Mwanamke Anavaa Hijaab Lakini Anavaa Suruwali Ya Kubana Anaposwali, Je, Swalaah Yake Inakubalika?
Mwanamke Anavaa Hijaab Lakini Anavaa Suruwali Ya Kubana Anaposwali,
Je, Swalaah Yake Inakubalika?
SWALI:
Mwanamke anayevaa hijabu lakini huvaa suruali ya kubana, kisha akasali vipi? Naomba majibu, Rabbi akuzidishieni elmu ya manufaa na akupeni taqwa na atuongoze nyie nasie AMIN.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Ikiwa mwanamke huyo atakuwa ni mwenye kutoka akiwa katika hali hiyo na hijaab yenyewe ikawa haijatimiza masharti ya hijaab basi atakuwa na makosa. Na atachukuliwa ni kama hajavaa hijaab ipasayo kama inavyoamrisha Shariy’ah ya Dini hii ya Kiislamu. Lakini ikiwa atakuwa amevaa hijaab iliyotimiza masharti yake na ndani yake amevaa suruwali kwa kusudio la kutaka kujistiri pindi akipatwa na ajali akakhofia asitirike mwili wake wa ndani, hilo hakuna ubaya.
Masharti ya hijab ipasavyo katika Shariy’ah ni kama yafuatayo:
1. Jilbaab liwe refu la kukufunika mwili mzima mpaka miguu, na kama halikufunika miguu basi mwanamke avae soksi.
2. Jilbaab liwe pana na sio lenye kuonyesha umbo, yaani lisiwe lenye kubana popote mwilini.
3. Jilbaab liwe zito na si jepesi la kuonyesha mwili.
4. Jilbaab lisiwe na marembo yoyote yale ya kuvutia.
5. Jilbaab halitakiwi lifanane na mavazi ya makafiri.
6. Jilbaab halitakiwi liwe ni katika mavazi ya fakhari.
7. Wanawake kutokuvaa nguo zinazofanana na nguo za kiume.
8. Kutotia manukato.
Lakini ikiwa anaswali akiwa kavaa suruwali iliyobana kisha anaswali huku shepu ya mwili wake inaonekana, akisujudu na akirukuu ndio zaidi hayo maumbile yake yanazidi kujitokeza, basi Swalaah yake itakuwa haifai kwani kujisitiri vizuri ni katika sharti ya Swalaah.
Hivyo nasaha kwa dada zetu wazingatie hili na wawe wanajifunika vizuri kwa vazi la hijaab ya Shariy’ah na katika Swalaah ni vyema kujiwekea nguo maalum za kuswalia ajifunike nazo mwili wote ila uso na viganja vya mikono.
Ikiwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaeleza kuwa Allaah hatomtazama mwanaume mwenye kuburuza nguo yake kwenye Swalaah, je, vipi huyo mwenye kuvaa nguo yenye kuonyesha maungo yake yote mbele ya Muumba wake?
Tazama pia maswali yafuatayo upate faida ziyada:
Hukmu Ya Hijaab - Je, Inasababisha Kutoka Nywele?
Je, Inafaa Mume Kumlazimisha Mke Kuvaa Niqaab?
Hijaab Ya Shari'ah Inahusu Kufunika Uso Na Miguu?
Na Allaah Anajua zaidi