Hukmu Ya Swawm Ijumaa Ikiwa Ni Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa
Hukmu Ya Swawm Ijumaa Ikiwa Ni Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa
Swali La Kwanza:
Assalaam 'Alaykum,
Shukurani zetu kwa kutujuilisha muandamo wa mwezi,
Pia nilikuwa nina masuala machache kuhusu mwezi huu. Jee tunaweza kufunga Arafa Ijumaa peke yake? au ni vizuri tufunge na Alhamis ili tuepuka kufunga siku ya Ijumaa pekee na kupata fadhila za Alhamis??
Pia kuna ushahidi wowote wa kufunga siku tisa za mwanzo za mfungo tatu (Hijja) kama ilivyozoeleka na wengi
Jazaka Allah Khayra
Swali La Pili:
Je inafaa kufunga Ijumaa ikiwa itaangukia ni siku ya tarehe 10 Muharram (Ashura)?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Mas-alah ya Swawm ya siku ya Ijumaa pekee au Jumamosi pekee zinapoangukia siku zilizotajwa kuwa ni siku za Swawm kama 'Arafah na 'Ashuraa, yana ikhtilaaf baina ya 'Ulamaa. Kuna waliosema kuwa inafaa kutokana na fadhila zilizotajwa katika Swawm za siku hizo na kuna waliopinga kabisa kutokana na Hadiyth za Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Makatazo ya Swawm Ya siku ya Ijumaa:
عن أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ سَمِعْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ : (( لا يَصُومَنَّ أَحَدُكُمْ يَوْمَ الْجُمُعَةِ إِلا يَوْمًا قَبْلَهُ أَوْ بَعْدَهُ )) رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allahu 'anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Asifunge yeyote siku ya Ijumaa ila ikiwa (akiunganisha) siku kabla yake au baada yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Vile vile,
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : (( لا تَخْتَصُّوا لَيْلَةَ الْجُمُعَةِ بِقِيَامٍ مِنْ بَيْنِ اللَّيَالِي وَلَا تَخُصُّوا يَوْمَ الْجُمُعَةِ بِصِيَامٍ مِنْ بَيْنِ الْأَيَّامِ إِلا أَنْ يَكُونَ فِي صَوْمٍ يَصُومُهُ أَحَدُكُمْ )) مسلم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msiufanye usiku wa Ijumaa kuwa ni mahsusi kwa Qiyaam (Kisimamcho cha kuswali usiku) baina ya nyusiku nyingine na wala msiifanye siku ya Ijumaa ni makhsusi kwa Swawm baina ya siku nyingine isipokuwa ikiwa ni miongoni mwa siku anazofunga mmoja wenu)) [Muslim]
Pia,
عَنْ جُوَيْرِيَةَ بِنْتِ الْحَارِثِ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ دَخَلَ عَلَيْهَا يَوْمَ الْجُمُعَةِ وَهِيَ صَائِمَةٌ فَقَالَ ((أَصُمْتِ أَمْسِ)) قَالَتْ لا قَالَ ((تُرِيدِينَ أَنْ تَصُومِي غَدًا)) قَالَتْ لا قَالَ ((فَأَفْطِرِي)) وَقَالَ حَمَّادُ بْنُ الْجَعْدِ سَمِعَ قَتَادَةَ حَدَّثَنِي أَبُو أَيُّوبَ أَنَّ جُوَيْرِيَةَ حَدَّثَتْهُ فَأَمَرَهَا فَأَفْطَرَتْ رواه البخاري
Kutoka kwa Juwariyah bin Al-Haarith (Radhwiya Allahu 'anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliingia kwake siku ya Ijumaa naye akiwa amefunga akasema: ((Je, ulifunga jana?)) Akasema: "Hapana." Akasema: ((Je, unataka kufunga kesho?)) Akasema: "Hapana." Akasema: ((Basi fungua)) [yaani usifunge] Na kasema Hammad bin Al-Ja'd “Nimemsikia Qataadah akisema, Abuu Ayyuwb kaniambia kuwa Juwayriyah alimhadithia (alivyozungumza na Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ) akamuamrisha afungue . [Al-Bukhaariy]
Makatazo ya Swawm siku ya Jumamosi:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ بُسْرٍ عَنْ أُخْتِهِ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : (( لا تَصُومُوا يَوْمَ السَّبْتِ إِلا فِيمَا افْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ ، فَإِنْ لَمْ يَجِدْ أَحَدُكُمْ إِلا لِحَاءَ عِنَبَةٍ ، أَوْ عُودَ شَجَرَةٍ فَلْيَمْضُغْهُ)) وأبو داود وابن ماجه صححه الألباني في "الإروا
Kutoka kwa 'Abdullaah bin Busr kutoka kwa kaka yake kwamba Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Msifunge siku ya Jumamosi isipokuwa ikiwa mmefaridhiwa na Allah kwenu. Ikiwa mtu hakupata chochote cha kula isipokuwa jani la zabibu au gome la mti, basi alitafune)) [Abuu Daawuwd na Ibn Maajah na kaipa daraja ya sahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika Al-Irwaa]
Bonyeza katika kiungo kifuatacho chenye maelezo zaidi kuhusu hukmu ya funga ya Jumamosi:
Swawm (Funga) Ya Jumamosi Inapoangukia Siku Ya 'Arafah Au 'Aashuraa Inafaa?
Kauli za 'Ulamaa kuhusu mas-alah haya:
Ibn Qudaamah kasema: "Ni makruuh kuipwekesha siku ya Ijumaa kwa Swawm ila ikiwa imeangukia katika siku ambayo ni kawaida yake mtu kufunga kama vile Swawm ya siku moja na ya pili kuacha (Swawm ya Nabiy Daawuwd) ikaangukia Swawm kama hiyo katika siku ya Ijumaa, au kwa mwenye tabia ya kufunga siku ya mwanzo au ya mwisho au ya katikati katika mwezi." [Al-Mughni, Mjadala 3 Uk. 53]
An-Nawawy kasema: "Wafuasi wetu (yaani Mashaafi'iy) wamesema: Ni makruuh kuipwekesha siku ya Jumamosi kwa Swawm. Lakini mtu anaweza kufunga siku kabla yake au baada yake. Au ikiwa imeangukia katika siku za kawaida yake kufunga, au kama kaweka nadhiri mfano; ni siku ambayo mpenzi wake amepona, au siku fulani atakayorudi, na ikatokea kuwa siku hiyo ni Ijumaa basi sio makruuh kufunga" [Al-Majmuu-sharh al Muhadhadhab, Mjadala 6, Uk. 479]
Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema: "Sunnah inasema kuwa ni makruuh kupwekesha (mwezi wa) Rajab kwa Swawm na ni makruuh kuipwekesha Ijumaa (kwa Swawm)" [Al-Fataawa al-Kubraa, Mjadala 6, Uk. 180]
Imaam Ibn 'Uthaymiyn kasema: "Ama Ijumaa, sio Sunnah kufunga siku hii, na ni makruuh kuipwekesha kwa ajili ya Swawm" [Ash-Sharh al-Mumti', Mjadala 6, Uk.465]
Tukiacha makatazo hayo ya kuipwekesha siku ya Ijumaa kwa Swawm, mtu anaweza kufunga ikiwa ni siku ya kawaida yake mtu kama mwenye kufunga Ayyaamul-Biydhw (tarehe 13, 14, 15 ya kila mwezi wa Kiislam), na mwenye kutaka kufunga 'Arafah na ikaangukia kuwa ni Ijumaa.
Vile vile ikiwa mtu anataka kulipa deni lake la Ramadhwaan anaweza kufunga Ijumaa peke yake. Hii ni kutokana na Fatwa inayosema: "Inaruhusiwa Muislamu afunge Ijumaa peke yake ikiwa ni Swawm ya deni la Ramadhwaan" [Fatwa al-Lajnah ad-Daaimah, Mjadala 10, Uk. 347]
Kwa hiyo ikiwa ni 'Arafah au 'Ashuraa imeangukia kuwa ni Ijumaa inaruhusiwa Swawm kwa sababu niyyah ni ya Swawm ya 'Arafah au 'Ashuraa na sio kufunga Ijumaa. Vilevile ikiwa mtu atafunga na siku ya Alkhamiys, itakuwa ni jambo jema zaidi kwani atakuwa amepata fadhila zaidi ya moja kama ifuatavyo:
1. Fadhila ya kutekeleza Sunnah ya Swawm ya siku hiyo kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufunga Jumatatu na Alkhamiys.
2. Fadhila ya Swawm ya siku ya kabla ya siku ya Ijumaa, na hivyo ni kuondosha shaka yoyote inayohusiana na kuipwekesha Ijumaa kwa Swawm.
3. Fadhila ya kutenda amali nzuri katika masiku kumi ya Dhul-Hijjah kama ilivyosisitizwa katika Sunnah.
Alhidaaya inawasisitiza sana ndugu Waislam kutanguliza Swawm siku ya Alkhamiys na kumalizia Ijumaa katika hali hii ya kuangukia ‘Arafah kuwa Siku ya Ijumaa.
Ama kuhusu swali lako la pili kuhusu Swawm za siku 9 za Dhul-Hijjah, jibu lake liko tayari kwenye kiungo kifuatacho:
Inafaa Kufunga (Swawm) Siku Zote 9 Za Dhul-Hijjah?
Tunawakumbusha tena waulizaji, muwe mnatembelea kitengo cha maswali na majibu kwenye tovuti kabla hamjauliza maswali yenu. Kufanya hivyo kunawasaidia kupata majibu ya maswali mnayotaka kuuliza ambayo tayari yashajibiwa, na kadhalika kutatuwepesishia sisi na kazi za ziada In Shaa Allaah.
Na Allaah Anajua zaidi