Ndoa Ya Siri Inafaa Juu Ya Kwamba Imefungwa Msikitini Na Imaam Na Mashahidi Wawili?


SWALI:

Asalam aleikum, Mimi ni mwanamke wakiisilamu ambae nimeolewa wasunatillah warasuloh (SAW) lakini ni ndoa ya siri.

Swali. Jee ndoa hii yaswihi au haiswihi kulingana na sharia za kiisilamu ingawa ndoa yetu ilifungwa msikitini mbele ya imam na mashahidi wawili na watoto wangu? Shukran wa jazakumullah kheir, 

 

 


JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ahli zake, Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum)   na walio wafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran dada yetu kwa swali lako hilo zuri. Kwa hakika kama tulivyojibu mara nyingi kuhusu masuala ya ndoa ni kuwa ndoa katika Uislamu ina nidhamu yake na masharti yake ambayo yakipatikana basi ndoa hiyo inakuwa ni halali. Miongoni mwa masharti ni:

     1.      Kupatikana walii wa binti.

2.      Kusiwepo na vizuizi kwa wenye kuoana vya kuwazuia kuuoana, kama undugu wa damu n.k. 

     3.      Kuwepo kwa mashahidi wawili waadilifu.

     4.      Kuwepo na Iyjaab na Qubuul, yaani walii kusema, nimekuozesha bint yangu...., na kujibu mume (muoaji), nimekubali kumuoa .....

 

Ikiwa ndoa ilifungwa Msikitini na kukawa na mashahidi wakiwemo watoto wako huwa si siri tena hiyo na ndoa hiyo imeswihi na ni ya sawa sawa. Kwa hakika ikiwa ni siri kabisa ambapo hakuna mashahidi wala walii ndoa hiyo kisheria haitakuwa ni yenye kusihi.

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share