Mirathi - Mama Alipofariki Alitengana Na Mumewe – Kaacha Watoto Watano

 

SWALI:

 

Namshuru Allah, mwingi wa rehema na mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na ndogo ndogo na natakia reheme Mtume wetu mtukufu, Muhamaad (SAW). Baada ya haya, swali langu ni je, Kama mama amefariki na ameacha watoto watano, wakike wawili (mmoja ana mme mmoja hana) na wakiume watatu, je mali aliyoiacha inatakiwa kugawiwaje? Wakati anapatwa na mauti alikuwa ametengana na mumewe kwa talaka ila mumewe bado yu hai. Je mirathi inatakiwa iweje?

 

Mwenyezi Mungu awabariki. Ameen

 


 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa muulizaji swali. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awape subira wafiwa na wawe ni wema kwa mama yao hata baada ya kufa kwa kumuombea du‘aa asamehewe na Allaah na awekwe mahali pema pamoja na wema.

 

Hakika ni kuwa tutachukua dhahiri ya swali lenyewe kuwa mama huyo hakuwa na wazazi. Mwanzo ni kuwa mtalaka wake hatakuwa na wirathi kwani aliyekufa hakuwa mkewe wakati huo. Hivyo, watakaorithi ni watoto wake tu – mtoto wa kiume atapata sehemu mbili ya mtoto wa kike. Mafungu yanakuwa sawa kwa watoto wakiwa wameoa, wameolewa, hawajaoa au kuolewa.

 

Kwa hiyo, kila mtoto wa kiume atapata robo (¼) ya mali yalioachwa na aliyefariki ilhali kila msichana atapata thumuni (1/8). Huo ndio mgao wa warithi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share