Vitisho Vinavyotolewa Katika Baadhi Ya Barua Ni Sawa?

 

 

Vitisho Vinavyotolewa Katika Baadhi Ya Barua Ni Sawa?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam Aleikum Warahmatullah Wabarakatuh.

 

Kwanza napenda kuwapongeza kwa juhudi zenu katika kueneza na kuelimisha waislam. Na In shaa Allaah, Allaah awalipe malipo yaliyo mema kabisa hapa duniani na Aakhirah.

 

Kuna barua pepe zinazotumwa zikieleza mambo ya kiislam kama vile kushahadia na hadiyth. Ama baada ya kumaliza kusoma barua pepe hizo mwishoni kuna kuwa na vitisho kuwa kama hujaituma kwa wengine basi wewe utapatwa na matatizo kama vile misiba na kufilisika nk. Je ni sahihi kuandika vitisho katika barua hizo unapokuwa mwandishi na unaposambaza?

 

Shukran,

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika nyaraka hizo ambazo zinagawanywa kwa Waislamu hazina msingi wowote katika Dini yetu tukufu. Haifai kwa Muislamu kutoa kopi au nuskha hizo na kuzigawanya au kuzituma kwa njia ya barua pepe kwani kufanya hivyo ni kueneza maasiya na madhambi. Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

..وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾

Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Maaidah: 2].

 

 

Kadhalika, barua kama hizo zenye maneno kama hayo zinaingia pia katika aina ya ushirikina kwani ni sawa na mtu kudai kujua ghaibu kw akusema utapatwa na kadhaa au utafikwa na kadhaa, mambo ambayo hakuna mwanaadam anaweza kuyajua isipokuwa yapo katika elimu ya Allaah pekee.

 

 

Kwa muhtasari, si sahihi kuandika barua hizo au kuzisambaza.

 

Zaidi soma yaliyomo katika kiungo kifuatacho:

 

Inayosemekana Miujiza Inayorushwa Katika Barua Pepe Ni Kweli?

Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

Je, Majina 99 Ya Allaah Kazi Yake Ndio Hii?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share