Aashuraa: Uzushi Unaodaiwa Kuhusu Mambo Yaliyotokea Siku Ya 'Aashuraa Tarehe 10
Uzushi Unaodaiwa Kuhusu Mambo Yaliyotokea Siku Ya 'Aashuraa Tarehe 10
SWALI:
Asalam aleikum
Nataka kujua kutoka kwenu Alhidaaya kuhusu haya mambo kuwa yametokea siku ya tarehe 10 Muharam, je ni kweli? Na upo ushahidi wake?
Mambo yenyewe ni haya
1-Nabi Adam aliumbwa siku hii
2- Allah alipokea toba ya nabi Adam
3- Nabiy Ibrahim alipewa daraja ya kuwa ni khalil wa Allah.
4-Nabiy Ayuwb aliponeshwa
6- Nabiy Muwsaa aliokolewa na Firauni
5 Jahazi ya Nabiy Nuwh ilitua katika ardhi kavu
7-Nabiy Suleyman alipewa ufalme
8-Nabiy Yaqub alionana na Yusuf baada ya miaka 40
9-Nabiy Yunuws alitolewa katika tumbo la nyangumi baharini.
10-Nabi Idrees alipandishwa mbinguni
11-Nabiy 'Iysa alipandishwa mbinguni
12-Siku ya kiyama kitatokea tarehe 10 Muharam
13-Bahari na mbingu zilumbwa
14-Mtu akioga siku hii hatoumwa tena.
15-Huu ni mwezi wa huzuni, hivyo mtu asiowe au kuolewa wala asiwe na furaha ya lolote.
16-Kupikwa chakula maalum katika siku hii ya Ashuraa.
17- Kuomboleza kifo cha Imam Husein siku ya leo na kujipiga mwili pamoja na kujikatakata
Nitashukuru kupata jibu kwani haya tunaletewa katika email na zinatumwa kwa wengi, nami sina hakika kama ni kweli haya au vipi.
Asanteni
Wa billahi Tawfik
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika mwenye kutaka haki basi ataipata tu kwa nia yake ya kuisafisha dini yetu tukufu. Uislamu umekamilika baada ya kufariki Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na yote tuliyoletewa tokea kupewa risala hadi kufariki kwake yamebainika wazi wazi kwa dalili katika Qur-aan na Hadiyth zake. Yasiyokuweko na dalili yote yatabakia kuwa ni uzushi na inampasa Muislamu asiwe na itikadi nayo na ajiepushe nayo kama Alivyotuamrisha na kututahadhirisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾
Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. [Al-Hashr: 7]
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
(( إن خير الكلام كلام الله وخير الهدي هدي محمد (صلى الله علي وسلم) وشر الأمور محدثاتها وكل محدثة بدعة وكل بدعة ضلالة وكل ضلالة في النار)) أخرجه مسلم في صحيحه
"Hakika maneno bora ni kitabu cha Allaah (Qur-aan) na uongofu mbora kabisa ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi, na kila jambo jipya (katika dini) ni bid'ah (uzushi) na kila bid'ah ni motoni." [Muslim katika sahiyh yake]
Hayo yote yaliyotajwa hayakupatikana dalili yoyote katika Qur-aan wala Sunnah isipokuwa nukta nambari 6 inayohusu Nabiy Muwsaa ('Alayhis-salaam). Hii tumeelezewa kuwa ni siku aliyookolewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana ukatili wa Fir'awn baada ya kuvuka bahari, na Fir'awn alivyojaribu kumfuata akaangamizwa kwa kugharikishwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na ndio maana siku hii alifunga Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akatuamrisha sisi pia tuifunge kwa kushukuru huko kuokolewa Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam). Dalili ni kama ifuatavyo:
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى ، قَالَ: (( فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ)) فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ" رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kasema “Alielekea Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Ashuraa, akasema: ((Nini hichi?)) (yaani kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa wana wa Israaiyl kutokana na adui wao, na Muwsaa alifunga siku hii. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mimi nina haki zaidi juu ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe" [Al-Bukhaariy]
Hayo mengine yote yaliyotajwa kwenye swali lako kuwahusu Mitume hakuna ushahidi wowote tulioupata katika mafunzo yetu, kwa hiyo hayatupasi kuwa na itikadi nayo.
Kuhusu kuwa ni mwezi wa huzuni nayo pia sio kweli. Ingawa Al-Husayn ambaye ni mjukuu wa Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), alifariki kwa kuuliwa siku hiyo ya tarehe 10 Al-Muharram, na hakika huu ni msiba mzito sana na wenye kutia huzuni kwa Waislam wote, lakini haina maana kuwa ndio iwe siku au mwezi wa huzuni kwetu, kwa sababu kwanza; hakuna popote pale tulipofundishwa kuazimisha misiba au kuomboleza kama wanavyoomboleza Mashia, vilevile maombolezi hayo ni ya kila mwaka na ndani yake kuna kujiadhibu, kujikatakata, kujitesa, kulaani Maswahaba na waliotangulia, watu wanakatazwa kuoana kwa sababu inadaiwa ni wakati wa huzuni n.k. na haya yote hayana ushahidi na isitoshe yamekatazwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyosema katika Hadiyth zifuatazo:
((Hayupo pamoja nasi atakayejipiga makofi ya mashavu akachana nguo zake na kutamka maneno ya kijahilia (yaliyokuwa yakitamkwa na washirikina kabla ya Uislamu)) [Al-Bukhaariy]
Na akasema:
((Mimi najitenga mbali na (kila) mwenye kupiga kelele na mwenye kukata nywele na mwenye kuchana nguo)) (anapokutwa na msiba). [Musim]
Na akasema:
((Kwa hakika mwenye kuomboleza kwa kupiga kelele asipotubu atavalishwa siku ya Kiama ngao ya shaba na nguo ya moto)) Muslim
Muislamu anapopatwa na msiba aseme kama Anavosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika Qur-aan:
الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ﴿١٥٦﴾
156. Wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” [Al-Baqarah: 156]
Na si kupiga kujikatakata mwili, kujipiga na kutukana na kulaani kama wanavyofanya Mashia.
Pia, wamefariki na kuuliwa wengi katika Maswahaba waliotajwa kwa utukufu na ubora zaidi kabla ya kufariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama Hamzah, Ja'afar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) nao ni bora kuliko Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu), na wala Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakufanya kuwa ni siku yao ya huzuni, wala hakututambulisha kuwa kutakapotokea kama hayo basi tufanye ni siku au mwezi wa huzuni. Na hata baada ya kufariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walifariki watukufu na wabora sana kama Abu Bakr, 'Umar, 'Uthmaan na 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhum), haswa hao watatu wa mwisho waliuliwa kwa dhulma vilevile kama alivyouliwa Al-Husayn (Radhwiya Allaahu 'anhu) na bila shaka yoyote ile wao ni bora sana kuliko yeye lakini hakuna aliyewahi kuwafanyia maombolezi kama yanayofanywa na Mashia!!
Je, Al-Husayn atakuwa ni bora zaidi kuliko 'Aliy bin Abi Twaalib ambaye ni baba yake na Khalifa wa Uislam? Na ambaye ni mtoto wa ami yake Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Na ambaye ni mume wa mtoto wake mpenzi Bibi Faatwimah (Radhwiya Allaahu 'anhaa)? Na ambaye ni wa kwanza katika vijana kuingia katika Uislam na kumuamini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Na ambaye amepigana kwa uhodari katika vita na mwenye sifa njema nyingi zinazojulikana? Kwa nini basi Mashia wasimuombolezee yeye kwanza kama kuna shariy’ah ya kuombeleza kama wanavyo omboleza?
Hayo ni mambo yasiyo ya msingi na ni kudhihirisha upotofu wa watu na kupenda kisasi na kutosahau wala kusamehe na kumwachia Allaah ambaye ni Hakimu Muadilifu ambaye Atawahukumu waliotenda maovu hayo ya kumuua kipenzi cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kipenzi chetu wote. Lakini hatupaswi kujidhuru wala kuishi na kisasi na kuyachanganya matukio hayo na mambo mengine yanayotuzunguka katika maisha yetu kama kuoana n.k.
Na Allaah Anajua zaidi