223-Asbaabun-Nuzuwl: Al-Baqarah Aayah 223: نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ ۖ وَقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُمْ
أسْبابُ النُّزُول
Asbaabun-Nuzuwl
(Sababu Za Kuteremshwa Suwrah Na Aayaat Za Qur-aan)
Imekusanywa na: Alhidaaya.com
Al-Baqarah Aayah 223: Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu…
نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ ۖ وَقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُمْ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَاعْلَمُوا أَنَّكُم مُّلَاقُوهُ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢٢٣﴾
223. Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu (panapotoka kizazi) vyovyote mpendavyo. Na kadimisheni (mema) kwa ajili ya nafsi zenu. Na mcheni Allaah na jueni kwamba hakika nyinyi ni wenye kukutana Naye. Na wabashirie Waumini.
Sababun-Nuzuwl:
Aayah hii: “Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu (panapotoka kizazi) vyovyote mpendavyo.“ imeteremka kuwazungumiza Mayahudi waliokuwa wakisema kuwa mwanaume akimuingilia mke wake kupitia upande wa nyuma, basi anazaliwa mtoto akiwa ana makengeza. Ndipo ikateremka hii Aayah. [Al-Bukhaariy, Muslim kutoka kwa Jaabir (رضي الله عنه)]
Pia, Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) alisema kuwa kauli hiyo; “Wanawake zenu ni konde kwenu“ iliteremshwa kuwazungumzia baadhi ya watu wa Answaar ambao walikuja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakamuuliza (kuhusu kumuingilia mwanamke kutokea upande wa nyuma). Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akawajibu: “Muingilie vyovyote upendavyo madhali ni ukeni.” [Ahmad]
Hadiyth kama ilivyothibiti :
عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ، أَنَّ يَهُودَ، كَانَتْ تَقُولُ إِذَا أُتِيَتِ الْمَرْأَةُ مِنْ دُبُرِهَا فِي قُبُلِهَا ثُمَّ حَمَلَتْ كَانَ وَلَدُهَا أَحْوَلَ . قَالَ فَأُنْزِلَتْ: ((نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّى شِئْتُمْ))
Imepokelewa kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah kwamba Mayahudi walikuwa wanasema pale mke anapoingiliwa mbele katika sehemu za siri, lakini akiwa amegeuka nyuma, na pindi anaposhika mimba husema kuwa mtoto atazaliwa kengeza. Hapo ikateremshwa Aayah: “Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu (panapotoka kizazi) vyovyote mpendavyo.“ [Muslim Kitaab An-Nikaah]