Du’aa Zipi Kusoma Unapofikwa Na Shida, Dhiki Na Balaa?

 

Du’aa Zipi Kusoma Unapofikwa Na Shida, Dhiki Na Balaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam aleikum, ni zipi dua unapoona dhiki kwa mambo yaliyonifika?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Du’aa kadhaa zimethibiti kwa hali hiyo kama zifuatavyo:

 

Du'aa ukiwa na wahka  na huzuni 

 

Ibn Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yeyote atakayefikiwa na dhiki na huzuni kisha akasema:  

 

اللَّهُمَّ إِنِّي عَبْدُكَ، وَابْنُ عَبْدِكَ، وَابْنُ أَمَتِكَ، نَاصِيَتِي بِيَدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤُكَ، أَسْأَلُكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ سَمَّيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أَوْ عَلَّمْتَهُ أَحَدًا مِنْ خَلْقِكَ، أَوْ أَنْزَلْتَهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ اسْتَأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الْغَيْبِ عِنْدَكَ، أَنْ تَجْعَلَ الْقُرْآنَ رَبِيعَ قَلْبِي، وَنُورَ صَدْرِي، وَجَلَاءَ حُزْنِي، وَذَهَابَ هَمِّي

Ee Allaah hakika mimi ni mja Wako, mtoto wa mja Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako Ulilojiita  Mwenyewe au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yeyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe Mwenyewe (na kujihusisha kulijua) katika ’ilmu ya ghayb Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu, na sababu ya kuondoka wahka wangu -

 

Hakuna isipokuwa Allaah Atamuondoshea dhiki na huzuni na Atambadilisha badala yake faraja.” Ikasemwa: Ee Rasuli wa Allaah! Je tujifunze? Akasema: ”Ndio, inampasa kwa mwenye kuisikia kujifunza.” [Ameipokea Ahmad (1/391) [452], Al-Haakim (1/509) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika As-Silsilah Asw-Swahiyhah (199) na Al-Kalimi Atw-Twayyib (124)]

 

Pia,

اللّهُـمَّ إِنِّي أَعْوذُ بِكَ مِنَ الهَـمِّ وَ الْحُـزْنِ، والعًجْـزِ والكَسَلِ والبُخْـلِ والجُـبْنِ، وضَلْـعِ الـدَّيْنِ وغَلَبَـةِ الرِّجال.

“Ee Allaah hakika mimi najilinda kwako kutokana na wahka  na huzuni na kutoweza kwa uvivu na ubakhili na uoga na uzito wa deni na kushindwa na watu.”

 

Du'aa ya kupatwa na janga au balaa

 

لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ الْعَظـيمُ الْحَلِـيمْ، لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ رَبُّ العَـرْشِ العَظِيـمِ، لا إلَهَ إلاَّ اللَّهُ  رَبُّ السَّمَـوّاتِ ورّبُّ الأَرْضِ ورَبُّ العَرْشِ الكَـريم

"Hapana muabudiwa wa haki ila ni Allaah aliye Mtukufu, Mvumilivu, hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, Rabb wa  'Arshi  tukufu, hapana muabudiwa wa haki ila Allaah Rabb wa mbingu na Rabb wa ardhi na Rabb wa 'Arshi tukufu."

 

Pia,

اللّهُـمَّ رَحْمَتَـكَ أَرْجـوفَلا تَكِلـني إِلى نَفْـسي طَـرْفَةَ عَـيْن، وَأَصْلِـحْ لي شَأْنـي كُلَّـه لَا إِلَهَ إِلَّا أنْـت

"Ee Allaah rahmah Zako nataraji, usinitegemeze  kwenye nafsi yangu japo kwa muda wa kupepesa jicho, na unitengenezee mambo yangu yote, hapana muabudiwa wa haki ila Wewe"

Pia,

اللهُ اللهُ رَبِّي  لا أُشْـرِكُ بِهِ شَيْـئاً

“Allaah, Allaah, Rabb wangu simshirikishi na kitu chochote kile"

 

Pia du’aa ambayo ilimtoa Nabiy Yuwnus ('Alayhis-Salaam) katika  tumbo la samaki wakati alipodhikika humo:  

لاَ إِلَهَ إِلَّا أنْـت سُـبْحانَكَ إِنِّي كُنْـتُ مِنَ الظّـالِميـن

“Hapana muabudiwa wa haki ila Wewe, kutakasika ni Kwako.  Hakika mimi ni miongoni mwa waliodhumu nafsi zao”

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

Share