Nisome Duaa Gani Ili Nipate Kibali Cha Kuishi Nchi Ya Kigeni?

SWALI:
 
asalam aykum waisalamu wenzangu,tatizo nikokuwwa nalo mimi na ninahitaji msaada kutoka kwenu alhidaya,mnifahaimishe kuwa ni dua gani au swala gani au nifanye nini hasa ili mwenyezimungu aweze kunijibu,sio siri mimi nahitaji kibali cha nchii hii ya kigeni ili niweze kufanikisha mambo yangu,    
 samahani sana alhidaaya kwa usumbufu wowote utakao kuwa umetokea na kama itakuwa kuna uwezo kana wa kuwa namba zenu naomba ili niweze kupatamajibu kwa haraka na niamue nini  cha kufanya
 
 

 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Tumepokea swali lako ambalo tumejitahidi kukujibu haraka, kwani kuna maswali mengi mno tuliyonayo, lakini kwa vile umetuomba sana na inaonyesha uko katika wahka mkubwa wa jambo hili, tumeona ni vyema kulipa kipaumbele Swali lako ili uondoshe wahka na ubakie katika iymaan thabiti kama yanavyotufunza mafunzo ya dini yetu.
 
Muislamu anapaswa kuamini kwamba kila jambo analojaaliwa, kheri au shari ndiyo Qadhwaa (mipango) ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), na aamini kwamba hali yoyote baina ya hizo kwake ni kheri, wala asitake kitu sana na kujitia katika wahka mkubwa hadi afike kujitia dhiki ya nafsi yake. Wala asichukie jambo sana linalomsibu na kuona kama ameonewa bali atambue kuwa ndani ya hiyo shari kuna kheri yake aliyopangiwa na Mola Wake. Tunapata mafunzo kutokana na Qur-aan na Hadiyth kama ifuatavyo: 
 
Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala),
 
((وَعَسَى أَن تَكْرَهُواْ شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَعَسَى أَن تُحِبُّواْ شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ وَاللّهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لاَ تَعْلَمُونَ))
 
((Na huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui)) [Al-Baqarah: 216]
 
Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
 
((عجباً لأمر المؤمن إن أمره كله له خير إن أصابته سراء شكر فكان خيراً له وإن أصابته ضراء صبر فكان خيراً له وليس ذلك إلا للمؤمن )) مسلم
((Ajabu ya hali ya Muumini kuwa mambo yake yote ni kheri; anapofikwa na furaha hushukuru na huwa kheri kwake, na anapofika na matatizo husubiri na huwa ni kheri kwake, na haiwi hivyo (sifa hiyo) ila kwa Muumini)) [Muslim]
Kwa hiyo iymaan yako ithibitishe katika hali hiyo, utaondokwa na wahka, wasiwasi na utabakia katika ridhaa ya nafsi na ridhaa ya Mola wako.
Kisha tambua kwamba ikiwa sio majaaliwa yako kupata kibali na kuishi nchi hiyo uliyoko, basi pia ni kheri kwako, pengine Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amekupangia uishi nchi nyingine ambayo itakuwa ni kheri kwako zaidi ya hiyo. Dunia ni pana na ardhi zote ni Zake Mola Mtukufu kama Anavyosema:
 
((يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ أَرْضِي وَاسِعَةٌ فَإِيَّايَ فَاعْبُدُونِ))
 
((Enyi waja wangu mlioamini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu)) [Al-'Anqabuut: 56]
Madamu ni hivyo, unatakiwa pindi utakaposhindwa kuishi hapo, bila ya kukata tamaa, utafute rizki yako sehemu nyingine, hii ni amri kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 
((هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ))  
 
((Yeye Ndiye Aliyeidhalilisha ardhi kwa faida yenu, basi tembeeni katika pande zake, na kuleni katika riziki zake)) [Al-Mulk: 15] 
 
Ufanye hivyo huku ukizidisha taqwa (ucha Mungu) kwani wenye Taqwa ndio wepesi kukubaliwa du'aa zao:
 
َ(( إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ))
 
((Allaah Huwapokelea wacha Mungu)) [Al-Maaidah: 27
 
Ama kuhusu kuomba du'aa kwa jambo mtu alitakalo, hakuna ubaya kufanya hivyo na ziko du'aa nyingi zilizothibiti katika Sunnah, tunazinukuu hapa chini baadhi yake pamoja na nyakati bora za kuomba du'aa. Lakini kwanza tunakushauri utazame kwa kina mambo yenyewe uyatakayo kabla hujamuomba Allaah, je, ni mambo ya kheri? Je, ni mambo yenye kukurengenezea ridhaa za Mola wako? Au ni mambo ya kutafuta maslaha ya kidunia na starehe zake tu? Je, kuishi kwako hapo unapotaka, ni kwa manufaa ya Dini yako au ni kutafuta hali bora tu ya kimaisha (kiuchumi) ili ustarehe kwenye dunia hii na kujifakharisha? Kama hakuna malengo yoyote ya manufaa katika Dini yako, basi ni bora urejee ulipotoka japo kwa fikra zako wahisi pana hali ngumu. Usisahau kuwa rizki yako ishakadiriwa na Mola wako, na popote utakapokuwa haitazidi kadiri ile ile uliyopangiwa. Kumbuka maneno ya Allaah Anapozungumzia mas-ala ya rizq:
Kwanza kabisa ni kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amejaalia kila kiumbe Chake alichokiumba uwezekano wa kupata rizki yake hapa ulimwenguni,
 
((وَمَا مِن دَآبَّةٍ فِي الأَرْضِ إِلاَّ عَلَى اللّهِ رِزْقُهَاوَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ))
 
((NA HAKUNA mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Allaah. Naye Anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu chenye kubainisha)) [Huud: 6]
Pia Anasema (Subhaanahu wa Ta'ala):
 
((إِنَّ رَبَّكَ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاء وَيَقْدِرُ إِنَّهُ كَانَ بِعِبَادِهِ خَبِيرًا بَصِيرًا))
 
((Hakika Mola wako Mlezi Humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona)) [Al-Israa: 30]
 
Vile vile:
 
((وَفِي السَّمَاء رِزْقُكُمْ وَمَا تُوعَدُونَ))
 
 ((Na katika mbingu ziko riziki zenu na mliyo ahidiwa)) [Adh-Dhaariyaat: 22]
  
Kama ni maombi yenye mas-ala ya kheri nay a kumridhisha Allaah, basi fanya yafuatayo:.
1. Amka usiku kuswali Tahajjud, kisha uombe sana kwani wakati huo ni   wakati wa kukubaliwa haja zetu kutokana na dalili, 
 
 
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسولالله صلى الله عليه وسلم قال:  ((ينزلربنا تبارك وتعالى كل ليلة إلى السماءالدنيا حين يبقى ثلث الليل الآخرفيقول: من يدعوني فأستجيب له؟ منيسألني فأعطيه؟ من يستغفرني فأغفر له ))
 
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani Ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah  Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
2.      Baina ya Adhaana na Iqaama ya Swalah.
3.      Inaponyesha mvua (au barafu)
4.      Kwenye kusujudu.
5.     Unapokunywa maji ya Zamzam kwa niya yake ya kuomba unachotaka.
6.     Unaposema Du'aa ya Nabii Yunus (Alayhis Salaam) nayo ni:
 
لاَ إِلَهَ إِلَّا أنْـت سُـبْحانَكَ إِنِّي كُنْـتُ مِنَ الظّـالِميـن
 
"Laa Ilaa Illa Anta Subhaanak Inniy Kuntu Minadhwaalimiyn"
“Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, kutakasika ni Kwako.  Hakika mimi ni miongoni mwa waliodhumu nafsi zao”
 
7.     Unaposema Du'aa ya:
 
 اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْأَلُـكَ بِأَنَّ لَكَ الْحَـمْدُ لا إِلـهَ إِلاّ أَنْـتَ وَحْـدَكَ لا شَـريكَ لَـكَ المَنّـانُ يا بَديـعَ السَّمواتِ وَالأَرْضِ يا ذا الجَلالِ وَالإِكْـرام، يا حَـيُّ يا قَـيّومُ إِنِّـي أَسْأَلُـكَ الجَـنَّةَ وَأَعـوذُ بِـكَ مِنَ الـنّار
 
Allaahumma Inniy As-aluka Bianna Lakal-Hamdu Laa ilaaha illa Anta Wahdaka laa shariyka Lakal-Mannaanu Yaa Badiy'as-Samaawati wal-Ardhwi Yaa Dhal-Jalaali  Wal Ikraami Yaa Hayyu Yaa Qayyuum Inniy As-alukal-Jannata wa A'uudhu Bika Minan-Naari.
 
“Ewe Allaah hakika mimi nakuomba, kwa vile sifa njema zote ni Zako, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, hali yakuwa Pekeyako, huna mshirika, mwingi wa kuneemesha.  Ewe Mtangulizi (muumbaji) wa mbingu na ardhi (bila kuwa na mfano kabla), Ewe mwenye Utukufu na  ukarimu, Ewe Uliye hai mwenye kusimama kwa dhati  Yako, hakika mimi nakuomba pepo, na najilinda  Kwako kutokana  na moto”
Mtu mmoja aliomba du'aa hii kisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia Maswahaba: ((Je, mnajua kaomba na nini?)) Wakasema: "Allaah Na Mjumbe Wake Wanajua zaidi". Akasema: ((Naapa kwa Yule Ambaye Nafsi yangu imo Mikononi Mwake, amemuomba Allaah ('Azza wa Jalla) kwa jina ambalo akiombwa nalo, Anajibu na Akiulizwa Hutoa)) [Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ahmad, Al-Bukhaariy katika Al-Adabul-Mufrad, At-Twabaraaniy na Ibn Mandah katika Tawhiyd (44/2, 67/1, 70/1-2) ikiwa na isnaad Swahiyh]
 
8.      Saa katika siku ya Ijumaa (na aghlabu ya kauli ni baina ya Swalah ya Alasiri na Magharibi)
9..      Du'aa unapofunga (Swawm)
10.    Du'aa baada ya Swalah (baada ya tashahhud kabla ya kutoa salaam).
 
Muhimu zaidi ni kuanzia Du'aa zako kwa kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kisha kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kuanza du'aa na kumalizia.
 
Tunakuombea tawfiyq kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama jambo hilo uliombali lina kheri nawewe, na kama hukujaaliwa basi tunatumai utaridhika na Qadhwaa ya Mola Wako kwa kuamini kuwa kuna kheri yake.
 
Usitusahau na sisi katika du'aa zako Allaah Atufanyie wepesi na Atutakabalie hizi amali kwa ajili Yake.
 
Na Allaah Anajua zaidi.
Share