Anaambiwa Nani Aayah: قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ

 

Anaambiwa Nani Aayah

 

قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ﴿٨١﴾

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleykum,

Alhamdulillah kua Allah mtakatifu ametupa uzima na uhai mpaka sasa. In shaa Allaah tuwe wenye kuongoka na nyinyi mlipwe wema kwa kutusaidia. Kwenye Suuratu-zzukhruf Aya ya 81: "Sema: Ingeli kuwa Rahmani ana mwana, basi mimi ningeli kuwa wa kwanza kumuabudu."

 

Je haya maneno alikua anaambiwa Nabiy Issa awambie watu au ilikua anaambiwa nani, kwani katika aya za juu zinaelezea kuja nabii Issa alayhi ssalaam na uongofu kutoka kwa Allah subhaanahu wataala. Kama anaambiwa Nabiy Issa itanisaidia kuwathibitishia rafiki zangu wa kikiristo kua Nabiy Issa si mwana wa Allaah

Jazaakumullahu khair.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Hiyo ni Aayah katika Suwrah Az-Zukhruf 

 

قُلْ إِن كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدٌ فَأَنَا أَوَّلُ الْعَابِدِينَ﴿٨١﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Kama ingelikuwa Ar-Rahmaan Ana mwana (kama mnavyodai), basi mimi ningekuwa wa mwanzo katika waja (Wake). [Az-Zukhruf: 81]

 

Kabla hajutaelezea Aayah hiyo, labda tuanze kwa kufahamisha vigawanyo vya Suwrah hii ya Az-Zukhruf. Miongoni mwa dondoo ni kuwa:

 

  1. Imeteremshwa Makkah.
  2. Imeelezea misingi ya Itikadi na Iymaan ya Kiislamu. Iymaan ya Umoja Wake, risala, ufufuo na jazaa.
  3. Kuthibitisha machimbuko ya Wahyi na ukweli wa hii Qur-aan.
  4. Kuonyesha dalili ya uwezo Wake, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
  5. Imeelezea maadili ya kijahili katika jamii kwa mambo ya khurafa na uabudu wa masanamu. Walikuwa wanawachukia mabinti, pamoja na kuwa walimchagulia Allaah kuwa na mabanati kwa ujinga na upumbavu wao. Kwa ajili hiyo wakadai kuwa Malaika ni binti wa Allaah. Kwa hiyo ikawarudisha kwa maumbile kuwa Allaah hana watoto.
  6. Kueleza miujiza ya Da'wah ya Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam), ambaye mushirikina wanadai kuwa wametokana na kizazi chake. Aayah zikatufahamisha kuwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) alikuwa mbali na kuabudu masanamu.
  7. Kisha ikaondoa ile fikra kuwa Nabiy mteule ni lazima awe na jaha na utukufu pamoja na kuwa tajiri. Aayah zikaja kufahamisha kuwa msingi wa utume si jaha wala utajiri.
  8. Kutajwa kwa kisa cha Muusa na Fir’awn, kufahamisha ile hakika ya hapo awali kuwa kuwa jaha na utajiri si msingi wa utume. Fir’awn alijifakhirisha kwa Muusa kwa ufalme wake na hivyo walivyofanya Ma-Quraysh, lakini natija itakuwa ni maangamivu.
  9. Kutajwa kwa Nabiy 'Iysaa (‘Alayhis-salaam) kama jawabu la mushrikina kuwa yeye hakuamrisha aabudiwe bali yeye alifundisha Uislamu sahihi kwa watu wake.
  10. Suwrah imehitimsha kwa kubainisha baadhi ya mambo ya Akhera na mateso yake. Pia kubainisha hali za waovu, watakavyoteseka katika Jahanamu.

Hizi ni baadhi ya dondoo kuhusiana na Suwrah hiyo.

 

Ama tukirudi katika swali lako ni kuwa maana ya Aayah hiyo ni jawabu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) aliyepewa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwajibu watu wake Ma-Quraysh waliokuwa mushrikina. Na maana yake ni kuwa lau Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Angekuwa na mtoto kama mnavyodai basi mimi (Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ningekuwa wa kwanza katika waja Allaah kukanusha madai hayo. Kwa maana nyingine ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hana mtoto kabisa wala Hastahiki kuwa na sifa hiyo.

 

Bali Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَـٰنُ وَلَدًا ﴿٨٨﴾

Na wamesema: “Ar-Rahmaan Amejifanyia mwana.”

لَّقَدْ جِئْتُمْ شَيْئًا إِدًّا ﴿٨٩﴾

Kwa yakini mmeleta jambo kuu ovu na la kuchukiza mno! [Maryam: 88-90]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share