Kumwita Mtu Muhammad, Kuliandika Na Kutamka Kama Linavyoandikwa Ni Makosa?

SWALI:

A/alaykum              

Je: Sheghe inakubalika mtu kumwita mtoto wake jina kama (Muhammad).

Na wakati sisi Waislamu tunapotamka jina la Mjumbe (Allaah s.w.) Ni lazima tutangulize na (s.a.w) Ispokua nafahamu tu kua unaweza kumwita mtoto jina kama. Ahmad, Ahmed, Muhammed. Kwa sababu unaweza ukaa ukamsikia mtu anamtaja Muhammad basi wewe ukajibu (s.a.w) kumbe anatajwa tu mtoto wa mtu. kwa hiyo hii mimi imenitia wasiwasi sana. Naomba munieleweshe. kama inakubalika. M/Mungu awabarik na kazi hii.

 Waasalam alaykum.

 


JIBU

:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa ndugu aliyeuliza swali hili kuhusu kupeana majina. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia sana kuwapatia watoto wetu majina yaliyo mazuri.

Katika hili nalo la mtu kupatiwa jina la Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Mtume mwenyewe hakutuacha kiholela bali alitupatia muongozo muafaka kabisa. Abu Wahb al-Jushamiy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Jiiteni majina ya Mitume. Na majina yapendezayo zaidi kwa Allaah ni ‘Abd-Allaah na ‘Abdur-Rahman” (Abu Daawuud na an-Nasaa’iy). Kulingana na Hadiyth Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), anatueleza kuwa tunafaa sisi kuwaita watoto wetu majina ya Mitume, naye alikuwa miongoni mwao.

Kisha ni hakika isiyopingika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hapati kosa isipokuwa hulirekebisha kwa njia kuwa halitorudia tena. Lau litarudia basi walinganizi wa haki watakuwa msitari wa mbele kabisa kulipinga hilo na kuelezea ukweli huo. Katika kipindi alichokuwa hai Abu Bakar asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipata mtoto na kumuita jina la Muhammad bila ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupinga hilo na wapo Maswahaba wengi waliokuwa na jina hilo.

Katika waliozaliwa baadaye ni mtoto wa ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyejulikana kwa jina hilo. Baada ya hapo tunapata Maimamu waliobobea katika elimu wakiitwa majina hayo kama Muhammad Idriys ash-Shaafi‘iy, Muhammad bin ‘Abdul-Wahhaab na wengineo 

Kwa hiyo hapana makosa yoyote kumuita mtoto kwa jina hilo.

Na itikadi kuwa ukimwita mtoto Muhammad kama inavyoandikwa, basi utakuwa umemfananisha na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni itikadi potofu kwa kuwa haina dalili ya kisheria wala ya kimantiki! Na kusema kuwa Muhammad ni jina tu la Mtume, na kama utamwita mtu basi ubadilishe baadhi ya herufi au matamshi, kwa kuandika Muhammed au Mohamed au kama hivyo, basi huko kunahitaji dalili na si hisia za watu tu zisizo na asli yoyote.

Kwa upande mwengine, tukichukulia mantiki hiyo ya baadhi ya watu  wanaoona hivyo, basi tutaona pia wao kuyageuza hayo majina, pia kutakuwa ni vibaya kwa sababu watakuwa wameharibu jina tukufu alilokuwa nalo Mtume wetu kipenzi (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Hivyo, ingelikuwa bora kwao kutokea wanapopata watoto wasiwaite jina hilo ikiwa hofu yao na hisia zao zinawatuma kuwa mtoto mwenye jina hilo ukimtukana au ukimgombesha, utakuwa ni sawa na kumtukana Mtume! Kwa nini wewe umpe mtoto jina kisha jina hilo hilo uligeuze na ulipindue uzuri wake wakati ulikuwa unaweza kumwita jina lingine lolote ambalo lisingekutia wasiwasi wa kumgombesha au kumtukana mwenye jina hilo pindi afanyapo makosa?

Kwa hiyo ndugu yetu unaweza kumuita mwanao au mtu yeyote Muhammad na hakuna tatizo, na usilikate jina hilo tukufu na kulibadilisha herufi au kulifupisha kama wanavyofanya wengine wanaojiita Muddy au Eddy n.k., na kufanya hivyo haipendezi, bali inachukiza kwa sababu pia ni katika kuwaiga makafiri ambao ndio wenye tabia hizo, au pia kutaka kufanana nao kwa kujiita hivyo!

Na kusema kuwa ukisikia jina la Muhammad linaitwa unaweza kumswalia ukidhani ni Mtume, ukweli ni kwamba ikiwa umefanya hivyo kwa nia hiyo na hali ulikuwa hujui, basi utapata ujira wa hilo, lakini jua kuwa linapoitwa au kutamkwa jina hilo inategemea wapi upo, kama kuna Muhammad hapo n.k. Kama upo kwenye mawaidha au mhadhara, bila shaka inaweza kuwa ni Mtume ndiye mwenye kutajwa, na ukiwa nyumbani au chumbani au barabarani na mtu anaita, basi bila shaka huyo muitwa atakuwa ni Muhammad asiye Mtume, na utaweza kuyapambanua hayo kirahisi sana ndugu yetu.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share