Mwenye Kuacha Swawm Za Fardhi Makusudi Nini Hukmu Yake?

 

 

Mwenye Kuacha Swawm Za Fardhi Makusudi Nini Hukmu Yake?

 

 Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum warahmatullah taala wabarakatu.

Naomba nielezwe adhabu za mwanamke/mwanamume aliye balegh na asofunga mwezi mtukufu wa ramadhan. Kwa mwanamke hayupo katika wakati wake wa
kutokuwa twahara lakini hafungi kwa kuwa hakujisikia kufunga. Shukran na Ramadhan Kareem kwa ndugu wote waislamu

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Kuacha Swawm kwa makusudi ni aina mbili:

 

1. Kuchukulia Swawm si nguzo ya Uislamu:

 

Ikiwa ni hivyo jambo hilo litamtoa mtu katika Uislamu na kuwa kafiri.

 

2. Kwa sababu ya udhaifu wake mwenyewe (kwa kutambua kuwa hiyo ni nguzo):

 

Kufanya hivyo ni dhambi kwake. Hapa duniani hapana adhabu maalumu atakayopatiwa isipokuwa ikiwa ipo dola ya Kiislamu naye anakula hadharani Qadhi atamtia adabu anayoona inafaa ili na wengine wasiwe ni wenye kumuiga katika maasiya hayo. Lakini Siku ya Qiyaamah ataadhibiwa vilivyo na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).   

 

Jambo linalotakiwa ni ni mtu au watu kuzungumza naye na kumueleza katika njia nzuri na ya sawa ili arudi katika misimamo ya kidini.

 

KiShariy’ah huyu mtu anatakiwa alipe kila siku aliyokula. Pia anatakiwa atubie, atake maghfirah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  tawbah ya kikweli kweli pamoja na kujuta na awe na azma ya kutorudia tena kosa hilo. Na anatakiwa ajitahidi kufanya amali za kheri nyingi ili mabaya yake yabadilishwe kuwa mema. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Anasema:

 

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

 

Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema.  Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.  

 

وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾

Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli.  [Al-Fuqaan: 70-71]

 

 

Lakini kwa yule ambaye hatatubia mpaka inafika wakati wa kukata roho basi hapo haitamsaidia kurudi na kutaka maghfirah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 

 

 وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾ 

Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapohudhuria kwa mmoja wao husema: “Hakika mimi sasa nimetubu.” Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa: 18]

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share