Imaam Ibn 'Uthaymiyn: Mwanamke Kusafiri Kwa Ndege Bila Mahram Haijuzu

Mwanamke Kusafiri Kwa Ndege Bila Mahram Haijuzu

 

Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je, inajuzu kwa Mwanamke kusafiri kwa ndege bila ya kuwa na Mahram ingawa kuna usalama?

 

JIBU: 

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke haijuzu kusafiri bila ya kuwa na Mahram.” [Al-Bukhaariy 3006 na Muslim 1341]

 

Kasema haya wakati alikuwa amesimama na kukhutubia siku ya Hijjah. Akasimama mtu mmoja na kuuliza: “Ee Rasuli wa Allaah! Mke wangu ametoka kwenda kuhiji nami nimejiandikisha kwenda kwenye vita (Jihaad) kadhaa.” Akajibu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Nenda ukahiji pamoja na mke wako.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimuamrisha aache Jihaad kwa ajili ya kumfuata mke wake na kuhiji pamoja naye. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakumuuliza: “Je, mke wako yuko katika usalama au yuko pamoja na wanawake wengine au yuko na majirani?” Hii inaonyesha kwamba makatazo kwa mwanamke kusafiri peke yake ni kwa ujumla ('Umuwm An-Nahyi).

 

 

Isitoshe kuna baadhi ya hatari katika ndege. Tuzitafakari pamoja:

 

 

1-Tuchukulie mwanaume ambaye kamuacha mke wake asafiri peke yake.  Mwanamume atampeleka mke kiwandani cha ndege kisha ataondoka baada ya yeye (mwanamke) kuingia ndani kwa ajili ya kupanda ndege na kuruka. Huko mwanamke atakuwa bila ya Mahram. Je, haiwezekani ndege kugoma kuruka kwa sababu fulani? Bila shaka inawezekana na hutokea wakati safari ikavunjika kama ikiwa kuna hali mbaya ya hewa.

 

 

2-Pia, tuchukulie mwanamke akaendelea na safari yake mpaka anapofika katika mji wa kuwasili. Itakuwaje ikiwa kituo cha ndege kitakuwa na zahma nyingi za ndege  au kwa bahati mbaya kukatokea hali mbaya ya hewa jambo ambalo likasababisha ndege kubadilisha mwelekeo na kutua katika mji mwingine? Hii pia inawezekana.

 

 

3-Pia tuchukulie kuwa ndege ikaruka kwa wakati wake maalumu na ikatua kwa wakati wake maalumu na uwanja wa ndege maalum.  Mahram wake aliyekusudiwa kumpokea kiwandani katika mji huo aliofika akatokewa na dharura ya kutoweza kukutana naye kwenye uwanja wa ndege.  Hii pia inawezekana.

 

 

 

4-Pia huenda ndani ya   ndege akapata kiti pamoja na mwanaume pembeni yake. Huyu mwanaume anaweza kuwa mmoja katika viumbe vya Allaah ambao ni wadanganyifu. Akaanza kucheka naye, kuzungumza naye, kufanya utani naye,  akachukua namba yake ya simu naye (mwanamke) akampa ya kwake. Je, hili haliwezekani? Nani anayeweza kuokoka kutokana na hatari hii? 

 

 

Kwa hiyo utakuta hikma kubwa ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukataza mwanamke kusafiri peke yake bila ya kuwa na Mahram, na makatazo haya yametajwa si kwa ufafanuzi na kwa upana zaidi ila hikmah yake kubwa sana.

 

Basi huenda mtu na akasema: “Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hajui ya ghayb. Alikuwa hajui kuweko ndege kama hizi. Kwa hiyo ndiyo maana sisi tunazilinganisha safari za kale ambayo walitumia ngamia.  Hivyo ilikuwa ni sawa kwa mwanamke kutofaa kusafiri kwenye ngamia bila ya kuwa na Mahram lakini kusafiri kwa ndege hakuna neno. Kadhaalika, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hajui hizi ndege ambazo kwa robo saa mtu huweza kufika;  Mfano Twaaif mpaka Riyaadh, wakati hapo zama za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilikua inachukua mwezi mzima kwake kusafiri umbali kama huu.”

 

Sisi tunajibu kwa kusema: 

 

Ikiwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hajui ghayb, hata hivyo Rabb wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Amejua na Anajua hilo. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa): 

 

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ﴿٨٩﴾

Na Tumekuteremshia Kitabu kikiwa ni kielezo bayana cha kila kitu na ni mwongozo na rahmah na bishara kwa Waislamu. [An-Nahl: 89]

 

 

Kutokana na dalili kama hizi za hatari, nawaonya ndugu zangu kutokuchukulia mambo kiwepesi kwa kumruhusu mwanamke akasafiri bila ya kuwa na Mahram. 

 

Vile vile, ninakuonyeni muache kuruhusu mwanamke kuwa ndani ya gari peke yake na dereva wa kiume, hata kama itakuwa ni safari fupi ya katika mji wake. Hii ni hatari kubwa sana!

 

Pia nakuonyeni kuwaacha wanawake kuwa faragha pamoja na   hamuw (binamm, shimeji n.k) peke yao.  Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((إياكم والدخول على النساء، قالوا: يا رسول الله أرأيت الحمو؟ قال: الحمو الموت)) متفق عليه

“Tahadharini kuingia kwa wanawake.” (majumbani mwao) Wakasema: Ee Rasuli wa Allaah, je, vipi kuhusu Hamuw? (shimeji, binammi)? Akasema: “Hamuw  ni mauti. [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Yaani aliwaonya kwa kutumia njia ya ukali kabisa ya kifo. 

 

[Fataawaa 'Ulamaa Al-Balad Al-Haraam, uk. 545 Toleo 22/05/2005]

 

Maana ya Hamuw

 

Maana ya “Hamuw” katika hali hii kunamaanishwa ndugu za mume (wa kiume). Haafidhw Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) kasema: "Atw-Twabariy kasema: "Maana yake ni kuwepo kwa mtu (mwanamke) katika chumba na kaka wa mke au binamu ya mke ni kama kifo, kwa kuwa Waarabu huzoea kuita kila kitu chenye hatari ni “kifo.” [Fat-h Al-Baariy 9/401]

 

 

 

Share