Ndoa Ikiwa Wazazi Hawataki Kwa Sababu Ya Ukabila Na Mume Alioa Kabla

SWALI:

Asslamu Alaykum!

Mimi ni muislamu mwanamke mwenye umri wa miaka 25. Niliwahi kupendana na mwanamme wakati nilipokua na umri wa miaka 19 na aliniahidi kunioa, lakini kumbe alikua hana nia hiyo na badala yake alikua ameniteka kiakili na akawa akinitumia kwa haja zake na yote hii ni kwa sababu yeye alikua ni mkubwa kwangu kwa miaka saba na nilikua nikimpenda sana lakini badala yake ilinibidi tu niachane naye kwani alitafuta mwanammke mwengine katika familia yake na kumuoa. Mpaka sasa hivi sina uhakika kama mie ni Bikra au laa!! Kwani siku nilizokua nikitembea naye nilikua sijui chochote na alikua akinizidi kimawazo. Alla atanisameh.

Nikapendana mwanamme mwengine wakati nina umri wa miaka 23 lakini kwa kweli huyu nilikua simpendi bali nilitaka kumtumia kwa haja zangu kwani nilikua siwezi tena kuzuia matamanio yangu ya nafsi tangu nilipokua nae mwanamme wa mwanzo. Lakini huyu mwanamme wa pili niliachana nae kwa sababu alikua na tabia mbaya! Alikua akinilazimisha tufanye tendo la ndoa nilimkatalia akanambia tufanye lawiti (kinyume na maumbile) ilinibidi niachane nae.

Kwa sasa nimetokea kupendana na mwanamme mwengine mwenye umri wa miaka 29 na aliwahi kuoa na ana watoto wawili (lakini mke amemwacha). Kwa kweli ninampenda sana lakini kila nikijitahidi nisikutane nae kimwili nashindwa! Yaani inafika muda yeye anaweza kustahamili lakini mimi siwezi. Huyu ndio tumeahidiana kuoana na ishaallah Allah akiwafiq tutaoana. Sote tuna nia safi ila wazee wangu wana utata na suala hili eti sababu sio kabila langu na pia amewahi kuoa.

Naomba munifafanulie kiundani ikiwa ndoa hii inafaa na jee nini nifanye ili kuzuia matamanio ya nafsi yangu. Pia naomba munifundishe toba na tohara kwani hakika najuta kwa madhambi yangu na sina la kufanya inafika wakati nalia sana lakini bado nashindwa kuzuia matamanio yangu.

Vile vile naomba unifahamishe vipi nitajijua kama mie bado ni Bikra au laa! Nataraji umenifahamu na naomba unisitiri muislamu mwenzio .

 

Wassalm


JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kwanza kabisa tambua kuwa binaadamu wote tuna makosa na kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  katika  Hadiythi ifuatayo kuwa :

 

((كل ابن آدم خطّاء وخير الخطائين التوابون))  رواه أحمد عن أنس رضي الله عنه

  ((Kila binaadamu ni mkosa na wakosa bora kabisa ni wanaotubu))  Imesimuliwa na Ahmad kutoka kwa Anas رضي الله عنه

Kwa hiyo madamu umetubu bila shaka Allaah سبحانه وتعالى   Atakusameh kama ulivyoomba.

Kutokana na maelezo yako inaonyesha kuwa  wewe ni mtu mwenye akili na kumkhofu Mwenyeezi Mungu, ila tu shaytaan amekughilibu kuingia katika ma'asi.  Kwa hivyo uwe unamshukuru Allaah سبحانه وتعالى  kuwa Amekutanabahisha makosa yako na kukutaka  urudi Kwake  kwani  wangapi huwa katika ma'asi na kuendelea bila ya khofu ya Mola wao hadi wanafika uzeeni na wengine hadi mauti yawafike, jambo ambalo ni la kukhofia sana kukutana na ghadhabu za Mola Mtukufu.

Kuhusu mwanamume unayependana naye hivi sasa ambaye umesema kuwa alikwisha kuoa na ana watoto wawili, na kwamba mmeahidiana kuowana, ila wazee hawakupendezewa, napenda kukujulisha kuwa madamu mwanamume huyo ni Muislamu na mnapendana basi una haki ya kuolewa naye, na wazazi hakika wanamakosa kufikiria kuwa haikupasi kuolewa naye kwa sababu ameshaowa kabla na kuwa na watoto na pia kwa sababu ya ukabila. 

Sababu zote mbili wanazoziona nzito wazazi wako hazikubaliwi katika sheria ya Kiislamu kumzuwia mtu kutokuolewa. Ikiwa kuhusu kuwa ana watoto, hiyo itakuwa ni thawaabu kuishi nao na kuwashughulikia hao watoto. 

Ama kuhusu Ukabila kuwa sio kabila lako, hii ndio kabisa haimpasi mtu kufikiria jambo hili kwani Allaah سبحانه وتعالى   Amesema:

((إ ِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ))

))Hakika Waumini ni ndugu((

Al-Hujuraat: 10

Vile vile Amesema Allaah سبحانه وتعالى

((إ ِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ))

))Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mchamngu zaidi katika nyinyi((

Al-Hujuraat:13

Lakini kwa upande mwengine, ni vizuri kuwaridhisha wazee, kwani hii ni kawaida ya wazazi hupenda kumtakia mtoto wao aolewe na mtu katika jami'i yao.  Kwa hiyo unaweza kufanya hivi:

1)     Wafahamishe wazazi wako kwa hikma na utulivu kwamba umri wako mkubwa sasa na bado hakutokea mume munaasib katika jamii yenu.

2)     Kwamba huyu anayetaka kukuowa ni Muislamu mwenzako na anakutaka kindoa sio nje ya ndoa, hivyo inadhihirisha kuwa ana nia safi na amekuwa tayari kuchukua mas'uliya ya kuwa na mke.

3)     Kama una jamaa zako khaswa watu wazima ambao wanaweza kuzungumza na wazee wako kuwasisitiza na kuwafahamisha kuwa dini ya kiislamu haikatazi mtu kuolewa na kabila jengine au kudharau kabila jengine kwani sote ni asili moja, na aya ifuatayo inathibitisha kuwa ukabila ni kwa ajili ya kujuana tu na aliyebora zaidi ni yule mcha Mungu

}}يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَى وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ{{

{{Enyi watu! Hakika Sisi Tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na Tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah  ni huyo aliyemcha Mungu zaidi katika nyinyi. Hakika Allaah ni Mwenye kujua, Mwenye khabari}}

Al-Hujuraat:13

 

 Kuhusu kufanya tawbah, bonyeza viungo vifuatavyo usome mada zinazohushu maudhui hii:

Maana ya Tawbah (Toba)
Allaah Anampenda Mja Anayeomba Tawbah
Hatari Ya Kuchelewa Kuomba Maghfira Na Tawbah
Vipi Kuomba Maghfira Na Tawbah?
Wakati Bora Wa Kuomba Tawbah
Tawbah Ya Kweli Na Masharti Yake
Faida Za Kuomba Tawbah (1)
Faida Za Kuomba Tawbah (2)

 

Kuhusu kujiepusha na matamanio ya nafsi yako ili kujitoharisha na uchafu huo,  njia iliyo bora kabisa ni kuolewa.  Kwa hiyo fanya kila njia ya kuwafahamisha wazazi wako wakubali.  Na kama wakikataa, basi kiislamu unahaki ya kutafuta Walii (Msimamizi) akakuozesha.

Jambo la pili la kufanya ni kumkubuka Allaah سبحانه وتعالى  sana kwa kila aina ya ukumbusho, zaidi ni Qur'aan, Istighfaar, kila ya aina za Tasbiih na kuomba sana Du'aa Allaah سبحانه وتعالى  Akuepushe na ma'asi na akuzidishie imani ya dini yako.   Vile vile kusikiliza mawaidha ni njia mojawapo ya kupata ukumbusho wa kumkhofu Allaah سبحانه وتعالى  na pia kupata matumaini ya Pepo na hapo ndipo imani itakapokuwa inazidi katika moyo wako.  

Tunakuombea Allaah سبحانه وتعالى Azidi kukuhidi utoke katika ma'asi na Akuingize katika nuru ya imani, na vile vile tunakuombea ndoa ya kheri.

Na Allaah Anajua zaidi. 

 

 

Share