Kula Dawa Kubadilisha Umbo Inafaa?

 

Kula Dawa Kubadilisha Umbo Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Ukila chakula kimewekwa madawa yaku shape mwili wako (an asana tumbo), je hiyo inakubalika katika dini ya kiislam??

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho. 

 

Mas-ala hii imekuwa ni tatizo kubwa kwetu tulioko Afrika Mashariki japokuwa hapo awali tatizo hii ilikuwa zaidi nchi za Kimagharibi.

 

Katika vyakula Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Ametuhalishia vilivyo halali na vizuri. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye akatubainishia kuwa "Halali iko wazi na pia haramu ni hali hiyo hiyo, lakini baina ya hivyo viwili kuna mambo yenye shaka. Haya ya shaka hayajulikani na wengi na mwenye kuepeukana nayo, bila shaka atakuwa amehifadhi Dini na heshima yake…" [al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

Mbali na hiyo Hadiyth ya juu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika Allaah ni Mzuri na Hakubali ila zuri. Na hakika Allaah Amewaamrisha Waumini yale Aliyowaamrisha Rusuli. Akasema:

يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ 

(Allaah Akasema): Enyi Rusuli! Kuleni katika vizuri na tendeni mema, [Al-Muuminuwn: 51].

 

Na akasema tena Allaah Aliyetukuka:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ

Enyi walioamini! Kuleni vizuri Tulivyokuruzukuni [2: 172”] [Muslim].

 

Vyakula vilivyo vizuri vinakuwa ni maslahi yetu ya afya na siha nzuri. Chakula chochote ambacho kinatiwa madawa ambayo tena mengi hayajulikani vinakuwa na madhara kwa mwili wa mwanadamu. Unapotumia tu dawa ya kuuweka mwili wako uwe na umbo zuri basi umbo hilo ili kubaki katika hali hiyo ni lazima uwe ni mwenye kutumia vyakula vyenye madawa hayo.

 

Hali hii itakuwa wewe ni mwenye kutumia vyakula hivyo, na utambue kuwa pindi utakapoacha basi madhara yako yatakuwa makubwa. Uislamu kwa kuwa unajali maslahi ya mwanaadamu hautaki yeye adhurike kwa njia yoyote ile. Kwa Uislamu una msingi kwa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Haifai kudhuru wala kulipana madhara" [Maalik, Ibn Maajah na ad-Daraqutniy].

 

Na Allaah Aliyetukuka Ameliweka hili wazi pale Alitueleza kuhusu madhara ya vileo:

 

فِيهِمَا إِثْمٌ كَبِيرٌ وَمَنَافِعُ لِلنَّاسِ وَإِثْمُهُمَا أَكْبَرُ مِن نَّفْعِهِمَا ۗ

Katika viwili hivyo mna dhambi kubwa na (baadhi ya) manufaa kwa watu. [Al-Baqarah: 219].

 

Hakika ni kuwa madhara ya vitu hivi ni kubwa hivyo kufanya kuwa haramu. Tutahadhari sana na kudangaywa kuhusu mambo haya kwani huenda tukadhurika na kukosa dawa na magonjwa yatatuvaa. Leo Bara Ulaya na Marekani inapiga kelele kuhusu vyakula vinavyokuzwa kwa kutumia teknojia ya jeni na kuitwa GMO’s kuwa zina madhara lakini hapo hapo teknolojia hiyo hiyo inaletwa Afrika ili kuondoa uhaba wa vyakula.

 

Vyakula vile vyenye rutuba ni vile vinavyokuuzwa kwa njia ya kawaida. Leo wageni wanaofika katika sehemu vyakula hivyo vinavyopatikana wanafurahi sana kwa ladha wanayoiona. Hakuna njia nzuri ya kuweka mwili wako uwezo kabambe kama kufanya mazoezi. Yapo mazoezi ya tumbo, misuli, miguu, kichwa ambayo unaweza kufanya nawe ukawa barabara kabisa. Na vyakula ni wewe kufunzwa au kununua vijitabu vinavyoeleza kuhusu lishe bora na kutizama utakuwa unakula nini na kiasi gani. Kufanya hivyo kitumbo hicho kitakuwa na umbile utakalo na madhara yatakuwa hayapo In shaa Allaah.

 

Tukumbuke kuwa Allaah aliyetukuka Ametuambia:

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ ۛ

Wala msijitupe katika maangamizi kwa (kuzuia) mikono yenu (isitoe). [Al-Baqarah: 195].

 

Kujibadilisha umbo Alilokuumba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni katika hila za shaytwaan ambaye hamuachi binaadamu kwa lolote ila kutaka kuwapotoa wapate ghadhabu za Mola wao, alisema shaytwaan:

 

إِن يَدْعُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا إِنَاثًا وَإِن يَدْعُونَ إِلَّا شَيْطَانًا مَّرِيدًا ﴿١١٧﴾لَّعَنَهُ اللَّـهُ ۘ وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ﴿١١٨﴾وَلَأُضِلَّنَّهُمْ وَلَأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الْأَنْعَامِ وَلَآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللَّـهِ ۚ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللَّـهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا ﴿١١٩﴾يَعِدُهُمْ وَيُمَنِّيهِمْ ۖ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلَّا غُرُورًا ﴿١٢٠﴾أُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَلَا يَجِدُونَ عَنْهَا مَحِيصًا ﴿١٢١﴾

Hawaombi badala Yake isipokuwa miungu ya kike na hawaombi isipokuwa shaytwaan muasi.Allaah Amemlaani. Na (shaytwaan) akasema: Kwa hakika nitashika katika waja Wako sehemu maalumu. Na hakika nitawapoteza, na nitawashawishi matamanio ya kulaghai, na nitawaamrisha. Basi watakata masikio ya wanyama (wawatukuze), na nitawaamrisha watabadili maumbile ya Allaah. Na atakayemfanya shaytwaan kuwa rafiki mwandani badala ya Allaah basi kwa yakini amekhasirika khasara bayana.Anawaahidi na anawashawishi matamanio ya uongo. Na shaytwaan hawaahidi isipokuwa ulaghai. Hao makaazi yao ni Jahannam, na wala hawatopata makimbilio ya kutoka humo.

 

Kwa hiyo inakupasa kujiepusha na maouvu hayo.  

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share