kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya khiyana katika kufikisha risala, kwani Allaah Amesema,

 

 الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]

 

Na kwa yule ambaye hakuwa na dini siku hiyo basi hatakuwa na dini leo” (al-I’tiswaam, Mj.1, uk. 49 ya Imaam ash-Shaatwiby).

 
Imaam Ahmad amesema: “Misingi ya Sunnah kwetu sisi ni kushikamana na yale waliyokuwa nayo Swahaba wa Nabiy, kuwafuata na kuacha bid'ah kwani kila bid'ah ni upotevu” (Ibn Ya’la al-Fara’, Twabaqaatul Hanaabilah, Mj. 1, uk.241).

 

Ibn Taymiyah naye anatuelezea ya kwamba, “Bid'ah katika dini ni ile ambayo haikuletwa na Allaah na Nabiy Wake na ile ambayo haikuamriwa kwayo kwa jambo ambalo ni wajibu wala lenye kupendeza” (Majmu’ul Fataawaa, Mjalada 4, uk. 107 – 108).

 

Na Ibn Rajab naye anasema: “Maana ya bid'ah ni yale yaliyoanzishwa ambayo hayana asili katika sheria yenye kuwafikiana nayo, na ama yale ambayo yana asili katika sheria basi sio bid'ah, japokuwa ni bid'ah kilugha (kumaanisha kuwa kwa matumizi ya lugha ya Kiarabu inafahamika hivyo lakini kisheria inakuwa ni kinyume na hayo matumizi ya kilugha)” (Jaamiul ‘Uluum wal hikam, uk. 233).

 

Katika maelezo hayo yameweka mipaka ya kwamba bid'ah sehemu yake ni katika dini na wala si katika mambo ya kidunia, na hiyo ni kuwa “ni njia iliyoanzishwa”. Na dalili katika hili ni kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

“Mwenye kuzua katika dini yetu hii lisilokuwamo humo litakataliwa” [Al Bukhaariy na Muslim].

 

Na katika baadhi ya riwaya nyengine:

 

“Yeyote atakayezua katika hili jambo letu – na makusudio pia (jambo letu la dini) lisilokuwamo humo, litakataliwa”. [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Dawuud na Ibn Maajah].

 

Yaani itakataliwa kutoka kwa mwenye kufanya kama zinavyorudishwa hela mbaya kwa mwenyewe.

 

Hadiyth hii pia inatambulikana kuwa ni miongoni mwa misingi ya Uislamu na ni katika Hadiyth Arobaini za Nawawi (ya 5). Panasemwa ya kwamba kuna Hadiyth 2 ambazo zinakamilishana moja kwa nyingine, Hadiyth ambazo hazina budi, kwani ni mizani ya yaliyo ndani ya mioyo, nayo ni Hadiyth:

 

“Hakika vitendo huzingatiwa kwa nia” [Imepokewa na Jama’ah].

 

Na Hadiyth ambayo hakuna budi kwayo, kwani ni mizani ya dhahiri na ni yale Hadiyth hii yaliyokuja nayo:

 

“Mwenye kuzua katika hili jambo letu lisilokuwamo humo litakataliwa”.

 

Hivyo ni budi kwa amali kukubaliwa kuwe na mambo mawili:

 

1. Lifanywe kwa kumridhisha Allaah Aliyetukuka.

 

2. Lifanywe katika njia inayokubaliwa katika sheria.

 

Hivyo alipoulizwa Fudhayl bin ‘Iyaadh, Faqihi mtawa – kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa),

الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ

Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Al-Mulk: 2]

 

Hivyo amali nzuri ni ipi? Akasema: “Akhlaswahu wa as-wabahu – yenye ikhlasi na iliyo sahihi”. Pakasemwa: “Ee baba ‘Aliy, maana ya yenye ikhlasi na ya sawa ni nini? Akasema: “Hakika amali inapofanywa kwa ikhlasi na isiwe kwa njia ya sawa (isiyo sahihi) haitokubaliwa, na ikiwa imefanywa kwa njia ya sawa lakini haina ikhlasi ndani yake pia haitokubaliwa. Hivyo mpaka iwe na ikhlasi na ya sawa, na yenye ikhlasi ni lazima ifanywe kwa ajili ya Allaah na kuwa sawa ni lazima iwe juu ya Sunnah (ifanywe kulingana na alivyofundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam))”.

 
Hivyo bid’ah haiwi isipokuwa katika dini. Na hapa wengi tunakosea kwa kudhania ya kwamba bid’ah inaingia katika mambo ya ada. Vitu vya kawaida haviingii katika bid'ah. Haiyumkini kusemwa kuwa: jambo hili katika mambo ya kimaisha ni bid'ah kwa sababu ma-Salaf miongoni mwa Swahaba na Tabiina hawakufanya. Inawezekana kuwa ni jambo jipya lakini haichukuliwi kuwa ni bid'ah kisheria na kama si hivyo basi tungechukua mengi ambayo tuko nayo leo kuwa ni bid’ah: kama hivi vipaza sauti, mazulia (carpets), hii meza, na hivi viti ambavyo tunakalia, vyote havikuwepo kwa wale Waislamu wa mwanzo na havikufanywa na Swahaba. Je, hizi zinachukuliwa kuwa bid'ah?

 

Na hivyo hukosea wengi katika watu katika jambo hili mpaka wanapoona, kwa sikitiko, minbar yenye zaidi ya vidaraja vitatu wanasema: ‘Hii ni bid’ah. Laa, haiingii bid'ah katika jambo hili.  (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akihutubu mwanzoni juu ya kigogo cha mtende lakini watu walipokuwa wengi aliambiwa, “Je, hatukufanyii kitu ambacho utasimama kwayo mpaka watu wakuone?” Wakaja na fundi seremala ambaye alikuwa Mrumi na kumtengezea minbar yenye vidaraja vitatu na lau jambo hili lingehitajia zaidi ya vidaraja vitatu wangefanya. Mambo haya hayaingii katika bid'ah. Na hizi ni katika ada ambazo kwamba zinatofautiana kwa kutofautiana kwa watu, mazingira na hali. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akila kufuatia ada za kaumu yake na hasa yenye kuafikiana na maumbile yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), maumbile ya usahali (wepesi), unyenyekevu na kujinyima. Hivyo haichukuliwi kuwa kula juu ya meza au kula kwa kijiko kuwa ni bid'ah katika dini”. (as-Sunnah wal Bid’ah, uk. 11 – 14).

 

Vigawanyo vya Bid'ah

 

Bid’ah imegawanywa sehemu mbili:

 

1. Uzushi katika mambo ya kawaida kwa kuzua katika vitu vya kisasa na hii inaruhusiwa kwani asli (msingi) wa mambo haya ni kuruhusiwa.

 

2. Uzushi katika dini na hii ni haramu kwani asli ya mambo ya dini ni tawqifiyyah (kufuata yalivyo au kutosheka na yalivyo). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“Mwenye kuzua katika hili jambo letu lisilokuwamo humo litakataliwa”. [Al Bukhaariy na Muslim]

 

Dkt. Muhammad Salim Badamana katika kitabu chake Hadiyth Arba’ini za Nawawi: Tafsiri na Sherehe yake anaeleza: ‘Kuzua’ ni kuanzisha kitu kwa kupenda mtu mwenyewe na kufuata hawaa (matamanio) yake tu. ‘Katika hili jambo letu’: Katika Dini yetu na sheria yetu aliyotuchagulia Allaah. ‘Lisilokuwamo humo’, Lenye kupingana na kutokubaliana na sheria ya Allaah na jambo ambalo halina ushahidi wala dalili yoyote ya kuafikiana na misingi ya dini. (uk. 40)

 

Bid'ah katika Dini zipo aina mbili pia:

1.   Aina ya kwanza: bid'ah za kauli za kiitikadi kama kauli za Jahmiyah, Mu’tazilah, Khawaarij, Rawaafidh (Mashia), Sufi (makundi ya twariyqah za dhikri kama Qaadiriyyah, Shaadhiliya, Dandarawiya, Naqshabandiya n.k.) na mapote (makundi) mengine yote yaliyopotea katika mas-ala ya Itikadi.

 

2.     Aina ya pili: bid'ah katika ibada kama kumuabudu Allaah kwa ibada ambayo haipo katika sheria. Na hii ina vigawanyo:

 

a)  Kigawanyo cha kwanza: Jambo ambalo katika asli yake ni ibada. Kama kuzua ibada ambayo haina asili katika sheria k.m. Swalah ambayo haipo katika sheria au funga ambayo haipo au sikukuu ambazo hazipo katika sheria kama sherehe za Maulidi na nyinginezo.

 

b)   Kigawanyo cha pili: Kuongeza katika ibada ambayo ipo katika sheria kama lau itazidishwa rakaa ya tano katika Swalah ya adhuhuri au alasiri.

 

c)   Kigawanyo cha tatu: Ni ile ambayo ina sifa ya kutekelezwa kama ibada ya kisheria lakini ikatekelezwa kwa njia iliyo kinyume na sheria. Na hivyo ni kutekeleza adhkaar za kisheria kwa sauti ya pamoja au kushadidisha nafsi katika ibada mpaka inafikia kiwango cha kukutoa katika Sunnah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

d)  Kigawanyo cha nne: Kuweka wakati au siku maalumu ya kufanya ibada ambayo ipo katika sheria lakini haikuhusishwa kisheria. Mfano ni kuweka siku ya 'Nisfu Sha’abaan' (tarehe 15) na usiku wake kwa kufunga na kusImaama kisImaamo cha usiku. Hakika msingi wa swiyaam na tahajjud (Swalah ya usiku) ni ibada ambazo zipo katika sheria lakini kuweka wakati maalumu inahitaji dalili (Sh. Dkt. Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan, Kitaabut Tawhiyd, uk 100 – 101)

 

‘Ulamaa Wengine Wamegawanya Bid'ah Kwa Njia Zifuatazo:

 

i.    Bid’ah nzuri na mbaya.

 

ii. Wengine wameigawanya katika sehemu tano, bid'ah ambayo ni waajib, bid'ah inayopendeza, bid'ah iliyo makruhu, bid'ah haramu na bid'ah inayokubalika (mubaah). Imaam ash-Shaatwiby amewajadili wananvyuoni wenye msimamo huu pamoja na kuchambua msimamo wao huu kwa kirefu ambapo amethibitisha kwa hoja thabiti ya kwamba vigawanyo hivi ni jambo ambalo limezuliwa na hakuna kabisa dalili za kisheria. Na kwamba katika hakika ya bid'ah ni kuwa hapana dalili za kisheria sio katika nassw (yaani Qur-aan na Hadiyth) wala si katika misingi yake. Na lau kama kungekuwa na dalili katika sheria juu ya wajibu au kupendeza au kuruhusiwa haingekuwa bid'ah.

 

iii.   Bid'ah zote katika dini ni upotevu (As-Sunnah wal Bid'ah, uk. 24 na pia tazama ‘Abdur-Rauuf Muhammad ‘Uthmaan, Mahabbatur Rasuul (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Baynal Itiba'a wal Ibtida'a, uk. 215 – 221).

 

Dalili ya Vigawanyo Hivyo Juu:

 

Kundi la kwanza lina rai kuwa si kila bid'ah ni upotevu, bali kuna nzuri na mbaya, na wametoa dalili zifuatazo:

 

• - Kauli ya ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) baada ya kuwaleta pamoja watu katika Swalah ya Tarawehe nyuma ya Imaam mmoja naye ni Ubayy bin Ka'b (Radhwiya Allaahu 'anhu). Aliporudi siku ya pili na kuona watu wanaswali nyuma ya Imaam alisema: “Ni’imatul bid'ah haadhihi" – ni uzuri ulioje wa bid'ah hii. [imepokewa na al-Al Bukhaariy, Ibn Khuzaimah, al-Bayhaqi]. Hivyo dalili hapa ni kauli ya ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuita hilo kuwa nibid'ah na akaisifu kuwa ni nzuri.

 

Jariyr bin Abdullah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

"Yeyote atakayeanzisha katika Uislam Sunnah iliyo nzuri atakuwa na ujira wake na thawabu za yule mwenye kufuata hilo bila kupunguziwa chochote katika ujira wao. Na yeyote atakayeanzisha Sunnah mbaya atapa madhambi na dhambi za wale wenye kufuata baada yake bila ya kupunguziwa chochote katika madhambi” [Muslim].

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal bin Haarith (Radhwiya Allaahu 'anhu) Yeyote atakayehuisha Sunnah miongoni mwa Sunnah zangu, ambayo imekufa baada yangu, atapata ujira sawa na ujira wa atakayeifanyia kazi bila kupunguziwa chochote katika ujira huo. Na atakayezusha upotevu mbaya ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hawakuridhia, (basi atapata mzigo wa madhambi) Sawa na yule atakayetenda uzushi huo, bila madhambi yao kupunguzwa" [Imetolewa na At Tirmidhiy]

 

• - Salaafus Swaalih miongoni mwa Swahaba na Tabi'iyn baada yao waliona vitu fulani ni vizuri ambavyo havina nas maalumu kutoka katika Kitaab na Sunnah na wakakubaliana kwayo. Wala ummah wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) haukubaliani katika upotevu, kwani wao wanajumuika katika uongofu na kwa yale ambayo ni mazuri. Mfano wa hayo ni kukusanya Qur-aan na kuiandika katika msahafu. Baadae watu wakawafuata katika hayo yaliyo mazuri, hivyo wakakusanya na kuiandika elimu na kuboresha na vyote hivi ni vitu vilivyoanzishwa kwani havikuwepo katika enzi ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) – na Swahaba wakaviona ni sawa. Hii kwao ni dalili ya kuwa bid'ah inagawanyika – nzuri na mbaya. Na pia wanatoa dalili ya kuwa Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema: “Kile kinachoonekana na Waislamu kuwa kizuri, hivyo mbele ya Allaah ni kizuri”.

 

Kundi la tatu limejikita kwa kuthibitisha ya kwamba bid'ah zote ni mbaya. Kundi hili limetoa dalili zifuatazo kutoka kwa Qur-aan na Sunnah sahihi:

 

• - Katika Qur-aan ni kauli ya Allaah inayosema:

 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.  [Al-Maaidah: 3].

 

Hii ni dalili kuonyesha kuwa sheria imekamilika, hivyo haihitaji ziada wala kupunguzwa. Lakini maneno ya mwenye kuzua ni kuwa sheria haijatimia na kuwa vimebakia vitu ambavyo ni lazima au vinapendeza kuongezwa katika madai yao. Na lau angekuwa na Itikadi ya kuwa dini imekamilika katika kila njia basi hangezua wala hangepatiliza kwa hilo. Na bila shaka ya kuwa yeyote anayeitakidi hili ni kuwa amepotea kutoka katika njia nyoofu (al-I’tisaam, Mj. 1, uk. 48–49). Na maelezo ya Imaam Maalik kuhusu aayah hii tayari tumeyaeleza nyuma.

 

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153].

 

Swiraatul Mustaqiyma ni njia nyoofu ni njia ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ambayo Ameita watu kwayo na Sunnah na as-Subul ni njia ya watu wa kuleta ikhtilafu na waliopotoka na njia nyoofu, nao ni watu wa bid'ah. Na maana ya as-subul si maasiya, kwani maasiya – kwa namna yalivyo – hayawekwi na yeyote katika njia ambayo itapitwa milele kwa ibada. Na hakika wasifu huu ni hasa kwa uzushi. Ibn Mas’uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituchorea mistari kwa mkono wake, kisha akasema,

 

Hii ni njia ya Allaah iliyonyooka", akasema kisha akachora mistari kuliani na kushotoni mwake. Kisha alisema, "Hivi ni vinjia (subul), hakuna chochote isipokuwa kuna shetani ambaye huwaita watu kwayo". Kisha akasoma aya hiyo ya 153 ya Suwrah An’am”. (Musnad ya Imaam Ahmad na al-Haakim, ambaye amesema ni sahihi na akaafikiana naye Imaam adh-Dhahaby).

 

Mujaahid amesesma kuhusu: 'Wala tattabius subul' ni bid'ah na mambo yenye utata. (Tafsiyrut Twabariy cha Abu Ja’afar Muhammad ibn Jariyr at-Twabariy). Na aaya nyengine ambayo inatumika kama dalili ni:

وَعَلَى اللَّـهِ قَصْدُ السَّبِيلِ وَمِنْهَا جَائِرٌ ۚ وَلَوْ شَاءَ لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ

Na juu ya Allaah kubainisha njia (ya haki), na humo ziko miongoni mwazo za kupotoka. Na kama Angetaka Angekuhidini nyote. [An-Nahl: 9].

 

'Qasdus Sabiyl' ni njia ya haki na nyingine yoyote imepotoka kutoka katika haki na hivyo kuelekea katika njia za bid'ah na upotevu na maasiya. Na Mujaahid amesema: 'Qasdus sabiyl' yaani njia ya katikati baina ya kuvuka mipaka na kuwa pungufu na hii inafaidisha ya kuwa Jaair ni yule mwenye kuchupa mipaka (extreme) au mwenye kupunguza, na zote mbili ni katika sifa za bid’ah.  [Mahabbatur Rasul, uk. 225 – 226].

 

• - Na aayah nyingine katika Qur-aan ni hii ifuatayo:

 

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُّحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ ۖ فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا

 

تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ ۗ وَمَا يَعْلَمُ تَأْوِيلَهُ إِلَّا اللَّـهُ ۗ وَالرَّاسِخُونَ فِي الْعِلْمِ يَقُولُونَ آمَنَّا بِهِ كُلٌّ مِّنْ عِندِ رَبِّنَا ۗ وَمَا

 

يَذَّكَّرُ إِلَّا أُولُو الْأَلْبَابِ

Yeye Ndiye Aliyeteremsha kwako Kitabu humo mna Aayaat zenye maana wazi, hizo ndio msingi wa Kitabu, na nyinginezo zisizokuwa wazi maana zake. Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotovu hufuata zile zisizokuwa wazi maana zake kutafuta fitnah (upotofu) na kutafuta maana zake zilofichika, na hakuna ajuae maana zake isipokuwa Allaah. Na wenye msingi madhubuti katika elimu husema: Tumeziamini, zote ni kutoka kwa Rabb wetu. Na hawakumbuki ila wenye akili. [Aal: ‘Imraan: 7].

 

Aayah hii inabainisha wazi hali ya wenye maradhi ambao hawafuati haki na hivyo hufuata katika Kitabu zile aayah ambazo ni Mutashaabihaat (Zinababaisha/kufichamana) ili wapate kueneza fitna katika dini na hiyo ni kwa sababu ya magonjwa katika nyoyo zao na ufisadi katika ufahamu wao. Na haya yanafanywa na watu wa bid'ah kwani wao huacha aayah ambazo ni Muhkam (zilizo wazi) na kushika zile ambazo ni Mutashaabih. Kuna Hadiyth ambayo inafasiri aayah hii na kuonya wenye kufanya bid'ah na mfano wao. Al-Bukhaariy amepokea kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anha) kuwa amesema:

 

“Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisoma aayah hii (yaani ya 7 katika Suwrah aal-‘Imraan), akasema, alisema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam); "Ukiwaona wale wanaofuata aayah zinazobabaisha hao ni wale ambao kwamba wametajwa na Allaah, hivyo tahadharini nao”.

 

• - Na miongoni mwa Hadiyth ni Hadiyth ya Irbaadh bin Saariyah ambayo inasema: "Siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). alituswalisha, kisha alipomaliza akatugeukia na kutupa mawaidha marefu yaliyotufanya tutokwe na machozi, na mioyo ikhofike. Mtu akauliza: 'Ee Rasuli wa Allaah! Inaelekea kama haya ni mawaidha ya kutuaga, je, unatuusia nini? Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu: Nawausia Ucha wa Allaah, na muwe wasikivu na watiifu hata kama akiwaongoza mtumwa, kwani watakaoishi miongoni mwenu baada yangu wataona tofauti (ikhtilaaf) nyingi. Shikamaneni na Sunnah zangu na za wale Makhalifa wangu waongofu. Ziumeni kwa magego (shikamaneni nazo kwa nguvu). Jiepusheni na mambo mapya ya kuzua, kwani kila mapya yanayoanzishwa ni uzushi, na kila uzushi ni upotevu".

[Imepokewa na Ahmad, Abu Dawud, at-Tirmidhy, Ibn Majah, ad-Daarimiy na ameisahihisha Ibn Hibbaan]. Na katika riwaya nyengine inamalizikia na 

 

“Na nawatahadharisha nyinyi na uzushi katika mambo kwani kila uzushi ni bid'ah na kila bid'ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni”. Hii ni Hadiyth ambayo inaonyesha kuwa kila bid'ah ni upotevu.

 

• - Na Hadiyth nyingine ni hii: “Wakati Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akikhutubia, macho yake yalikuwa mekundu, na sauti yake ikawa juu, na hasira zake zikapanda kama vile mtu anayetoa onyo kuhusu maadui na akisema: ''Maadui wamewashambulia asubuhi na jioni''. Na akisema mara nyingine: "Nimetumwa kama viwili hivi, na akiunganisha vidole vyake viwili vya kati. Kisha akiendelea "Maneno bora kabisa ni yale yaliyomo katika Kitabu cha Allaah, na muongozo mzuri kabisa ni muongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na mambo mabaya kabisa ni uzushi; na kila uzushi ni upotofu". [Imesimuliwa na Muslim].

 

Amesema al-Haafidh Ibn Hajr al-Asqalaaniy: “kauli yake 'Kulla bid’atin dhwalaalah' ni kanuni ya kisheria kamili katika kufahamika kwake. Kama ni kusema hukmu kadhaa ni bid'ah na kila bid'ah ni upotevu hivyo haitakuwa katika sheria kwani sheria yote ni uongofu. Inapothubutu kuwa jambo Fulani lililotajwa ni bid'ah, unasimama imara katika utangulizi wake na hivyo kupata natija inayotakiwa” (Fat-hul Baariy, Mj. 13, uk. 267 – 268).

 

• - Na katika Hadiyth nyingine, ni ile iliyopokewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

 

“Atakayezua akatia katika Dini yetu hii ambacho hakiko atarejeshewa mwenyewe.” [Al- Bukhaariy na Muslim].

 

Na katika riwaya ya [Muslim],Atakayefanya amali ambayo haina amri yetu basi atarejeshewa mwenyewe”.

 

Hii Hadiyth ni dalili ya kwamba yeyote atakayezua katika Dini chochote ambacho hakina msingi wa kisheria kitakuwa batili na atarudishiwa mwenye kukifanya. Imaam an-Nawawy amesema yafuatayo katika kuisherehesha Hadiyth hii: “Na Hadiyth hii ni msingi mkuu katika misingi ya Uislamu na ni katika ukamilifu na upangilifu wa uzungumzi wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ipo wazi katika kukataa kila bid'ah na zenye kuzushwa. Na katika riwaya ya pili kuna nyongeza, nayo ni kuwa huenda mwenye kufanya bid'ah iliyokuwepo tayari akatoa hoja ya riwaya ya kwanza, akisema: ‘Mimi sijazua chochote.’ Hivyo, riwaya ya pili inakataa kila kinachozuliwa kipo wazi kabisa na hii inakuwa ni dalili juu yake, sawa ikiwa ameanzisha mwenye kufanya au imeanzishwa kabla yake naye akafuata. Na hii Hadiyth inafaa ihifadhiwe na kutumiwa katika kuondosha maovu na kuitumia kama dalili”. [Swahiyh Muslim Bisharhin Nawawy, Mj. 12, uk. 16].

 

Na Hadiyth hizi mbili za mwisho ni dalili ya kuwa kila uzushi katika dini ni bid'ah na kila bid'ah ni upotevu anayerudishiwa mwenye kufanya. Na maana ya hayo ni kuwa bid'ah katika Ibadah na Itikadi ni haramu lakini uharamu unatofautiana na aina ya bid'ah. Katika hizo ni zile ambazo ni ukafiri wa wazi kama kutufu kaburi ili kujikurubisha kwa maiti aliyezikwa na kuchinja na kuweka nadhiri ili kukadimisha kwa maiti na kuwaomba mahitaji yako, na kwa kauli zilizovuka mipaka za Jahmiyah na Mu’tazilah – na nyengine ni njia za shirki kama kujengea makaburi na Swalah na du’aa kwenye makaburi.

 

Nyingine ni Fisq za Kiitikadi kama bid'ah za Khawaarij, Qaadariyah na Murji'ah katika kauli zao na Itikadi zao zinazokwenda kinyume na dalili za kisheria. Na nyingine ni za maasia kama bid'ah za kufunga huku umesimama katika jua na kukata uume kwa ajili ya kukata matamanio ya jimai (Sh. Dkt. Saleh Fawzaan, Kitaabut Tawhiyd, uk. 101 – 102).

 

• - Na Hadiyth nyingine ni ile ya Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambayo ni kama ifuatayo: Kundi la watu watatu lilikwenda kwenye nyumba za wake wa NAbiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). wakiuliza ni jinsi gani Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifanya ibada zake, na walivyojibiwa, wakahisi kwamba ibada zao wazifanyazo hazitoshi na wakasema,

 

"Tupo wapi sisi na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Pamoja na kwamba madhambi yake yaliyotangulia na yajayo yashasamehewa." Kisha mmoja wao akasema: "Nitakuwa nikiswali usiku mzima siku zote" Na mwingine akasema: "Nitafunga swaum mwaka mzima bila kupumzika" Na wa tatu akasema: "Nitakaa mbali na wanawake na sitooa milele". Rasuli wa Allaah alivyosikia hayo akawatokea na kusema: "Nyinyi ndio wale mliosema kadhaa na kadhaa? Kwa jina la Allaah, mimi ni Mtiifu zaidi kwa Allaah na Mwenye kumcha zaidi kuliko nyinyi; pamoja na hivyo nafunga (swaum) na kufungua, nalala usiku na vilevile naoa. Hivyo, asiyetaka kufuata Sunnah (mwenendo) zangu, sio katika mimi (sio miongoni mwa wafuasi wangu)." [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Hadiyth hii inatuonya pamoja na kutoa adhabu kali kwa yeyote anayekengeuka na Sunnah na kufuata njia nyingine kwa ajili ya hawaa (matamanio) na kuzua.

 

Imaam ash-Shaafi'iy na wafuasi wake wameshikilia msimamo wa kikundi cha kwanza ambacho kinagawanya bid'ah – nzuri na mbaya. Ama Imaam ash-Shaafi'iy ana kauli mbili ambayo moja inafasiri nyingine. Naye anaona kuwa bid'ah ambayo ni mbaya ni ile ambayo haina asli katika Sheria na ile nzuri ni kuwa kile kinachozuliwa kina asli katika sheria. Ametufahamisha hayo al-Hafidh Ibn Rajab kwa kusema: “Amepokea al-Haafidh Ibn Nu’aym kwa isnadi yake kutoka kwa Ibraahiym ibn al-Junayd ambaye amesema, ‘Nimemsikia ash-Shaafi'iy akisema: Bid'ah ni aina mbili – nzuri na mbaya. Ile inayoafikiana na Sunnah ni nzuri na inayokwenda kinyume na Sunnah ni mbaya. Na akatoa dalili ya kauli ya 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu), ‘Ni’matul Bid’atu hiya’.  Na mapendekezo ya ash-Shaafi'iy katika hili ni yale tuliyoyataja kabla kuwa asli ya bid'ah mbaya ni ile ambayo haina msingi katika sheria na hiyo ni bid'akatika muono wa sheria. Ama bid'ah nzuri ni ile yenye kuafikiana na sheria. Yaani ile ambayo ina asli katika Sunnah inarudi kwake, na hiyo ni bid'ah kisheria lakini si kilugha. Imepokewa kutoka kwa ash-Shaafi'iy maneno mengine yanayofasiri haya pale aliposema, ‘Vinavyozuliwa ni aina mbili: kinachokwenda kinyume na Kitabu cha Allaah au Sunnah au Athari (maneno ya Swahaba) au Ijma’a, na hii ni bid'ah ya upotevu na vile vilivyozuliwa katika mambo ya kheri ambayo hayaendi kinyume na hivyo tulivyovitaja juu, hivyo aina hii si mbaya (yaani ni nzuri)” (Jaami‘ul-‘Uluum wal Hikam, uk. 234 – 235).

 

Hebu tuziangalie Hadiyth za pote (kundi) hili:

 

I.    Kauli ya 'Umar, ‘Neema ya bid'ah hii’, pale alipowakusanya watu nyuma ya Imaam mmoja katika Swalah ya Tarawehe. Na hii sio dalili kwa kuwepo bid'ah iliyo nzuri katika sheria, kwani 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) hakukusudia hilo bali alikuwa ametumia matumizi ya neno hilo kilugha ambayo ni pana zaidi kuliko matumizi ya kisheria. Kwa kuwa katika lugha zinaingia zote nzuri na mbaya zilizozuliwa kinyume na sheria ambapo inatumika kwa vilivyozuliwa ambazo ni vibaya. Kisha Swalah ya Tarawehe kwa jamaa ni jambo ambalo limefanywa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Hebu tuitazame Hadiyth ifuatayo ambayo imepokewa na mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) na kunukuliwa na Jama’ah isipokuwa at-Tirmidhiy.

 

"Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali msikitini (usiku wa Ramadhwaan) na watu wengi wakaswali nyuma yake. Usiku uliofuata akaswali tena na watu walikuwa wengi zaidi walioswali naye. Kisha watu wakaongezeka na kukusanyika usiku wa uliofuata lakini, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakutoka kuwaswalisha. Asubuhi baada ya Swalah akawaambia: "Hakika niliona mlichokifanya, hakikunizuia mimi kutoka ila kuwachelea msije kufaridhishiwa (hii Swalah ya Tarawehe)." (Na hicho kilikuwa kipindi cha Ramadhwaan).

 

Hivyo jamaa katika kisimamo cha usiku ni katika Sunnah wala si bid'ah. Pindi alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ile khofu ya kuwa Tarawehe inaweza kufaradhishwa iliondoka kwa sababu wahyi ulikatika, hivyo kumfanya 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) aifufue Sunnah hii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufanya iswaliwe kwa jamaa.

 

Abdur-Rahmaan Abdul-Qaariy amesema: “Nilitoka pamoja na 'Umar usiku mmoja wa Ramadhaan kuelekea Msikitini, ndani kulikuwa na watu waliokuwa wakiswali makundi tofauti. Wengine walikuwa wanaswali peke yao na wengine katika makundi madogo. 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema, ‘Nafikiri itakuwa vyema nikiwakusanya nyuma ya Imaam mmoja’. Kisha alifanya hivyo kwa kumchagua Ubayy bin Ka’ab kuwa Imaam. Kisha nilienda pamoja naye usiku mwengine na watu wote walikuwa wakiswali nyuma ya Imaam mmoja na 'Umar akasema, ‘Neema ya bid'ah hii, lakini ni bora kulala hadi sehemu ya mwisho ya usiku’. Lakini watu walikuwa wanaswali sehemu ya mwanzo ya usiku”. [Al-Bukhaariy, Ibn Khuzaymah na al-Bayhaqi].

 

Kisha ilipatikana Ijmaa' (makubaliano) ya Swahaba kuhusu usahihi wa aliyofanya 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) na hivyo Ijmaa' yao (kukubaliana kwao) ikawa ni dalili. Juu ya hayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,

 

"Shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa wangu waongofu baada yangu …" [Abu Dawuud, At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Maajah].

 

Alivyokusudia 'Umar ni ile maana ya bid'ah kilugha na wala si kisheria (Tazama, Mahabbatur Rasuul cha Abdur-Rauf Muhammad, uk. 233 na Kitaabut Tawhiyd cha Dkt. Saleh Fawzaan, uk. 103 – 104 na Iqtidhaus Swiraatul Mustaqiym cha Ibn Taymiyah, Mj. 2, uk. 589 – 590).

 

II. Ama Hadiyth ya pili ni ile ya Jariyr bin Abdillahi (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyesema: “Tulikuwa tuko mbele ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) jioni moja. Wakaja watu ambao hawakuwa na chochote isipokuwa nguo za magunia na wengine wana nguo kama joho na panga zao zikiwa zinagusa chini. Karibu wote walikuwa kutoka katika kabila la Mudhar. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifadhaika sana kuwaona, miili yao ikiwa imekwisha na njaa. Alisimama akamwambia Bilaal aadhini kwani ulikuwa ni wakati wa Swalaat kisha akaongoza Swalaat. Aliwahutubia watu kwa kusema, 

 

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَخَلَقَ مِنْهَا زَوْجَهَا وَبَثَّ مِنْهُمَا رِجَالًا كَثِيرًا وَنِسَاءً ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ

 

الَّذِي تَسَاءَلُونَ بِهِ وَالْأَرْحَامَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلَيْكُمْ رَقِيبًا

Enyi watu! Mcheni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni kutokana na nafsi moja (Aadam) na Akaumba kutoka humo mke wake (Hawwaa) na Akaeneza kutoka hao wawili wanaume na wanawake wengi. Na mcheni Allaah Ambaye Kwake mnaombana (haki zenu kwa kuunga) undugu. Hakika Allaah ni Mwenye kuwachunga daima. [An-Nisaa: 1]

 

na kisha akasoma aayah nyengine, 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ

Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Hashr: 18].

 

Baada ya kusoma aayah hizi Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaomba waliokuwepo kutoa mchango wao wa sadaka kwa dinari na dirham, nguo, ngano na tende hata ikiwa ni nusu tende. Kusikia hivi mmoja katika Answaar alileta mzigo mzito ambao ulimlemea nakisha wengine wakafuata mpaka kukawa na milima miwili ya chakula na nguo. Nikaona kuwa uso wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) unang’aa kama dhahabu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, ‘Yeyote atakayeanzisha katika Uislamu jambo zuri, atapata malipo yake na pia malipo ya wale wenye kufanya hilo bila kupunguza chochote katika malipo hayo. Hivyo hivyo yeyote atakayeanzisha jambo baya katika Uislamu, atapata dhambi ya hilo na wote wenye kumfuata watapata madhambi bila kupunguzwa kwa njia yeyote mzigo wa matendo yao mabaya” [Imesimuliwa na Muslim].

 

Hadiyth hii inatufahamisha ya kwamba makusudio ya Sunnah nzuri ni kile kitendo cha yule Swahaba ambaye alifanya haraka kutoa sadaka na hivyo kufungua mlango wa wengine kumfuata. Hivyo akawa ni ufunguo wa jambo zuri katika wema huu. Na pia sadaka ni jambo ambalo lipo katika sheria hivyo hakuzua chochote kipya. Na maana ya Sunnah nzuri inapanuka kuchanganya kila jambo ambalo ni mlango wa kheri ambalo limezungumziwa na sheria na kuhimizwa kwa sharti ya kuwa juu ya kusudio la kisheria katika kufuata. Upande wa pili, kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ‘Yeyote atakayeanzisha katika Uislamu jambo zuri’ haiwezi kuchukuliwa kuwa limeanzishwa kwa sababu kuwa ni Sunnah nzuri au mbaya haijulikani ila kwa kuafikiana au kutofautiana na sheria. Inayowafikiana na sheria ni katika Sunnah nzuri, na maana ya Hadiyth inatufahamisha hivyo. Na hupatiwa jina Sunnah mbaya kwa moja katika mawili:

 

§   Ya kwanza: Kuanzisha maasiya na uchafu kama katika Hadiyth ya mwanadamu wa kwanza katika Hadiyth ya Ibn Mas'uud (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

“Hakuna nafsi ambayo inauliwa kwa njia ya dhulma isipokuwa mwanadamu wa kwanza anapata sehemu yake ya umwagaji wa damu, kwani alikuwa wa kwanza kuanzisha mauaji” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

§   Ya pili: Kuzua katika dini na kufanya bid'ah. Lau kama ingefaa kuitumia Hadiyth kwa kuwepo bid'ah nzuri basi ingekuwa inakwenda kinyume na Hadiyth ambayo ni hoja ya jumla kuhusu bid'ah. Na zikipingana dalili za ujumla na hasa (makhsusi), haiwezi kuchukuliwa (Angalia, al-I'tiswaam, Mjalada 1, uk. 181 na baada yake).

 

III.    Ama Hadiyth ya Bilaal bin al-Haarith (Radhwiya Allaahu 'anhu) na ndani yake ina, Na yeyote anayeanzisha bid'ah ya upotevu …’ Hadiyth hii haiwezi kutumiwa kwani ni dhaifu na sababu ya udhaifu wake ni kuwa haya ni mapokezi ya Kathiyr bin Abdillaah bin Amr bin 'Awf al-Muzani, naye ni mmoja ambaye Hadiyth zake hazichukuliwi. Imaam Ahmad amesema, ‘Hadiyth zake ni za kuzua’. Na akasema al-Aajiriy: ‘Aliulizwa Abu Dawuud, akasema; alikuwa miongoni mwa waongo’. Na mfano wa hayo ndivyo alivyosema Imaam ash-Shaafi'iy. Ibn Hibbaan amesema, ‘Amepokea Hadiyth za kuzua ambazo hazifai kuweka hata katika vitabu na wala katika mapokezi’.

 

IV.  Ama kwa dalili ya ile kauli ya Ibn Mas’ud (Radhwiya Allaahu 'anhu): Yale yanayoonekana mbele ya Waislamu kuwa mazuri, yanakuwa mazuri mbele ya Allaah’. Hebu labda tuilete Hadiyth yote: Hakika Allaah Aliangalia katika mioyo ya waja, Akapata kuwa moyo wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndio bora kabisa, hivyo Akamchagua kwa nafsi Yake na kumpatia Utume. Kisha Akaangalia katika mioyo ya waja baada ya moyo wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kupata mioyo ya Swahaba zake bora katika mioyo ya waja, Akawajaalia wawe Mawaziri wa Nabii Wake. Wakawa wanapigana kwa ajili ya Dini Yake. Hivyo yale yanayoonekana mbele ya Waislamu kuwa mazuri, yanakuwa mazuri mbele ya Allaah”. Watu wengi wamechukua maneno haya kuwa ni dalili ya kuwepo bid'ah nzuri na ni hoja kwa kuwa watu wamezoea. Inaonekana kuwa athari (masimulizi ya swahaba) hii imenyanyuliwa mpaka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), japokuwa kauli hii ni mawquuf kwa Ibn Mas'uud na haiwezi kunyanyuliwa kwa hali yoyote. Na Hadiyth hii si dalili kwa yale wanayofikiria kwa sababu:

 

Ø   Kauli hii ni Mawquuf hivyo haiwezi kuchukuliwa kuwa hoja ikiwa inakwenda kinyume na nas iliyo wazi kabisa: “Kila bid'ah ni upotevu”.

 

Ø   Kusudio la hii kauli ni Ijmaa ya Maswahaba lakini laam katika al-Muslimuun si ya utekwaji katika fikra bali ni ya kipindi.

 

 

Ø   Na ikiwa maana ya Waislamu inaingia wale wasiokuwa Maswahaba, je inamaanisha kuwa wanakusudiwa wanavyuoni wao na wale ambao hawana elimu (majahili)? Hapana, bali kusudio ni watu wa ijtihadi.

 

Ø   Ikiwa kusudio ni kwa Waislamu wote – wenye elimu na wasiokuwa nayo ingekuwa ni batili kwa sababu:

 

Hii inakwenda kinyume na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

-       

“Umma wangu utagawanyika makundi 73 yote yataingia motoni ila moja pekee…”

Na mgongano hapa ni kuwa Hadiyth inatuonyesha kwa uoni wa wenye kuitumia kuwa ni hoja kuwa kila Muislamu anapata, ambayo uhakika
sivyo.

-       Na ni wazi kuwa amali ambayo inaonekana kuwa ni nzuri mbele ya watu Fulani ni mbaya kwa wengine, na hii itakuwa ni batil. Na ikiwa kusudio ni kulifanya kuwa jema kwa Waislamu wa kawaida, utafungua mlango wa uzushi katika dini.

 

VI.    Ama hoja ya kuwa kuna bid'ah nzuri ni kuandikwa kwa Qur-aan na kuandikwa kwa Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hakika katika hili hakuna jipya lililozuliwa kwani zote kuna dalili ya nyenzo za kisheria. Kuhusu kukusanywa kwa Qur-aan katika Mas-haf moja haikufanywa wakati wa Nabiy lakini Qur-aan ilikuwa inaandikwa kama ilivyokuwa ikiteremka. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiamuru kuandikwa kwa Qur-aan na alikuwa na waandishi wake maalumu kama kina Zayd ibn Thaabit, 'Uthmaan ibn 'Affan, 'Aliy ibn Abi Twaalib, na wengineo. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

“Msiandike kutoka kwangu isipokuwa Qur-aan, na yeyote aliyeandika kisichokuwa Qur-aan afute” [Imepokewa na Muslim.]

 

Nabiy hakuikusanya katika Msahafu kwa sababu Qur-aan ilikuwa bado inateremshwa na hivyo ingekuwa kila ikiteremka aayah au suwrah iandikwe tena upya. Lakini alipofariki kukawa hakuna tena wahyi mpya. Na ama kuandikwa kwa Hadiyth na elimu nyingine ni katika mlango wa kufikisha ujumbe ambalo ni jukumu la kisheria. Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alihimiza katika Hijjatul Widaa aliposema,

 

“Afikishe ujumbe yule ambaye yupo hapa kwa wengine ambao hawapo” [Al- Bukhaariy].

 

Na tena: “Nifikishieni japokuwa ni kwa aayah moja” [Al- Bukhaariy].

 

Na imethibiti katika Sunnah ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa amri, “Mwandikieni Abu Shaah” [Al- Bukhaariy].

 

Na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akisema kuwa: “Hakuna Swahaba yeyote wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ana mapokezi mengi zaidi ya Hadiyth kuliko mimi isipokuwa 'Abdillah bin 'Amr bin al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwani alikuwa akiandika na mimi sikuwa nikiandika”. Abdillahi bin 'Amr (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipatiwa ruhusa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuandika yote yanayotoka katika kinywa chake kwa kuwa maneno yake ni ya kweli na uadilifu” (Sayyid Sulaymaan Nadwi, Muhammad: The Ideal Prophet).

 

Kwa kifupi juu ya hayo tunasema kwamba, bid'ah ambazo zimetajwa kuwa ni upotevu katika shari'ah ni zile:

 

Kila kinachokwenda kinyume na Sunnah katika kauli, amali au Itikadi.

 

Kila jambo ambalo ni kujikuribisha kwa Allaah, ambalo limekatazwa na sheria.

 

Kila jambo ambalo halina dalili katika sheria, yanayohusiana na Ibadah na Itikadi.

 

Kila Ibadah ambayo haikuja isipokuwa kwa Hadiyth ambayo ni dhaifu au ya kutungwa.

 

v  Kila Ibadah ambayo imeelezewa na sheria lakini watu wakaifunga kwa mafundo au masharti Fulani kwa mfano kuiwekea sehemu na wakati au njia au idadi maalumu.

 

v  Kila jambo ambalo haiyumkiniki kufanyika isipokuwa kwa nas au kwa mfano na hapana nas (maandiko, Qur-aan na Hadiyth) inakuwa ni bid'ah, isipokuwa ikiwa imetoka kwa Swahaba.

 

Jambo ambalo linapatikana katika maandiko kutoka kwa baadhi ya wanavyuoni na hata wale wa zama zetu lakini bila dalili ya kisheria.

 

Kuvuka mipaka katika Dini (Shaykh Muhammad Naasirud Diyn al-Albaaniy, Ahkaamul Janaa'iz, uk. 242).

 

Allaah Atuelekeze kwenye Sunnah sahihi za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tuzifuate, na Atuepushe na kila bid'ah na upotevu. Aamiyn.

 

Share