Maulidi: Ameweka Nadhiri ya Kusoma Maulidi Kisha Katambua kuwa Ni Bi'dah Afanyeje?

 

Ameweka Nadhiri ya Kusoma Maulidi Kisha Katambua kuwa Ni Bi'dah Afanyeje?

 

www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Asalamu alaykum,

Dada yangu aliweka nadhiri kusoma maulidi pindi akizaa mtoto wa kike. Baada ya kuzaa mtoto wa kike, kashukuru lakini alikuja kusikia kuwa maulidi ni jambo la uzushi, hivyo akaingiwa hofu kufanya. Lakini mtoto wake heshi kuumwa umwa, na watu wa nyumbani wamemuambia kuwa lazima atimizie nadhiri yake japo kama jambo la uzushi. Naomba tafadhali mashekhe wa Alhidaaya watujulishe la kufanya, je ni kweli aendelee kufanya maulidi? Au afanye nini?

Nitashukuru kupata majibu yenu haraka kumsaidia dada yangu. 

 

JIBU

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Mwanzo kabisa tungependa kutoa maana ya nadhiri ili ifahamike vyema kabla ya kulijibu swali lako.

 

Maana ya nadhiri kilugha ni ahadi, nayo ni kujaalia mwanadamu ahadi ya wajibu kwa nafsi yake. Ama ki-Shariy’ah, ni kujilazimu kwa mtu nafsi yake kwa kitu kinachomkurubisha au utiifu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na si wajibu kwake akalifanya kuwa wajibu juu yake kwa lafdhi yenye maana hiyo.

 

 

Ahadiyth sahihi zimekuja katika mas-ala ya nadhiri kuwa haifai nayo imekatazwa. Hivyo, ‘Ulamaa wengi wamesema ni makruhu, lakini inapotokea kuwekwa basi inakuwa wajibu kuitekeleza.

 

Amesema Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuwekwa nadhiri akasema: “Hakika hiyo hairudishi chochote, lakini inatoa kitu kutoka kwa bakhili” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Pia imepokewa kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msiweke nadhiri, kwani nadhiri haifadishi chochote na Qadar, hakika hiyo inatoa kwayo kutoka kwa bakhili” [Muslim, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ahmad]

 

Qur-aan na Sunnah zinatupatia dalili kuwa ni wajibu kutekeleza nadhiri katika mambo ya utiifu na kuwasifu wanaotekeleza nadhiri zao. Anasema Aliyetukuka:

 

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ ﴿٢٩﴾

Kisha wamalize ‘ibaadah zao; wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale. (Al-Ka’bah) [Al-Hajj 22: 29]  

 

Na katika kuwasifu wanaotekeleza nadhiri, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِنَّ الْأَبْرَارَ يَشْرَبُونَ مِن كَأْسٍ كَانَ مِزَاجُهَا كَافُورًا﴿٥﴾

5. Hakika Waumini watendao wema kwa wingi watakunywa katika vikombe vya mvinyo mchanganyiko wake ni (kutoka chemchemu iitawayo) kaafuwraa.

 

عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا عِبَادُ اللَّـهِ يُفَجِّرُونَهَا تَفْجِيرًا﴿٦﴾

6. Chemchemu watakayokunywa humo waja wa Allaah, wataibubujua kwa wingi.

 

يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا﴿٧﴾

7. Wanatimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea kwa upana. [Al-Insaan 76: 5-7]

 

Na Anasema tena (Subhaanahu wa Ta’aalaa): 

 

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ ۗ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴿٢٧٠﴾

270. Na chochote mtoacho au mkiwekacho nadhiri, basi Allaah Anakijua. Na madhalimu hawana wa kuwanusuru. [Al-Baqarah 2: 270]

 

 

Nadhiri zimegawanyika sehemu mbili. Nazo ni:

 

1-Kuweka nadhiri kumtii Allaah:

 

Mwenye kuweka nadhiri hii ni juu yake kujilazimisha kutekeleza kwa kadri ya uwezo na kiwango anachoweza. Katika kuweka nadhiri aina hii basi aweke jambo au amali ambayo ataweza kufanya kwa usahali asiweke jambo gumu ambalo anajua hataliweza kulifanya. Akifanya hivyo itabidi avunje nadhiri yake. Dalili ni kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akiwa katika mashaka. Akauliza: “Nini hii?” Akaambiwa: “Ameweka nadhiri ya kutembea mpaka nyumbani”. Akasema: “Hakika Allaah ni Mwenye Shani ni Mkwasi kwa yeye kuiadhibu nafsi yake”. Kisha alimuambia apande kipando [al-Bukhaariy na Muslim]

 

2-Kuweka nadhiri ya kufanya maasiya:

 

Mtu anapoweka nadhiri ya kufanya maasiya kama kunywa pombe, kuzini, kuua, kuchinja kaburini, kufanya juhudi kutembelea Msikiti mbali na ile mitatu, kutofanya uadilifu baina ya watoto, kutekeleza bid‘ah kama kusoma Mawlid na kadhalika. Hii ni aina ua nadhiri ambayo haifai kutekelezwa bali ni haraam. Dalili ni Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anayeweka nadhiri ya kumtii Allaah basi Amtii. Na yeyote anayeweka nadhiri kumuasi basi asimuasi” [al-Bukhaariy, Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah]

 

Imepokewa pia kwa ‘Imraan bin Haswiyn (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana kutekeleza nadhiri katika maasiya, wala kutekeleza nadhiri kwa asichomiliki mja au mwanadamu” [Muslim, Abu Daawuwd, an-Nasaa’iy na Ibn Majaah].

 

Kwa sababu nadhiri imewekwa kufanya kitendo ambacho hakifai kisheria ni wajibu ya mweka nadhiri asitekeleze nadhiri yake ba ni juu yake kutoa kafara. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hapana nadhiri katika maasiya, na kafara yake ni kafara ya yamini” [Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah na imesahihishwa na Imaam Al-Albaaniy).

 

Kafara la kula yamini kisha kutotekeleza imetajwa kwa mpangilio katika Qur-aan Tukufu:

 

لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّـهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ وَلَـٰكِن يُؤَاخِذُكُم بِمَا عَقَّدتُّمُ الْأَيْمَانَ ۖ فَكَفَّارَتُهُ إِطْعَامُ عَشَرَةِ مَسَاكِينَ مِنْ أَوْسَطِ مَا تُطْعِمُونَ أَهْلِيكُمْ أَوْ كِسْوَتُهُمْ أَوْ تَحْرِيرُ رَقَبَةٍ ۖ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ ۚ ذَٰلِكَ كَفَّارَةُ أَيْمَانِكُمْ إِذَا حَلَفْتُمْ ۚ وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٨٩﴾

89. Allaah Hatokuchukulieni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini Atakuchukulieni kwa (kuvunja) viapo mlivyoapa kwa niyyah mlioifunga thabiti. Basi kafara yake ni kulisha maskini kumi chakula cha wastani mnachowalisha ahli zenu, au kuwavisha nguo, au kuacha huru mtumwa. Lakini asiyeweza kupata (katika hayo), basi afunge Swiyaam siku tatu. Hiyo ndio kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini yamini zenu (msiape kila mara). Hivyo ndivyo Allaah Anavokubainishieni Aayaat (na hukmu) Zake ili mpate kushukuru. [Al-Maaidah 5: 89]

 

Mpangilio wa kafara uliowekwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni  kama ufuatao kwa utaratibu huo:

 

Kwanza: Kuwalisha masikini kumi chakula cha wastani, akitoweza;

 

Pili: Kuwavisha nguo idadi hiyo ya masikini, akitoweza; 

 

Tatu: Kuacha mtumwa huru. 

 

Nne:  Ikiwa hakuweza haya ndio itabidi afunge siku tatu (3).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share