Swalaah Ya Sunnah Ya Alfajiri Inaswaliwa Vipi Na Wakati Gani? Na Surah Zipi Zisomwe?



SWALI:

Assalamu alaykum,

Je ni wakati gani mtu yampasa aswali ile swala kabla ya Salatul-Fajr, iliyo na ajra ya ulimwengu mzima na yote yaliondani ya dunia?



 

JIBU:

 Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Swalah ya Sunnah ya Alfajiri ambayo fadhila zake ni kuwa ina kheri kuliko dunia na yaliyomo huswaliwa baada ya adhaan ya Alfajiri kabla ya Swalah hiyo ya fardhi ya alfajiri.

عَنْ عَائِشَة رضي الله عنهاَ عَنِ النَّبِيِّ  صلى الله عليه وسلم ، قَالَ: َ((ركْعَتَا الْفَجْرِ خَيْرٌ مِنَ الدُّنْيَا وَمَا فِيهَا)) مسلم 

 Imetoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنهاَ kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Raka'a mbili za Alfajiri ni kheri kuliko dunia na yaliyomo ndani yake)) [Muslim] 

Tunaona jinsi gani fadhila kubwa zilizokuwemo katika Sunnah hii, na kuiswali haimchukui mtu zaidi ya dakika tano. Na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa haiachi kuiswali Sunnah hii pamoja na Sunnah ya Witr abadan hata alipokuwa safarini [Swahiyh Fiqhus-Sunnah 1:373]

Adaab za kuswali Sunnah ya Alfajiri:

Ufupi wake:

عن عائشةَ رضيَ اللّهُ عنها قالت: «كان النبيُّ صلى الله عليه وسلم يُخفِّفُ الرِّكعتَينِ اللتَّينِ قبلَ صلاةِ الصبحِ حتى إني لأقولُ: هل قرأَ بأُمِّ الكتاب)) البخاري

Imetoka kwa Bibi 'Aisha رضيَ اللّهُ عنها ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akizifupisha (kuswali) Raka'ah mbili ambazo ni kabla ya Swalah ya Asubuhi hadi nilikuwa nasema, je, amesoma humo Ummul-Kitaab (Suratul-Faatiha)? [Al-Bukhaariy]

Surah/Aayah za kusoma:

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه ، أَنَّ رَسُولَ اللّهِ قَرَأَ فِي رَكْعَتَيِ الْفَجْرِ: {قُلْ يَا أَيُّهَا الْكَافِرُونَ} و {قُلْ هُوَ اللّهُ أَحَدٌ}.  مسلم 

 Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma katika Raka'ah mbili (za Sunnah ya Alfajiri) (Qul-Yaa Ayyuhal-Kaafiruun) na (Qul-Huwa Allaahu Ahad) [Muslim]

 

 عن ابْنَ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما  أَنَّ رَسُولَ اللّهِ كَانَ يَقْرَأُ فِي رَكْعَتَيِ الْفَجْرِ: فِي الأُولَىٰ مِنْهُمَا: {قُولُوا آمَنَّا بِالله وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْنَا} (البقرة الآية: 136). الآيَةَ الَّتِي فِي الْبَقَرَةِ. وَفِي الآخِرَةِ مِنْهُمَا: {...آمَنَّا بِالله وَاشْهَدْ بِأَنَّا مُسْلِمُونَ} (آل عمران الآية: 52).  صحيح مسلم 

 Imetoka kwa ibn 'Abbaas رضي الله عنهما  kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma katika Raka'h za Alfajiri; ya kwanza akisoma (Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa sisi) [Al-Baqarah:136] Aayah iliyokuwa katika (Surah) Al-Baqarah na (katika) Raka'ah nyingine (...tumemuamini Allaah, na shuhudia kwamba hakika sisi ni Waislamu)  [Al'Imraan:52] [Sahiyh Muslim]

عَنِ ابْنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما  ، قَالَ: كَانَ رَسُولُ اللّهِ يَقْرَأُ فِي رَكْعَتَي الْفَجْرِ: {قُولُوا آمَنَّا بِاللّهِ وَمَا أُنْزِلَ إِلَيْنَا}. وَالَّتِي فِي آلِ عِمْرَانَ: {تَعَالَوْا إِلَىٰ كَلِمَةٍ سَوَاءٍ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمْ} (آل عمران الآية: 64).  صحيح مسلم 

Imetoka kwa ibn 'Abbaas رضي الله عنهما  amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma katika Raka'ah za Alfajiri (Semeni nyinyi: Tumemuamini Allaah na yale tuliyoteremshiwa sisi) na iliyokuwa katika [Suratul-'Imraan  64] (… njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi) [Al-'Imraan:64] [Sahiyh Muslim]

 

Kulala upande wa kulia baada ya kuswali Sunnah ya Alfajiri.

عن أَبي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه ، قالَ قالَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: «إذا صَلَّى أَحَدُكُمُ الرَّكْعَتَيْنِ قَبْلَ الصُّبْحِ فَلْيَضْطَجِعْ عَلَى يَمِينِهِ))  سنن أبي داوودو , احمد و البيهاقي

Kutoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema ((Anaposwali mmoja wenu Raka'ah mbili kabla ya Swalah ya Asubuhi ajilaze kwa upande wake wa kulia)) [Sunan Abi Daawuud, Ahmad na Al-Bayhaaqiy]

Kukidhiwa Sunnah hii na wakati wake.

Kwa jinsi ilivyo muhimu sana Sunnah hii ya Alfajiri hata ikiwa imempita mtu kwa dharura fulani ikafika hadi baada ya kutoka jua, basi ni bora kuikidhi kwa kuiswali kabla ya Swalah ya fardhi nayo ni kutokana na dalili:

عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((من لم يصلي ركعتي الفجر ؛ فليصلهما بعدما تطلع الشمس)) الترمذي و ابن خزيمة والحاكم وابن حبان

Imetoka kwa Abu Hurayrah رضي الله عنه ambaye amesema: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema: ((Asiyeswali Raka'ah za Alfajiri basi aziswali baada ya kutoka jua)) [At-Tirmidhiy, Ibn Khuzaymah, Al-Haakim na Ibn Hibbaan]

Lakini haina maana kwamba aliyeacha kuiswali asiiswali hadi litoke jua kama walivyosema Maulamaa, bali ni kwa yule ambaye hakuiswali kabisa kwa dharua hadi likatoka jua. [Swahiyh Fiqhus-Sunnah]

Ama ikiwa amewahi mtu kuamka kabla ya kutoka jua basi aswali Sunnah hii kwanza kisha ndio aswali Swalah yake ya fardh.

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share