Anaona Kinyaa Kupokea Mkono Anaposalimiwa Kwa Sababu Ya Uchafu

SWALI:

 

suala langu la pili kuhusu utulivu ndani ya swala tunakuta wenzetu wengine wanakuja hali ya kuwa wanajikuna kila wakati na katika kujikuna kwao unafikia unakuwa unaona kinyaa kwani kuna baadhi ya watu ni kawaida yao wanafikia mpaka wanajichokoa pua na kutoa uchafu ndani ya swala halafu baada ya swala anakupa mkono kwa kukusalimia sasa suala langu linakuja mimi ninatakiwa nimsalimie kwa kurejesha mkono au nini nifanye na kama ninaona kinyaa sitakuwa mkosa kwa ALLAH kuwa labda nina kiburi au kitu kama hicho ninaogopa adhabu za ALLAH ninawaombeni ndugu zangu munisaidie kwa hili na niweze kuchapisha kwa kuwaelimisha wenye mtindo kama huu ASSALLAM ALLAIKUA WARAHMATULLAH WA BARAKATU


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuona kinyaa kusalimiana kwa mkono. Hakika hilo ni jambo la kimaumbile kabisa lakini, bora tueleze ili kila mmoja aweze kuelewa.

 

Uislamu umeweka nidhamu yake ambayo inatakiwa ifuatwe kikamilifu na kila anayejiita Muislamu. Katika hilo ni usafi, na Muislamu ni lazima awe msafi. Kwa ajili ya hiyo ndio Allaah Aliyetukuka Akamuagizia Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"Na nguo zako uzisafishe" (74: 4).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Uislamu ni usafi, basi jisafisheni kwani haingii Peponi ila aliye safi".

Na tena:

"Hakika Allaah Aliyetukuka ni Mzuri na Hakubali ila zuri" (Muslim).

 

Uzuri umechanganya mambo mengi sana mojawapo ikiwa ni usafi na unadhifu.

 

Kutoa uchafu katika pua kisha bila ya kusafisha mikono ni hatari kwani sehemu hiyo ya pua inakusanya viini vingi vya ugonjwa na hivyo kumweka katika hatari yule unayemsalimia na yeye mwenyewe pia. Jambo la busara ni kumpatia nasaha huyo kaka kuhusu unadhifu na usafi ili asiwe ni mwenye kujiingiza katika matatizo.

 

Usiwe ni mwenye kukataa tu bali mnasihi na kumwelezea Uislamu unasema nini kuhusu hilo kwa njia nzuri na ya busara bila kumkemea wala kumkejeli. Kuhusu hilo, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"Dini ni nasiha'. Tukauliza kwa nani, akajibu: 'Kwa Allaah, na Kitabu Chake, na Mtume Wake, na kwa viongozi wa Waislamu na watu wa kawaida'" (Muslim, Abu Daawuud na an-Nasaa'iy).

 

Kwa kufanya hivyo utakuwa umefanya ulinganizi na utalipwa na Allaah Aliyetukuka kwa hilo. Twakuombea kila la kheri.

  

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share