Mashairi: Sherehe Ya Valentine, Ya Mapagani Warumi

                      ‘Abdallah Bin Eifan

                   (Jeddah, Saudi Arabia)

Salaamu kila pahali, leo nina simulizi,

Nitasema ya ukweli, wengi hawasikilizi,

Tuwe macho kwelikweli, kuna mengi sikuhizi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Mapagani wa Kirumi, Waloanzisha upuuzi,

Wakasambaza uvumi, ya sherehe ya mapenzi,

Uhakika hawasemi, fanyeni upelelezi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Walianzisha zamani, miaka sio miezi,

Sherehe za kishetani, kumshiriki Al-'Azizi,

Mawaridi madukani, mekundu wanayaenzi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Mwezi wa Februari, umeingia majuzi,

Wamejiweka tayari, kwa maua na mavazi,

Washike madaftari, na wapeane pongezi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Watoto wako nyumbani, wape mazuri malezi,

Wasifuate ya kigeni, na tabia za kishenzi,

Wafundishe yao dini, waambie waziwazi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Kuwaigiza Pagani, mwisho ni maangamizi,

Wao hawajui Manani, mabaya ni yao kazi,

Hufuata ya takani, mwisho wao ni majonzi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Dini imetufundisha, imeshaweka mizizi,

Yote imetuonyesha, na bila ya kizuizi,

Hakika imetuamsha, toka kwenye usingizi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Mayahudi na Nasara, kuigiza hatuwezi,

Dini yetu ya busara, kila kitu kipo wazi,

Na tena ipo imara, na sheria hatuchezi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Dini yetu safi sana, hutakuta ubaguzi,

Tumshukuru Rabana, Yeye Ndie Mkombozi,

Na Yeye tukionana, tufurahi kwa machozi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Kulea malezi bora, ni jukumu la wazazi,

Wasifanye maskhara, na watoto chipukizi,

Wafundishwe yalo bora, kule hamna mtetezi,

Sherehe ya Valentine, ya Mapagani Warumi.

Share