Kusikiliza Qur-aan Huku Unafanya Kazi Zako

 

Kusikiliza Qur-aan Huku Unafanya Kazi Zako

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI

 

Jee unaweza kusikiliza Qur-an kwa makini huku unafanya kazi zako jikoni kama kupika au kukosha vyombo ingawa akili yako yote iko katika kile kisomo? 

 

 

JIBU:

 

 AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hii haina shaka kwani kusikiliza huko kwa makini ndiko kumesisitizwa zaidi. Na linalochukiza kwa baadhi ya ‘Ulamaa ni kuzungumza na huku Qur-aan inasomwa kwa ushahidi wa aya hii:

 

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾

Na inaposomwa Qur-aan, basi isikilizeni kwa makini na bakieni kimya (mzingatie) ili mpate kurehemewa. [Al-A'araaf: 204]

 

Hata hivyo pamoja na baadhi ya wanachuoni kusema kuwa aayah hiyo makusudio ni popote, ila wanachuoni wengi na wafasiri kama Ibn Kathiyr katika tafsiri yake kasema: "Maana yake ni ukiwa ndani ya Swala ya Jamaa'ah, pindi Imamu anaposoma kwa sauti (swala za Alfajiri, Maghrib na 'Ishaa') kama ilivyopokewa na  Imaam Muslim kwenye Sahiyh yake kutoka katika hadithi ya Abu Muwsaa Al-Ash'ariy aliyesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa Sallam) amesema:  ((Imaam amewekwa ili afuatwe, kwa hivyo akisema: "Allaahu Akbar nanyi mfuateni kwa kusema kama yeye na akianza kusoma, nyinyi nyamazeni))

 

Vile vile akasema tena Ibn Kathiyr: Ibraahiym Ibn Muslim Al-Haajriy amepokea kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: Wao (Swahaba) walikuwa wakizungumza na hali ya kuwa wamo ndani ya swala, kwa hivyo ilipoteremshwa aya hii ... waliamrishwa wawe kimya.

 

Naye Imam At Twabariy kwenye tafsiri yake anasema kwamba Ibn Mas'uud amesema: Tulikuwa tukipeana salamu miongoni mwetu tukiwa ndani ya swala, kisha ikaja katika Qur-aan: Na isomwapo Qur-aan isikilizeni na nyamazeni.

 

Kwa hoja hizo inaonyesha aayah hiyo haihusiani na Qur-aan isomwayo maredioni na kwenye matelevisheni makompyuta au na watu nje ya swala, hata hivyo kwa kuyapa heshima maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  ni bora kunyamaza isomwapo au kuizima kama huwezi kusikiliza. Wa Allaahu A'alam

 

Nasiha Ya Kufuata Adabu Za Tilawa (Kusoma) Qur-aan;

Kwa hali yeyote ilivyo, ni bora kuipa heshima Qur-aan kwa kutimiza adabu za kusoma Qur-aan kwani ni maneno ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa na kuyatukuza ni wajibu. Nazo ni:  

 

1)   Kupiga mswaki

2)   Kuwa na wudhuu

3)   Kujifunika vizuri (mwanamke)

4)   Kuelekea qibla

5)   Kusoma kwa kutafakari

6)   Kusoma kwa Tajwiid na kufuata sheria zake.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share