Kuomba Du'aa Kwa Sauti Au Kimya Kimya Nini Maana Ya Unyenyekevu

SWALI:

Kwajina la mwenyezi mungu mwingi wa rehema , mimi naomba kuuliza.

{1} Jee kama mtu ukopekeyako labda umeamka usiku kuswali na ikafikia wakati wa kuomba duwa, jee katika kuomba kwako duwa bora ni vipi kuomba kwasauti kidogo au kimya kimya ndani ya moyowako?

{2} Jee kunatafsiri zaidi ya neno "UNYENYEKEVU"?        

 Salaam aleykum,

 


JIBU: 

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  Aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad

 

1)     Kuomba Du'aa

Miongoni mwa adabu za kuomba du'aa nyakati zozote ikiwa ni usiku au mchana ni kuomba kwa utulivu, upole, kwa khofu, ukiwe peke yako, na kwa sauti ndogo ndogo isiyosikika na watu walio karibu. Na kila ibada inapokuwa ni ya siri zaidi ndipo inapokuwa yenye thamani zaidi.

Anasema Allaah سبحانه وتعالى :

 ((ادْعُواْ رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً))  

((Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri))

[Al-A'araaf: 55]

Tuchukue mfano mzuri wa Zakariyaah عليه السلام  alipomuomba Mola wake mtoto akiwa katika hali ya uzee na mkewe akiwa tasa, alimuomba kwa siri :

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ 

((كهيعص))   ((ذِكْرُ رَحْمَةِ رَبِّكَ عَبْدَهُ زَكَرِيَّا))   ((إِذْ نَادَى رَبَّهُ نِدَاء خَفِيًّا))

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

((Kaf Ha Ya A'yn S'ad))

((Huu ni Ukumbusho wa rehema ya Mola wako Mlezi kwa mja wake, Zakariya))

((Alipomwita Mola wake Mlezi kwa siri))

Vile vile Anasema Allaah سبحانه وتعالى

((وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعاً وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالآصَال))

((Na mkumbuke Mola Mlezi wako nafsini kwako kwa unyenyekevu na khofu, na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni)) [Al-A'araaf: 205]

Maswahaba walipomuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم "Je, Mola wetu yuko karibu ili tumuombe kwa siri, au yuko mbali ili tupandishe sauti zetu? Allaah سبحانه وتعالى Aliteremsha aya:

((وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ))

((Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba)) [Al-Baqarah: 186]

Na katika Hadiyth sahiyh imerekodiwa kwamba Abu Muusa Al-Ash'ariy amesema: "Watu walipandisha sauti zao katika Du'aa wakati wakiwa katika safari. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akawaambia:

((أيها الناس، أربعوا على أنفسكم، فإنكم لا تدعون أصمَّ ولا غائبًا؛ إن الذي تدعونه سميع قريب))

((Enyi watu, jifanyieni wepesi nafsi zenu kwani Mnayemuomba sio kiziwi wala si mwenye kukosekana, bali mnayemuomba ni Mwenye Kusikia Aliye karibu))  [Al-Bukhaariy na Muslim]  

 

Lakini haina maana kwamba mtu aombe kimya kimya kabisa yaani moyoni, bali kwa ni kwa kunong'ona kabisa kama tulivyofundishwa kufanya katika Swalah na kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى

 ((وَلاَ تَجْهَرْ بِصَلاَتِكَ وَلاَ تُخَافِتْ بِهَا وَابْتَغِ بَيْنَ ذَلِكَ سَبِيلا))

((Wala usitangaze Swalah yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo)) [Al-Israa: 110]

2)     Maana ya unyenyekevu

Maana ya unyenyekevu ni khushuu (utulivu). Kwa maana kwamba unaposwali au kuomba du'aa, uwe ni mwenye kunyenyekea kwa unyonge, akili na moyo wako uwe mtupu usioshughulika na mengine yoyote isipokuwa ni khofu ya kuwa mbele ya Mola wako ukiyatia akilini na moyoni yale unayoyasoma au kuomba na ukikumbuka kuwa Yeye Anakuona ingawa wewe humuoni, hivyo utambue kuwa unazungumza na Mola Mtukufu, Mwenye kumiliki yote yaliyo mbinguni na ardhini na utukufu wote Alionao pamoja na Sifa Zake zote zisizomhusu mwingine yeyote. Na hapo ndipo utakapokuwa umepata sifa mojawapo ya miongoni mwa watakaokuwa wamefaulu na kupewa Pepo ya Firdaws kama Anavyosema Allaah سبحانه وتعالى 

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

((قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ))   ((الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ))

 

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU

((HAKIKA wamefanikiwa Waumini))

((Ambao ni wanyenyekevu katika Swalah zao))[Al-Muuminuun: 1-2]

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share