Zingatio 9: Zifunge Swiyaam Za Sitta Shawwaal

 

Zingatio 9: Zifunge Swiyaam Za Sitta Shawwaal

 

Naaswir Haamid

 

 

 Alhidaaya.com

 

 

Mgeni wetu Ramadhwaan ametuondoka tukiwa bado tunamuhitajia kwa hamu kubwa. Ametuachia mafunzo mengi mazuri na miongoni mwao ni Swiyaam za Sitta Shawwaal.

 

 

Hizi ni Swiyaam ambazo ameihimiza mno Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema:

 

 

((Mwenye kufunga Ramadhwaan kisha akaifuatilizia siku sita katika mwezi wa Shawwaal (mfunguo mosi) inakuwa kama aliyefunga mwaka (mzima kamili).)) [Imepokewa na Imaam Muslim]

 

 

Basi ni nani ambaye hataki kupata fadhila za siku hizi sita tu? Iwapo Muislamu amefunga masiku yote ya Ramadhwaan basi anashindwa kufunga siku hizi tu? Ni sawa na kusema: “umekula ngo'mbe wote amekushinda mkia.”

 

 

Fadhila za Swawm ni nyingi mno haswa pale Muislamu anapofunga kwa ajili ya kupata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Nayo ni ‘ibaadah pekee ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anaijua siri ya mja wake kinyume na Swalaah ambayo tunaonana tukiswali.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kwamba mwenye kufunga angalau siku moja basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Atamuokoa mja huyo kutokana na adhabu za Moto kwa umbali wa miaka sabini:

 

 

Kutoka kwa Abu Sa’iyd Al Khudriyy (Radhwiya Allahu ‘anhu) hakika Nabiy (swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Mwenye kufunga siku [moja] kwa ajili ya Allaah, [Allaah] Atamuokoa uso wake kutokana na moto kwa umbali wa miaka sabini.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Hizi ndizo ‘amali za kuzifanya kwa wakati huu tukiwa hai. Kwani Qiyaamah hakuna fedha, dhahabu, makasri wala chengine ambacho kitamfaa mwana Aadam. Ni amali zake za kheri ndizo zitakuwa muombezi wake. Na Swiyaam za Sunnah ya Sitta Shawwaal itakuwa miongoni mwao.

 

 

Miongoni mwa maombezi ya Qiyaamah ni ‘amali za Swawm na Qur-aan. Mwenye kuvipuuza vitu hivi navyo vitampuuza siku ya Hisabu. Itakuja Swawm siku ya Hisabu ikimuombea mja kwamba alikuwa akiacha kinywaji chake na chakula chake kwa ajili ya kupata radhi za Muumba. Naye kwa Rahmah Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atampatia shafaa’ah mja Wake. Hii sio siku ya kutegemea uombezi kutoka kwa baba, mama, ndugu wala rafiki. Hao sio kabisa! Zaidi labda wakuangamize kwa kudai haki zao juu yako wakufanye muflis wa ‘amali zako njema.

 

 

Share