Ndoa Ya Siri Ikiwa Wazazi Hawataki Kwa Sababu Wanamsomesha Wakijua Watakataa Kumlipia Ada

 

SWALI:

Aslam Alyekum

Mie ni binti wa kiislam ambaye niko masomoni nchini Uingereza na nimepata mchumba muislam huku UK na anataka kunioa, lakini mtihani tulikuwa nao ni  kwamba mie nasomeshwa na wazazi wangu na kwamba wakijua kwamba ninamchumba na ninataka kuolewa nae watakataa kunilipa ADA ( School Fees). (Mchumba wangu hana uwezo wa kunilipia). 

Je naomba ushauri kama inawezekana binti kufunga ndoa kisiri bila wazazi wake kujua (au baba yake kumuodhesha ikiwa yuko hai?). Kusema ukweli huu ni mtihani mkubwa kwetu kwani uvumilivu wetu kila siku unapata mitihani na tunataka kufunga ndoa ili tufanye tendo lile kwa halali lakini kama nilivyosema wazazi wangu wakijua mie shule basi tena na bado nahitaji msaada wao kwa miaka miwili iliyobaki ya course yangu.

Naomba nijibiwe swali langu.

 


 

 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani nyingi kwa dada yetu aliyeuliza swali hili nyeti katika Dini na ambalo vijana wengi wanalipuuzia. Ifahamike kuwa ndoa katika Uislamu ina masharti yake au nguzo zake ambazo zinaifanya iwe halali na yenye kukubaliwa kisheria. Kukosekana nguzo mojawapo inaibatilisha ndoa hiyo. Nazo ni kama zifuatavyo 

1.    Kuwepo kwa walii ambaye ni baba, ikiwa hayuko au amekufa ndugu wa kiume, na kadhalika;

2.    Kwa uchache mashahidi wawili waadilifu;

3.    Namna ya kufunga ndoa: Ni Walii kumuozesha binti yake huyo mume na mume mwenyewe kukubali;

4.    Kutolewa mahari na mume.

Hakuna ndoa ya siri katika Uislamu, kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza kuwa ndoa itangazwe. Na ikiwa ndoa inayoitwa ya siri ni ile ambayo kwamba mume anaoa mke wa pili lakini hataki mkewe wa kwanza ajue hilo, basi itasihi ikiwa imetimiza masharti hayo hapo juu.

Mara nyingi huwa tunasema nimekutana na mvulana na namuona ameshika Dini, lakini mara nyingi huwa hatumjui vilivyo. Kwani utakuwa umekutana naye katika darasa na kupendana kwa kule kuonana tu mara ya kwanza.

Kuwepo Walii katika ndoa ni kuhakikisha kuwa maslahi ya binti yametimizwa na kusiwe na udanganyifu wowote. Hii ni kuwa wasichana wanakuwa madhaifu na Uislamu unataka kuhakikisha kuwa maslahi yao na haki zao hazidhulumiki.

Katika kadhiya yako hii ni kuwa masharti ya ndoa hayajakamilika na kukaa pamoja au kuoana itakuwa mnazini na kupata madhambi. Kisha itakuwa taabu zaidi kwako lau mzazi atakuja kujua kuwa unakaa na mvulana nawe umemficha. Hiyo shida ambayo hutaki kuipata ndio itakuwa kubwa zaidi. Hakika ni kuwa huwezi kuliweka jambo hilo kuwa siri kwa muda wote wa miaka miwili ambayo upo chuoni. Unaweza kushika mimba au ikafika habari hiyo nyumbani. Utawajibu nini wazazi kuhusu hilo?

Nasiha zetu kwako za dhati ni kuwa mwanzo umfahamu zaidi huyo mume. Je, anazo sifa ambazo zinatakiwa mume wa Kiislamu awe nazo katika Dini, Ibadah, Maadili na mengineyo au umempenda kwa sababu ya sura zake na mengineyo. Miaka miwili si mingi na ikiwa huyo mvulana anakupenda kweli, basi anaweza kukusubiri mpaka umalize. Katika hali hiyo mnaweza mkawa mnafunga Swawm ya Sunnah ili kupunguza matamanio. Ni lazima msiwe mnakutana kama ilivyoagiza Dini ya Kiislamu ili msije mkafanya dhambi ambapo ndio mara nyingi hutokea. Ukiona huwezi vumilia basi itabidi uzungumze na mzazi wako ima mama au baba ambaye unaona anaweza kukuelewa kuhusu jambo hilo. Mara nyingi binti huwa anaweza kuzungumza kwa uwazi zaidi na mama ambaye naye anaweza kumueleza baba kuhusu hilo. Ikiwa wataelewa na kukufahamu basi itakuwa ni kheri lau wamekataa, basi jipinde katika masomo na InshaAllah tunamuomba Allah Aliyetukuka Akupatie lenye kheri nawe hapa duniani na kesho Akhera.

Usifanye haraka.

Na Allah Anajua zaidi

Share