Maulidi: Sherehe Za Harusi Zina Maasi Uzushi Wa Maulidi Nyimbo Na Kujifakharisha
Maulidi: Sherehe Za Harusi Zina Maasi Uzushi Wa Maulidi Nyimbo Na Kujifakharisha
SWALI
Kwanza namshukuru Allah Subhaana-hu-wataala kwa kupata majibu mazuri kutoka kwenu. Naomba niulize suala jengine kuhusu sherehe za kiislam hasa za harusi kuhusu Maulidi ni bidaa au si bidaa. Na jengine wanawake wanaokusanyika katika harusi na kupigwa maulidi ya madufu wakacheza kama mfano wa rusha roho na kuvaa nguo wanazozijua wao ama za kifahari kwa kuoneshana na kukachukuliwa picha za video na still na wanaume wanakuwepo au hata hawajakuwepo kuna hukumu gani juu ya wanaofanya hivyo.
ahsante
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Tufahamu kuwa Uislamu umetupatia muongozo wa kila kitu ukijumlisha sherehe za harusi na pia misiba. Maulidi ni Bid’ah katika misingi ya sheria ya Kiislamu.
Ama katika sherehe za harusi wanawake wanaruhusiwa kuimba nyimbo nzuri na pia kupiga madufu wakiwa peke yao. Haifai kusomwa Maulidi kwani kama tulivyosema ni bid’ah na kisha ni ajabu kuwa Maulidi ambayo ni sherehe ya mazazi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanasomwa wakati wa harusi ambayo haina mahusiano na mazazi hayo.
Pia haifai katika sherehe hizo watu warushe roho wala kuvaa nguo ambazo hazifai kisheria kuvaliwa na mwanamke au kuvaa nguo za kifakhari. Mambo yote hayo kufanywa na wanawake. Ama kuchukua video ni jambo halina faida yoyote kwani video hizo zitakuwa zinazungushwa na kuwafikia hata wanaume wasio Mahram ambao hawafai kuwatazama wanawake hao. Na ama kukiwa na mchanganyiko ambao unakatazwa na sheria itafanya sherehe hizo zisikubaliwe Kiislamu.
Tufahamu yeyote mwenye kufanya mambo yanayokatazwa anapata madhambi. Na pia mwenye kuandaa jambo lililokatazwa na Uislamu anapata madhambi hivyo ni vyema Waislamu wasiwe ni wenye kwenda katika sherehe zinazokatazwa na sheria.
Bonyeza viungo vifutavyo upate maelezo zaidi ya maovu haya:
Ikhtilaatw (Kuchanganyika Wanaume Na Wanawake)
Kuchangia Na Kushiriki Shughuli Za Bidaa Ni Dhambi?
Kusoma Maulidi Kwenye Harusi Badala Kupiga Ngoma Inafaa?
Kuhudhuria Mwaliko Unaochanganyika Mazuri Na Maovu Inafaa?
Na Allaah Anajua zaidi