Wanja Unafaa Kupakwa Kwa Wanawake?

SWALI:

 

A. aleykum nilikuwa nauliza mwanamke kupaka wanja ni haramu? Watu wengine wanasema Sunna. Sasa sielewi ni ruksa ama si ruksa.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika Maswahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kupaka wanja. Kupaka wanja inafaa na ni Sunnah lakini mpakie mumeo ukiwa nyumbani kwako kwani wanja ni urembo na mapambo na hayo anayefaa kuyaona ni mumeo na si watu wengine huko nje. Hivyo, haifai kupaka wanja ukitoka nje kwani hayo ni mapambo na hayafai kuonwa na wasio Mahram zako.

 

Wanja pia ni dawa kwa magonjwa ya macho, hivyo kukiwa na dharura ya mwanamke au mwanamme kupaka kwa ajili ya kuondoa ugonjwa kutakuwa hakuna tatizo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share