Swawm Ya Nabiy Daawuwd Ukianza Kufunga Lazima Uendelee Haifai Kuacha?

 

Swawm Ya Nabiy Daawuwd Ukianza Kufunga Lazima Uendelee Haifai Kuacha?

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Swawm ya Nabii Daawuud

Asalam alay kum warahmatullahi  wabarakatuh

Mimi nataka kuwa nafunga swaumu kama ile ya nabiyyullahi iberaahiym  na kula leo na funga kesho lakini mimi napenda kusafiri sana sasa inajuzu kwangu kufunga swaumu hiyo ama uki anza haijuzu kupumzika na hakuna udhuru wowote?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ndugu yetu hiyo Sunnah uliyoitaja sio swawm ya Nabiy Ibraahim (‘Alayhis Salaam) bali ni swawm ya Nabiy Daawuwd (‘Alayhis Salaam).

 

Hakika hilo ni wazo zuri na niyyah nzuri kwa kila Muislamu kuwa nayo. Kwa hiyo, tunakuombea tawfiki wewe nasi pia tuweze kuihuisha Sunnah hiyo njema.

 

 

Nabiy Daawuwd (‘Alayhis Salaam) alikuwa na Sunnah nzuri sana katika mas-ala ya Swawm, kufunga siku moja na kuacha kufunga siku ya pili mpaka kitendo hicho kikapigiwa mfano na Nabiy wetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa  sallam) akasema:

 

أَحَبُّ الصِّيَامِ إِلَى اللَّهِ صِيَامُ دَاوُدَ، كَانَ يَصُومُ يَوْمًا وَيُفْطِرُ يَوْمًا

"Swawm inayopendeza zaidi kwa Allaah ni Swawm ya Daawuwd, alikuwa anafunga siku moja na anakula siku moja” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na pia Hadiyth ya  ‘Abdullaah bin ‘Amruw bin al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Hakika wewe unafunga kila siku na kuswali usiku mzima?” Nikasema: “Ndio”. Akasema: “…Hapana swawm ya mwenye kufunga milele, swawm ya siku tatu kila mwezi ni kama swawm ya mwezi mzima”. Nikasema: “Mimi naweza kulivyo”. Akasema: “Hivyo, funga swawm ya Daawuwd (‘Alayhis Salaam), yeye alikuwa akifunga siku na kula siku ya pili yake, na hakimbii anapokutana na adui” [al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na pia,  

 

Amesimulia ‘Abdullaah bin ‘Amruw bin al-‘Aasw (رضي الله عنهما): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Swawm inayopendwa zaidi na Allaah ni Swawm ya Daawuwd; alikuwa akifunga siku moja na akiacha siku moja. Na Swalaah inayopendwa zaidi na Allaah ni Swalaah ya Daawuwd. Alikuwa akilala nusu ya usiku, akiswali thuluthi yake na kulala sudusi (1/6) yake.” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

Hizi Swawm na Swalaah zilizotajwa ni zile za Sunnah sio za faradhi.

 

Ni vyema na vizuri kwa Muislamu anapoanza jambo jema (Sunnah yoyote) basi adumu nayo hata kama inaonekana ndogo na hilo ndilo jambo bora. Lakini kwa kuwa Uislamu ni Dini ya Fitwrah, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Ametuwekea mfumo wa kutekeleza hayo. Katika Ibaadah za faradhi kama vile Swawm, Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Ametusahilishia kwa njia kuwa lau mtu atakuwa mgonjwa au katika safari anaweza kula siku katika Ramadhwaan kisha kulipa baadaye. Sasa kwa kuwa wewe ni mtu wa safari unaweza kuwa unafunga wakati uko nyumbani au mjini kwako, na wakati ukiwa katika safari ukawa unakula. Lakini kwa neema ya Uislamu, ikiwa utashika Sunnah hii au nyingine yoyote na ukashindwa kuitekeleza kwa sababu ya udhuru basi Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anakuandikia thawabu ya aliyefunga ukiwa na ikhlaas na niyyah nzuri.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share