Nitakuwa Nimelogwa? Je, Kutumia Kombe Inafaa?

 

 

Nitakuwa Nimelogwa? Je, Kutumia Kombe Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalamu Alaykum.

 

Alhamdulillah kwa kunipa uhai na afya njema. Nawashukuruni na nyinyi munaotusaidia kwa ajili ya Allaah-inshAllaah atakulipeni mema.

 

Suali langu ni:- Mimi nimeolewa na mume ambaye aliwahi kuoa na kazaa watoto wawili wanawake, baada ya mgogoro mkubwa kati yao na wazee wakaamua kuachana na mwanamke mwenyewe ndiye aliyedai talaka.

 

Baada tu ya kuolewa mie, yule mwanamke akawa kila siku anafanya fujo eti anamataka mume wangu kwa nguvu wakati ameshaachika. Nilichukua uja uzito na haikuchukua muda ile mimba ikatoka, nikasafishwa. Baada ya mwezi nikawa naumwa tena na tumbo nikaambiwa kua ile mimba ya mwanzo haikusafishwa uzuri ikabidi nisafishwe tena. Kwa bahati nilikwenda sehemu kutembea na nikakutana na bibi mmoja wa kiislamu (hanijui simjui) ni mgeni kwangu na kuniuliza juu ya matatizo yangu na alikua akinitajia moja baada ya moja kuhusu mume wangu, mie na yule mwanamke aliyeachwa.

 

Na yote alokua akiniambia ni kweli na Allaah ni shahidi wa hayo. Nilimdadisi mengi yule bibi kwani nilishangaa kajuaje? Akanijibu kuwa yeye ana ruhani na anasoma sana Qur an na anawatibu watu kwa Qur an. Bibi akanieleza kuwa yule mwanamke aliyeachwa amekufanyiwa shirki ili usizae, kwa hivyo nitakupa kombe ili utumie na uepukane na janga hilo. Na kwa kweli hakutaka malipo (pesa) yoyote. Mie nikachukua kombe na bado sijaanza kutumia, nitaanza kutumia wiki ijayo In shaa Allaah.

 

Jee, waalimu wetu mnanishauri nini juu ya hili? Naomba jibu kwa haraka iwezekanavyo kabla sijaanza kutumia hizi dawa. Shukran

 

Wa ‘Alaykumus Salaam

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Na tunaomba radhi kwa kuchelewa kujibu swali lako kutokana na kuwa kuna maswali mengi sana yaliyokuwa yametangulia kabla ya lako.

 

Mwanzo tungependa kukumbushana kuwa mas-ala ya ghaibu hakuna ayajuaye ila Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na kwako msomaji baadhi ya dalili katika hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ 

Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu.  [Al-An'aam: 59].

 

Pia,

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ 

Sema: Hakuna katika mbingu na ardhi ajuaye ghayb isipokuwa Allaah. [An-Naml: 65]

 

Na Anasema tena:

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا﴿٢٦﴾

Mjuzi wa ghayb na wala Hamdhihirishii yeyote ghayb Yake. [Al-Jinn: 26].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuelezea kuwa hata Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa wa aalihi wa sallam) hajui mas-ala ya ghayb, pale Aliposema:

 

قُل لَّا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ 

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Sikuambieni kuwa mimi nina hazina ya Allaah; na wala kwamba najua ya ghayb;.. [Al-An'aam: 50].

 

Pia,

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۚ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ ۚ 

Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa yoyote wala dhara yoyote isipokuwa Apendavyo Allaah. Na lau ningekuwa najua ya ghayb, bila shaka ningelijikithirishia ya khayr, na wala lisingelinigusa ovu. [Al-A'raaf: 188].

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuarifu kuwa hata majini (maruhani) nao hawajui kuhusu ghayb, kama alivyosema:

 

فَلَمَّا قَضَيْنَا عَلَيْهِ الْمَوْتَ مَا دَلَّهُمْ عَلَىٰ مَوْتِهِ إِلَّا دَابَّةُ الْأَرْضِ تَأْكُلُ مِنسَأَتَهُ ۖ فَلَمَّا خَرَّ تَبَيَّنَتِ الْجِنُّ أَن لَّوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ الْغَيْبَ مَا لَبِثُوا فِي الْعَذَابِ الْمُهِينِ ﴿١٤﴾

Basi Tulipomkidhia mauti, hakuna kilichowajulisha kifo chake isipokuwa mdudu wa ardhi akila fimbo yake. Basi alipoanguka ikawabainikia majini kwamba lau wangelikuwa wanajua ya ghayb, basi wasingebakia katika adhabu ya kudhalilisha. [Sabaa: 14].

 

Kuhusu kuwa na jini au rohani kama anavyosema huyo mwanamke ni jambo ambalo linawezekana. Na viumbe hawa ambao hawaonekani hutumika katika kumpasha habari mwanaadamu. Mara nyingi habari zao ni za uongo kwani wao wana tabia hiyo katika habari wanazotoa 99% zinakuwa ni za uongo na 1% ndio kweli. Hivyo, huyo bibi si mwema na wewe kama Muislamu hufai kutumia kombe hilo.

 

Nasaha tunayokupa ni kuwa umtafute Shaykh, mcha wa Allaah ambaye atakutibu kufuata ile njia ya Sunnah ya kukusomea Qur-aan (Ruqyah) ambayo ni dawa. Na kawaida waalimu hawa huwa hawachukui chochote. Na tanbihi ni kuwa ikiwa utakwenda kwa wale wanaojulikana au kujiita ni waalimu wakaanza kusoma kisomo kisichoeleweka njia hiyo pia itakuwa haifai.

 

Na kuhusu kombe, ingawa kuna baadhi ya Maulamaa wamesema inafaa kwa kudai kuwa Swahaba Ibn ‘Abbaas alitumia, lakini Qauli yenye nguvu na Maulamaa wengi wanapingana nayo kwa kutokuwa na ushahidi sahihi wa hili na pia kutofundishwa njia hiyo na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alifundisha njia zote za kutibu au kujikinga na uchawi, husda, kijicho, na hayo ya marohani n.k. kwa kutufundisha du’aa mbalimbali na Aayah za Qur-aan ambazo baadhi yake tunakutajia chini. Hivyo, ni bora uachane na hayo mambo ya kombe Ambayo yana utata na ufuate zile njia sahihi zilizothibiti.

 

Baadhi ya wanaojiita Mashekhe na Maaalimu wanatumia njia hizo kula pesa za Waislam.

 

Njia nyengine ni kuwa na muda wa wewe mwenyewe kusoma zile Aayah na Suwrah ambazo ni kinga kwa Muislamu kama alivyotufundisha Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama Suwrah Al- Ikhlaasw, Al-Falaq na An-Naas asubuhi na jioni. Na Suwrah Al-Baqarah Aayah za 1-5, 255–257 na 284–286. Na pia kusoma Qur-aan  sana.

 

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akupatie shifaa kwa njia iliyo ya sawa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share