Safari Isiyokuwa Na Mashaka Na Ya Muda Mfupi Anaweza Kufunga (Swawm) Ikiwa Anaweza?

 

SWALI:

 

 

Assalam alaykum warahmatullah wabarakat. Swali langu linahusu swaum safarini, moja: inajuzu kufunga ukiwa safarini, kama ntaweza? Mfano: safari ya ndege, gari, nk..., ambazo sio safari za siku nzima?

 


JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Inategemea na safari yenyewe, ikiwa ni hali kama ulivyotaja kuwa safari si ndefu na ya mashaka, na pia vile mtu anavyopenda kuamua anaweza kufunga akipenda na anaweza kula akipenda. Dalili ni Hadiyth zifuatazo:

 

عن عائشة أن حمزة بن عمرو الأسلمي سأل رسول الله صلى الله عليه وسلم عن الصوم في السفر وكان يسرد الصوم فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم ((إن شئت فصم وإن شئت فأفطر)) البخاري و مسلم

 

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwamba Hamza bin ‘Amru Al-Aslamy ambae alikuwa akifunga sana, alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuhusu Swawm katika safari, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema ((Ukipenda funga na ukipenda kula). [Al-Bukhaary na Muslim]

 

Pia,

عن أبي سعيد الخدري رضي الله عنه قالغزونا مع رسول الله صلى الله عليه وسلم لست عشرة مضت من رمضان ، فمنا من صام ومنا من أفطر ، فلم يعب الصائم على المفطر ، ولا المفطر على الصائم  - مسلم

Kutoka kwa Abu Sa’iydil-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Tulikwenda safarini katika vita  pamoja na Mtume Swalla-Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) siku ya kumi na sita Ya Ramadhaan. Miongoni mwetu walikuweko waliofunga na wengineo walioukula,na waliofunga hawakulaumu walokula. [Muslim]

 

Lakini fursa ya kutokufunga tumepewa tuitumie hivyo ni kheri zaidi kutumia fursa kupata fadhila za kutekeleza Sunnah na usimulizi ufuatao unapendekeza hivyo:

 

عن جابر بن عبدالله أن رسول الله صلى الله عليه وسلم رأى رجلا يظلل عليه والزحام عليه فقال : ((لَيْسَ مِنَ الْبِرِّ الصِّيَامُ فِي السَّفرَ))  صحيح أبي داود    

Kutoka kwa Jaabir bin 'Abdillaah ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuona mtu akiwa amewekwa chini ya kivuli hali yake taabani baada ya kudhoofika kutokana na Swawm akamwambia: ((Si katika wema (ucha Mungu) kufunga katika safari)) [Swahiyh Abiy Daawuud]

 

Ikiwa hutofunga itabidi ulipe siku hiyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share