Zakaatul-Fitwr: Kutoa Zakaatul-Fitwr Kiwango Zaidi Na Kutoa Siku Kumi Kabla Ramadhwaan Kumalizika
Kutoa Zakaatul-Fitwr Kwa Kiwango Zaidi Ya Anachostahiki Maskini Na Kutoa Siku Kumi Kabla Ya Ramadhwaan Kumalizika
SWALI:
Assalam alaykum,
naomba kuuliza,
1. ikiwa mie natakiwa kutoa Zakaatul fitr yenye thamani ya pesa zaidi ya laki moja na nayelenga kumpa ana hitajio la juu sana, yajuzu kumpatia zaka iyo siku 10 kabla ya Eid el fitr?
2. je naweza kumpatia kiasi cha zaidi ya ile ninayowajibikiwa kutoa nikiwa na niya ya kumfanya awapendezeshe watu wa nyumbani kwake na awalishe pia?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himdi Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu Swalaah na salamu zimshukie kipenzi chetu Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Wa 'Alaykumus-salaam wa RahmatuLLaahi wa Barakaatuh,
Zakaatul-Fitwr hutolewa chakula na si pesa kwa mujibu wa Ahaadiyth zilizopokelewa katika mlango huo.
Dalili:
Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliifanya kutoa swaa' (pishi) ya tende au swaa' (pishi) ya shayiri (ngano) kuwa ni Zakaatul-Fitwr iliyowajibika kwa Waislamu wote, mtumwa aliye huru, mwanamke na mwanamume, kijana na mzee, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul-'Iyd). [Al-Bukhaariy]
Abu Sa'iydil-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: "Tulikuwa tukilipa Zakaatul-Fitwr swaa' (pishi) moja ya chakula, au swaa' (pishi) ya shayiri (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama hizo) au swaa' (pishi) ya tende au swaa' (pishi) ya aqit (mtindi mkavu) au swaa' (pishi) ya zabibu" [Al-Bukhaariy]
Kwa dalili hizo, ni dhahiri kwamba Zakaatul-Fitwr lazima iwe ni chakula, si pesa. Hivyo lazima tutekeleze ilivyoamrishwa katika Sunnah. Hivyo lipa swaa' (pishi) moja ya chakula chochote kinachotumika na watu katika nchi yako mfano mchele au ngano kwa ajili yako na kila mtu katika nyumba yako. (swaa' (pishi) ni sawa na taqriban kilo 2 na nusu au kilo 3).
Kwa hiyo, ikiwa pesa zake atazitoa ili zinunuliwe aina ya hiyo ya chakula kinacholiwa zaidi hapo mjini kwake kama vile mchele, basi hakuna neno kama hizo pesa zitanunuliwa mchele na kisha kugaiwa kwa wanaostahiki.
Muda wa kuitoa kwa kauli sahihi ambayo Wanachuoni wameenda nayo kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi, ni kutolewa Zakaatul-Fitwr jua linaposhuka siku ya mwisho wa Ramadhwaan au Alfajiri ya siku ya 'Iyd kabla ya Swalaah ya 'Iyd kwa sababu ndio wakati wake na ndio lengo lake.
Ingawa kuna ikhtilaaf na kauli nyingi kuhusu suala hilo la muda wa kuitoa na kuna waliosema inaweza kutolewa hata mwanzo wa Ramadhwaan na wengine walioona inaweza kutolewa masiku kabla na wengine siku moja au mbili kabla kwa mapokezi yafuatayo:
Imepokewa kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhwiya Allaahu anhumaa) ambaye amesema: Walikuwa wakitoa Zakaat al-Fitwr siku moja au mbili kabla (Ya 'Iyd). [Al-Bukhaariy].
Ama kuhusu kutoa ziada kwa maskini kwa ajili ya kumtimizia mambo yake mengine na kumpa furaha na familia yake, hilo halikatazwi kwa mujibu wa Ahlul-'Ilm. Isipokuwa kama wapo maskini wengine na hawajapata Zakaatul-Fitwr, ni bora kutanguliza kuwapatia wao ili waifurahie sikukuu yao kuliko kumpa ziada mmoja.
Tafadhali soma Fataawa katika viungo vifuatavyo upate faida ziyada.
Fataawaa: Za Zakaatul-Fitwr
Fataawaa: Mukhtasari Wa Fataawaa Za Zakaatul-Fitwr
Na Allaah Anajua zaidi