'Aqiyqah Afanye Nchi Za Nje Anakoishi Ambako Hakuna Jirani Waislamu Au Afanye Nyumbani Walipo Masikini?
SWALI:
ASALAM ALYKUM WARAHMATLLAH,
SUALI LANGU KUHUSIANA NA HAKIKI YA MTOTO KUIFANYA HAPA UK,
KWANI NINAVYO FAHAMU MIMI NIKWAMBA UCHINJE MBUZI MMOJA KWA MTOTO WAKIKE AU WAWILI KWA MTOTO WA KIUME NA UIGAWANYE NYAMA HIO MAFUGU MATATU MOJA UWAPATIE MAJIRANI ZAKO LAPILI UWAPATIE MASKINI NA LATATU LIWE KWA AJILI YAKO. SASA SUALI LANGU LIPO HAPA JUU YA KUWAPATA HAWA MASKINI KWA HAPA UK NA PIA HAWA MAJIRANI KUWEZA KUWAPELEKEA HIO NYAMA KWANI MAJIRANI ZANGU WOTE NI WAZUNGU ILA MMOJA TU NDIYE MUISLAMU MSWAHILI AMBAYE ANAWEZA KUPOKEA NYAMA HIYO. VILE VILE SITOWEZA KUPATA HAO MASKINI KWANI WOTE NI WATU WENYE UWEZO WAO. NAOMBA NIPATIWE MAFAHAMISHO ILI NIWEZE KUIFANYA HAPA AU NIFANYE KWETU VIJIJINI? NAOMBA UFAFANUZI JUU YA HILI TAFADHALINI.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ‘Aqiyqah ambayo ni sadaqa inayofanywa pindi wanandoa wanapopata mtoto, wa kiume au wa kike. Hakika lengo ya sadaqa zote katika Uislamu ni kutolea katika mtaa na mji anaoishi mmoja wetu ila kama kutakuwa na haja itakayopelekea kuhamishwa.
Haifai sadaqa kuhamishwa kutoka mji mmoja hadi mwengine ila kwa dharura za kishari’ah.
Tukizungumzia kuhusu ‘Aqiyqah upo ufahamu wa makosa kuwa ni lazima igawanywe mafungu matatu. ‘Aqiyqah mtu ameachiwa uhuru kabisa, anaweza kula yeye kila kitu, anaweza akatoa nyama yote na anaweza kumpatia amtakaye. Muhimu ni kule kumwagwa damu ya mnyama kwa lengo hilo la kutekeleza maagizo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Hivyo, fahamu kuwa hakuna ulazima wa kugawa nyama hiyo ingawa inapendeza kufanya hivyo.
Ama kwa hali yako hapo ulipo, unatakiwa kuifanya ‘Aqiyqah hapo ulipo na ukala nyama yako hiyo na unaweza kumpatia na huyo jirani yako Muislamu.
Unaweza pia kumpatia huyo jirani yako asiye Muislamu, sababu ni kuwa hata yule jirani asiyekuwa Muislamu ana haki moja na anaweza kupatiwa nyama hiyo kwa kutengeneza ujirani mwema na pia ni njia ya kumfanyia Da’wah akapata kuujua Uislamu.
Kwa hiyo, si lazima upate maskini ndio uwapatie hiyo nyama, na isiwe hiyo ndio sababu ya kukuzuia wewe kufanya ‘Aqiyqah hapo ulipo kwa sababu hakuna maskini.
Na Allaah Anajua zaidi