Mkate Mtamu Laini Wa Kuoka (Baked)

Mkate Mtamu Laini Wa Kuoka (Baked)

 

 

Vipimo

 

Unga mweupe - 3 Vikombe vikubwa (mugs)

Sukari -  1/3 mug (chini ya nusu mug)      

Maji -  ¾ mug

Maziwa ya unga - ½ mug

Mafuta -  ¼ mug

Mtindi -  1 kijko cha kulia

Hamira (instant) - 2 vijiko vya kulia

Yai -  1

Hiliki - 1 kijiko cha chai                                                     

 

Namna Ya Kutayarisha Na Kupika  

  1. Koroga maziwa ya unga katika maji.
  2. Ikiwa hamira ni ya chengachenga, weka katika kikombe kidogo cha kahawa, tia chembe sukari na maji iuumuke. Ama ikiwa ya instant changanya moja kwa moja katika unga.
  3. Changanya vitu vyote katika bakuli, ukande vizuri sana mpaka uwe laini.  Ukiwa na mashine ya kukandia ndio vizuri zaidi.
  4. Ukishalainika, funika kwa muda mpaka uumuke kidogo.
  5. Washa oveni moto mdogo mdogo (kiasi 150 degrees) Unaweza kuchoma katika mkaa pia.
  6. Pakaza siagi katika treya za kuokea (baking trayers) weka tayari.
  7. Fanya madonge saizi upendavyo kisha weka madonge kiasi ya kutosheleza treya zako. Huenda ukatumia treya zaidi ya mbili kulingana na ukubwa wa treya na wingi wa madonge.
  8. Funika treya uumuke tena vizuri.
  9. Weka katika oveni upike kwa muda robo saa takriban hadi ugeuke rangi ya hudhurungi (golden brown).
  10. Epua ukishapoa, toa katika treya panga katika sahani ukiwa tayari.

 

Bis-swihhah wal-hanaa (kula kwa siha na kufurahika)

 

 

 

Share