Yuko Katika Dhiki Kwa Sababu Posa Zake Zinavunjika, Wadogo Zake Wameolewa Yeye Bado,

 SWALI:

  

Assalam ALeikum Warahmatullahi Wabarakatu.

 

Naomba sheikh nisaidie kwa kunipa dua au mawaidha itakayoburudisha roho yangu mimi nahisi dhiki na huku nakuandikia mimi machozi yananitoka kwa uchungu hata sina la kufanya zaidi ya kumsujudia mola wangu subhana wataala na kumuomba. Mimi ni msichana wa miaka 30 roho yangu inaniuma kuona wenzangu wanaolewa mimi nipo nikisubiri mdogo wangu kishaolewa ana mtoto na inshallah kuna mwingine posa yake mashallah imesimama.

 

Mimi najiuliza nimekosa nini ila nakubali ni mitihani ya mola wangu subhana wa taala, na zaida kinachoniumiza mimi posa zangu zilizotangilia zikusimamiwa kama za wenzangu na hii ndio inanifanya nilie kila siku. Lakini inshallah mungu yupo hamtupi mja wake kuna siku na saa atanipa. Naomba nijibu kwa kutumia email yangu hapo juu. Shukran na jazakallah kher.


 

 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuvunjika kwa posa zako zinapokuja. Hakika ni kuwa dunia hii tunayoishi ni sehemu na mahali pa mitihani. Na kila mwanadamu anapata mitihani aina yake. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuarifu kuwa:

 

 “Allaah Akiipenda kaumu basi huitia katika mitihani”. 

 

 

Na juu ya mitihani tofauti Allaah Aliyetukuka Anatuarifu:

Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanaosubiri, Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Allaah, na kwake Yeye hakika tutarejea” (2: 155 – 156).

 

Na huu ndio mwendo na Sunnah ya Allaah Aliyetukuka katika maisha ya hapa duniani

, pale Aliposema:

 

Hii ni ada ya Allaah iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Allaah (33: 62).

 

Kwa hivyo, mwanadamu ni lazima apitiwe na majaribio katika maisha yake hapa duniani. Na mara nyingi sisi huwa tunalolitaka huwa hatufikirii hatima yake bali kila tulitakalo huliona kuwa ni jema. Lakini sikiliza Anayosema Allaah kuhusu mambo ya hapa, kwa tunayotaka na tusiyoyataka. Anasema Aliyetukuka:

 

Lakini huenda mkachukia kitu nacho ni kheri kwenu. Na huenda mkapenda kitu nacho ni shari kwenu. Na Allaah Anajua na nyinyi hamjui” (2: 216).

 

Hivyo basi amini Qadhwaa (aliyokupangia Allaah) na Qadar (aliyokukadiria) ili upate kukinaika na majaaliwa hayo

 

Hebu sasa turudi katika yanayokukumba katika maisha. Unapata mume wa kukuposa lakini harusi inavunjika, kuvunjika kwake kunaonekana si jambo zuri lakini sisi hatufahamu wala hatujui mazuri yetu. Mwenye kujua yote hayo ni Allaah Aliyetukuka. Kutofanikiwa harusi hizo ni kuwa hazina kheri nawe kwa namna moja au nyingine. Inatakiwa uwe na subira, uzidi kumuomba Allaah Aliyetukuka Akupe mume wa kheri ambaye ataweza kukusaidia na kusaidiana katika unyumba. Wala usidhanie kuwa kukosa mume kuwa una kasoro bali ni aina ya mtihani uliokufikia. Jambo linalotakiwa kwa kila Muislamu ni,

Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kuswali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu” (2: 45).

 

Zidi kumuomba Allaah Aliyetukuka Akupe mume wa kheri, mwema, mcha Mungu na maadili mazuri. Hasa muombe katika nyakati ambamo du’aa hukubaliwa kama saa za usiku unapoinuka kwa ajili ya Tahajjud, unapofunga, na hasa wakati wa kufungua, baina ya adhana na iqaamah, unapokuwa safarini. Bila shaka Allaah Aliyetukuka Atakusaidia wala usifunjike moyo kabisa katika hilo.

Ingia katika kiungo kifuatacho chenye makala nzuri kabisa zilizojaa maliwazo upate kuburudika moyo wako:

 

Usihuzunike  

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share