Du'aa Za Kanzul-Arsh Na Du'aa Za Masiku Ya Wiki Zimethibiti?

 

Du'aa Za Kanzul-Arsh Na Du'aa Za Masiku Ya Wiki Zimethibiti?

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalaam aleiqum,

 

Suna budi na kumshukuru All Subhanahu wa Ta'aalaa alitujaalia akatufikisha katika kusherehekea kwa wenzetu waliopo Mecca Saudia kwa 'ibaadah tukufu, Rabb awajaliae Hijah makubul na awape malazi mema peponi waliotangulia mbele ya haki kutokana na msongomano uliokuwe Jamarat (amin) na inshalla Rabb alete subra kwa wafia wote.

Nimefurahi kupa jawabu langu ambalo nikilisubiri kwa muda mrefu, hata kufikia kukata tamaa, Allaah akubarikini ili muweze kwa uwezo wake Allah kutuongoza.

 

Umenifahamisha Bwana wetu Nabiy alivyokuwa akisali, na umenambia rakaa zake zilikuwa kumi na moja tu, ukiamisha ni kuwa pamoja na ile ya mwisho rakaa 1. Suali langu liko hapa nikifahamishe ninavyosali mimi kuanzia usiku wa kuamkia jumaapili mpaka usikuwa kuamkia Ijumaa kuamkia Jumaamosi na vitabu vyangu ninavyosema ili kama ninavyofanya ndivyo niendelee na kazi nakosema uweze kunielekeza.

 

Kwa kuanza:  Usiku wa Jumaapili:-  huanza na rakaa mbili za tahajudi na baada ya shahada soma majina ya Allaah 99 kwa kumshukuru allah na neema zake zote. Na sali tena tahajudi rakaa 2 na kusoma Kanji Laarsh. Naendelea na rakaa mbili nyeingine ambazo humsalia Nabiy wa kirefu, na baaada ya hapo ndio humalizia na witri mbili na  moja pekee. Baada ya kumalizia hapo hua kila siku na dua zangu za vitabu huwa nasoma na kumalizia na Quraan tukufu, adhana akiwa tayari nasali rakaa mbili Sunnat Subhi na kisha nasali faradhi. Nasalli Asharaq na ndio naelekea kibaruani.

 

Huu ndio utaratibu wangu wa wiki nzima pakiwa hapana udhuru wowote unaonitokezea. Ila siku ya Alkhamis husali baada hizo rakaa 2 - 2,  Tasbih  mwsiho nasali Witri.

 

Jumla hua nasalli Tahajudi 6,rakaa mbili witri na miwsho moja. Sujui hivi ninavyofanya ndivyo? Ningefurahi sana kupata muongozi.

Maasalam.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tunaona kwamba ulikuwa karibu ukate tamaa kupokea jibu la swali lako, tunapenda kukujulisha wewe na wengineo wanaotuma maswali yao kwamba, maswali yanazidi kila siku kumiminika mengi hadi yanatushinda nguvu, kwa hiyo kila anayetuma swali tunamuomba awe ana subira ya kupokea jibu lake kwani huwa tunajibu kwa mpango wa aliyetangulia, ila kama tunaona kuna ambalo linahitajia kujibiwa haraka sana ndio tunalijibu.

 

Vile vile tunamshukuru Allaah  Subhaanahu wa Ta'aalaa kuona kwamba dada zetu wengi wako katika jitihada kubwa ya 'ibaadah na khaswa kama 'ibaadah hiyo ya kuswali Swaalah ya Tahajjud ambayo ni 'ibaadah nzito kuitekeleza na yenye fadhila kubwa kama Anavyosema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa :

 

تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿١٦﴾فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٧﴾

Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa. Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda. [As-Sajdah 16-17]

 

Lakini, ili kuweza kupata malipo ya 'ibaadah zetu zote au vitendo vyote vyema, lazima kutimizwe masharti mawili haya yafuatayo ambayo wataalamu wa dini yetu wameyaweka kuwa ni asasi (msingi) ya kila 'ibaadah, na bila ya kupatikana masharti hayo mawili, basi huwa ni kazi bure, kwani Muislamu atajitahidi kwa kupoteza mali yake au wakati wake na pengine kujikalifisha kutekeleza hizo 'ibaadah au amali lakini zikawa hazina thamani yoyote mbele ya Rabb wetu hivyo asipate malipo yoyote kama Anavyosema Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa:

 

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya ‘amali yoyote ile, Tutayafanya   chembechembe za vumbi zinazoelea hewani zinazotawanyika. [Al-Furqaan:23]

 

Vile vile Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam  amesema:

((من عمل عملاً ليس عليه أمرنا فهو رد)) البخاري

((Atakayetenda kitendo kisichokuwa na mafunzo ya dini yetu basi kitarudishwa.)) [Al-Bukhaariy]   

 

Juu ya hivyo kwa vile itakuwa mtu amejiingiza katika uzushi ni hatari zaidi kwake kwani uzushi humpeleke mtu katika upotofu na moto kama alivyokuwa akisema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):   

((عليكم بسنتي وسنة الخلفاء الراشدين المهديين من بعدي ، تمسكوا بها وعضوا عليها بالنواجذ ، وإياكم ومحدثات الأمور، فإن كل محدثة بدعة ، وكل بدعة ضلالة)) و في رواية ((و كل ضلالة في النار))

((Kamateni Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa walioongoka baada yangu, zishikilieni na mzibane kwa magego (mzikamate kisawasawa). Na tahadharini na uzushi, hakika kila uzushi ni bid'aa na kila bid'aa ni upotevu)) [Abuu Daawuud  na At-Tirmidhy] na katika riwaya nyingine ((kila upotevu ni kwenye moto (wa jahannam))

 

Sharti zenyewe ni: 

1- Ikhlaasw – kwa maana kwamba 'amali iwe inafanywa kwa kutaka Ridhaa ya Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Pekee na sio kwa ajili ya mtu mwingine au kwa ajili ya maslahi ya kidunia.

 

2- 'Amali hiyo iwe  inatokana na mafundisho sahihi ya Qur-aan na Sunnah. Bila ya shaka ndugu yetu utakuwa umetimiza sharti la kwanza kuwa unaifanya 'ibaadah yako kwa ajili ya Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa  Pekee. Lakini tunaonaona kwamba sharti la pili hukuitimiza kwani hivyo unavyofanya sio kabisa kama ilivyo katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.  

 

Kutokana na maelezo yako, tumejumuisha kuwa Raka'ah unazoswali jumla kwa usiku mmoja ni tisa zikiwa pamoja na Raka'ah tatu za Witr. 

 

Idadi hiyo haina shaka wala hukosei, kwani unaweza kuswali kutokana na uwezo wako, Rak'ah tatu, au tano, au saba, au tisa au kumi na moja. Na hivyo ndivyo alivyokuwa akiswali Nabiy Swalla Allaahu 'aalayhi wa sallam kama tulivyosema hakuzidisha zaidi ya idadi hizo kumi na moja abadan katika maisha yake ikiwa ni Ramadhwaan au miezi ya kawaida kama tulivyoonyesha katika Hadiyth yake tukufu katika jibu la kabla ya hili. 

 

Katika idadi hizo zozote upendavyo kuswali, tatu za mwisho ziwe za Witr ambazo unasoma Raka'ah ya mwanzo na ya pili Suwrah Al-A'laa (Sabbihisma Rabbikal-A'aala) na Raka'a ya pili Suwrah Al-Kaafiruun (Qul Yaa-Ayyuhal-Kaafiruun) kisha unatoa salam na kumalizia na Raka'ah ya mwisho ambayo unasoma Suwrah Al-Ikhlaas (Qul-Huwa-Allaahu Ahad), Au mara moja unaweza kusoma pamoja na Suwrah hiyo  Suwrah Al-Falaq (Qul-A'uwdhu Birabbil-Falaq) na Suwrah Al-Naas (Qul A'uwdhu Birabbin-Naas).

 

Vile vile mara nyingine unaweza kuswali Raka'ah zote tatu kwa tahiyaatu (tash-shahud) moja tu ya mwisho, na baada ya kutoka kwenye rukuu, unaweza kusoma du'aa ya Qunuutul-Witr (Allaahummah-dina fiy-man Hadayta)

 

Na baina ya kila Raka'ah mbili haitakiwi kusoma chochote kama unavyofanya wewe kuwa kila baada ya Raka'ah mbili unasoma aidha Asmaau Allaahil-Husna (Majina Mazuri ya Allaah) au kusoma uradi wowote au kumswalia Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam kwa kirefu, bali unaendelea tu kuswali moja kwa moja hadi umalize Swalah ya Witr. Hivi ndivyo ilivyothibiti katika mafunzo ya Sunnah ya Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam.

 

Makosa mengine tunayoyaona unayotenda kutokana na maelezo yako ni hizo du'aa unazozisoma baina ya Swalah ya Tahajjud nazo ni hizi kama ulivyozitaja, na tunakuwekea hoja wazi kuhusu ubaya wake na kukupa zilizo sahihi badala yake.  

 

Uradi Wa Kanzul-‘Arsh  

Du'aa hii haijulikani kabisa katika vitabu vya Sunnah. Inavyoelekea imezushwa kutoka kwa Masufi na Mashia ambao wanaiita 'uradi wa kanzil-'arsh', nayo ni mkusanyiko wa du'aa na maneno yaliyotayarishwa kwa ajili ya wafuasi wao kusoma mara kadhaa katika hali kadhaa.

 

Na haifai kuwafuata katika nyiradi wanazozusha.  

 

Du’aa Za Wiki Nzima (Kila siku na Du’aa yake)  

Du'aa hizi pia nazo ni du'aa zilizopangwa na watu kuwa ni du'aa za wiki nzima, yaani kila siku na du'aa yake, kama "Du'aa ya Alkhamisi", "Du'aa ya Ijumaa" na kadhalika.

 

Ingawa baadhi ya du'aa humo zitakuwemo zilizothibiti katika Sunnah, lakini kwa vile zimepangwa kuwa kila moja ina siku yake khaswa, hili ni jambo lisilothibiti katika Sunnah na haifai kuzidumisha kusoma na kujipangia kuzisoma kama zilivyopangwa hivyo.

 

Swalaatut-Tasbiyh:

'Ulamaa wengi wameona kwamba Swalah hii haikuthibiti katika Sunnah, kwa sababu kuna udhaifu wa mmoja wa wapokezi wa hadiyth inayozungumzia Swalah hiyo! Nayo ni bora kuiacha.

 

Yote hayo juu ni mambo yasiyokuwepo katika sharia, hivyo inampasa Muislamu aepukane nayo na kufuata yaliyo katika mafundisho ya Sunnah.

Nabiy  Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam amesema:

((الدعاء هو العبادة ))  رواه أبو داود والترمذي. قال حديث حسن صحيح،

((Du'aa ni 'ibaadah)) [Abuu Daawuud na At-Tirmidhiy amesema Hadiyth sahiyh].

 

Na msingi wa mwanzo unaotakiwa au sharti katika 'ibaadah ni  tawqiyfiyah  yaani kuweka kisimamo kwa kutofanya ila kile kilivyoelezewa katika shariy'ah (mafundisho ya Qur-aan na Sunnah) na sio kwa kufuata yaliyozushwa na watu.

 

Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyah  Rahimahu Allaahu Amesema:

"Bila ya shaka dhikr na du'aa ni katika vitendo bora kabisa vya 'ibaadah na vifanyike vikiwa halisi na tawqiyf (kama ilivyoelezewa katika sheria, sio vilivyoanzishwa upya) na sio kwa kufuata mawazo, matamanio au uzushi. Du'aa na dhikr zilizosimuliwa na Nabiy Swalla Allaahu wa aalihi wa sallam ni bora kuliko du'aa zozote nyingine utakazozipata, na mwenye kujiweka katika mipaka nazo atakuwa yuko katika msimamo thabiti na salama. Manufaa yanayotoka na kupatikana humo hayawezi kufumwa katika maneno au kufahamika kikamilifu na binaadamu. Dhikr nyinginezo zinaweza kuwa ni haraam au makruuh, kwani zinaweza kuhusisha na shirki ambayo watu wengi hawatambui na ambayo maelezo yake yatachukua muda kufahamisha.

 

Hana haki mtu yeyote kuwatungia watu dhikr au du'aa ambayo haiko katika Sunnah na kuifanya kama ni kitendo cha 'ibaadah ya kawaida ili watu watende kama wanavyotekeleza Swalah tano za kila siku. Bali kufanya hivyo ni uzushi katika dini (bid'ah)  ambayo  Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Hakuruhusu. Ama kujipangia nyiradi au dhikr ambazo hazikutolewa mafunzo katika sheria, hili ni jambo lililokatazwa. Na juu ya hivyo du'aa na adhkaar ambazo zimetolewa mafunzo katika sheria ni bora kabisa na zinaongoza katika kufanikisha azma na lengo. Hakuna mtu anayeziacha na kufuata za uzushi isipokuwa ni mtu mjinga, mdharaulifu au mhalifu"

 

Mengineyo unayofanya kama kuswali Sunnah ya asubuhi, kisha kuswali fardh ya Alfajiri, kisha kubakia katika dhikr hadi kutoka jua (shuruuq) kisha ukaswali tena Raka'ah mbili ni jambo jema kabisa na thawabu zake ni kama mtu aliyefanya Hajj na 'Umrah kikamilifu kama ilivyothibiti katika Hadiyth sahihi.

 

Lakini vile vile dhikr zote utakazofanya ziwe za Sunnah na ukumbusho bora kabisa Muislamu kusoma ni maneno ya Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa nayo ni Qur-aan Tukufu ambayo fadhila zake zimetajwa katika Hadiyth nyingi sana na utazipata katika kiungo kifuatacho:

 

Fadhila Za Kusoma Na Kuhifadhi Qur-aan.

 

Kwa hiyo tunamalizia kwa kukupa nasaha njema ili unufaike na 'ibaadah yako kwa kuwa na uhakika wa matumaini ya kupata thawabu kuliko kupoteza wakati wako wa thamani na kufanya 'ibaadah ambayo haina uzito wowote mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Na hivyo tunatoa Swali hili alijibu kila anayefanya 'ibaadah isiyo ya Sunnah: 

Ikiwa umepewa du'aa na nyiradi za aina mbili:

 

1- Za uhakika kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  

2- Zilizotungwa na watu tu.

 

Je, ipi utakayoithamini zaidi?  

Bila shaka mwenye kumkhofu Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa na kumpenda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallamatazithamini du'aa zake na kuacha za watu.

 

Du'aa za wakati wowote, kwa jambo lolote au hali yoyote na nyiradi zote za asubuhi na jioni alizotufundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinapatikana zote katika kitabu cha Hiswnul-Muslim ambacho kinapatikana maduka ya vitabu vya Kiislamu na kina tasfiyr ya kila lugha na kinauzwa kwa bei nafuu kabisa.

 

Na hapa kipo katika mtandao wenu wa Alhidaaya.com

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

Na pia Duaa mbalimbali katika kiungo kifuatacho:

 

 

Dua Na Adhkaar

 

na khasa  Du'aa Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

 

Tunatumai utakuwa umefahamu maelezo na umetambua umuhimu wa kujiepusha na uzushi na kufuata Sunnah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share