Mimi Ni Mji Wa Elimu Na ‘Aliy Ni Mlango Wake

 

 

Mimi Ni Mji Wa Elimu Na ‘Aliy Ni Mlango Wake

 

Abuu 'Abdillaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Mashia (Raafidhwah) huitumia sana Hadiyth hii: "Mimi Ni Mji Wa Elimu Na ‘Aliy Ni Mlango Wake'', kuitolea kama ni ushahidi wa utukufu wa Khaliyfah wa nne ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu), na kama ndio moja ya hoja yao kuu ya kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa ni bora kuliko Swahaba wengine na kwamba alistahiki kuwa Khaliyfah wa kwanza baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

 

Hapa Tutapata Maswali Yafuatayo Na Majibu Yachambuayo:

 

 

 

Maswali:

1. Ni nini makusudio ya Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),”Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake”, basi atakayetaka kuingia katika mji huo na apitie mlango wake.’?

 

 

2. Je, hii Hadiyth haimaanishi kwamba njia pekee ya kupata elimu – elimu ya kidini – ni ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kwamba njia zingine zote zilizotumika kupata elimu hiyo ni pungufu, na kwa sababu hiyo hazina umuhimu wowote katika Uislamu?

 

 

 

Majibu:

Kabla ya kutumia Hadiyth kutolea hoja ni lazima kwanza kuangalia kama hiyo Hadiyth imepokewa kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa njia (isnaad) sahihi au laa. Kisha baada ya kuhakikisha hivyo tujaribu kuangalia maneno (matni) ya hiyo Hadiyth na kuelewa kwamba yanamaanisha kitu gani. Kuielewa Hadiyth moja ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘layhi wa aalihi wa sallam) kwa maana ambayo itakuwa inapingana na kauli zake zingine nyingi, au ambayo itasababisha mabaya mengi, haiwezi kuwa sahihi. Badala ya hiyo kama kuna maana nyingine ya hiyo Hadiyth ambayo haipingani na kauli zingine za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ambayo haisababishi baya lolote basi maana hiyo ndiyo itakayokubalika na mtu yeyote mwenye akili timamu.

 

 

Kwa kuzingatia kanuni hii inatupasa kwanza tuangalie hadhi ya hii Hadiyth, ‘Mimi ni mji wa elimu’ kwa upande wa Riwaya (elimu ya kuchunguza sanad au mapokezi ya Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Katika vitabu Sahihi vya Hadiyth. Hadiyth hii imepokewa na At-Tirmidhiy peke yake na yeye ameisimulia kwa maneno, ‘Mimi ni nyumba ya hekima na ‘Aliy ni mlango wake’ badala ya ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake’. Raawiy (msimulizi) wake ni ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe. Baada ya kunukuu Hadiyth hii Imaam At-Tirmidhiy anasema yafuatayo kuhusu usahihi wake:

 

 

'‘Hii ni Hadiyth Ghariyb na Munkar. Baadhi yao wameipokea hii Hadiyth kutoka kwa Shurayk na hawakumtaja Sunaabihi katika sanad yake. Na hatuijui hii Hadiyth kutokana na Thiqah yeyote isipokuwa Shurayk.’'

 

 

Hadiyth Ghariyb, katika Istilahi ya Wanachuoni wa Hadiyth, ni Hadiyth ambayo inategemea mpokezi mmoja tu katika sehemu yoyote ya sanad yake, na Munkar ni Hadiyth ambayo si Ghariyb tu bali mpokezi wake (huyo mmoja) pia ni dhaifu. Kwa hiyo tunajua hadhi ya Hadiyth hii ya At-Tirmidhiy kwa upande wa Riwaya na pia kuitegemea kuweka msingi wote wa Dini ni kiasi gani.

 

 

Baada ya At-Tirmidhiy Hadiyth zote zenye maana hii zinategemea kitabu Al-Mustadrak cha Al-Haakim ambacho chenyewe hakihesabiwi katika vitabu vyenye kutegemewa vya Hadiyth. Yeye ananukuu Hadiyth mbili zenye matni tofauti kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na Jaabir bin ‘Abdullaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Riwaya ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake kwa hiyo mwenye kuukusudia mji huo basi apitie mlango wake’ na Hadiyth ya Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu)  ni, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake kwa hiyo mwenye kutaka kupata elimu basi na apitie huo mlango.’

 

 

Al-Haakim amedai kuwa Hadiyth hizi mbili ni Sahihi. Lakini kwa maoni ya wanachuoni wakubwa wa Hadiyth, Hadiyth hizi mbili na Hadiyth zingine zote katika mlango huu ni dhaifu na si zenye kutegemewa. Kuhusu Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Haafidh Adh-Dhahabiy anasema wacha kuwa sahihi, hii Hadiyth ni Mawdhuu’ na maoni yake kuhusu Hadiyth ya Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni, ‘Namshangaa Al-Haakim na ushujaa wake katika kusahihisha Hadiyth hii na Hadiyth zingine batili mfano wake, wakati huyu Ahmad (mmoja katika wapokezi wa Hadiyth hii) ni muongo sana.’

 

 

Yahya bin Ma’iyn anasema kuhusu Hadiyth hii, ‘Haina asli yoyote.’ Maoni ya Al-Bukhaariy ni kwamba, ‘Ni Munkar na haina sanad yoyote sahihi.’ An Nawawiy na Jazriy wanaitaja kuwa ni Mawdhuw’ (ya kutungwa). Haijathibiti vilevile kwa Ibn Daqiyq Al-‘Iyd. Ibn Jawziy amejadili kwa kirefu na kuthibitisha kuwa Hadiyth zote zenye maana ya ‘Mimi ni mji wa elimu’ hazina sanad hata moja sahihi.

 

 

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba, ni sahihi kiasi gani kutumia Hadiyth ambayo hali ya sanad yake ni hii! Kuamua maamuzi makubwa kama kuchukua elimu kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kumpitia ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yake na kuwaacha Swahaba wengine wote? Ni dhahiri kwamba hayo si maamuzi madogo. Baada ya Qur-aan mwongozo wetu ni maisha na mfano mwema ya Nabiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na ni Swahaba peke yao ambao wanaweza kutuambia miongozo ya Nabiy (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) katika nyanja mbalimbali za maisha yalikuwa yapi. Sasa kama tutategemea Hadiyth hii na kumfanya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu)      ndiye chanzo pekee cha elimu hiyo, basi bila shaka tutakuwa tunajinyima sehemu kubwa sana ya elimu hiyo iliyonukuliwa na Maswahaba wengine. Je, haiingii akilini kwamba ili tuweze kufanya maamuzi makubwa kama hayo basi tungekuwa na Hadiyth ambayo imetufikia kwa sanad yenye nguvu zaidi na yenye kutegemewa zaidi kuliko Hadiyth hii? Bali ingepasa iwe imenukuliwa kupitia si sanad moja tu bali sanad nyingi sahihi ili kusiwe na shaka kabisa kuhusu usahihi wake.

 

 

Tuangalie sasa, jinsi gani Hadiyth hii inapingana na Hadiyth zingine nyingi za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na matendo yake kama tutaielewa kwa dhahiri ya maneno yake. Nabiy (Swalla Allaahu ‘layhi wa aalihi wa sallam) aliwatuma Swahaba wengi kama viongozi wa majeshi yake katika misheni mbalimbali, Aliwateua kuwa magavana wa sehemu mbalimbali wa Dola ya Kiislamu, Aliwateua kukusanya Zaka, Aliwateua kuswalisha Swalah za Jamaa na kuwatuma katika miji tofauti tofauti kwenda kufundisha Uislamu. Haya ni mambo ambayo ni vigumu sana kwa mtu yeyote kuyakataa. Swali ni kwamba, je, kazi zote hizi zilifanywa bila ya hawa Swahaba kuwa na elimu ya Kidini? Au kwamba hawa Swahaba wote hawakuwa wanafunzi wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bali wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu)? Kama mambo haya mawili si kweli basi ukweli ni kwamba Swahaba wote hawa walipata elimu kutoka katika ‘Mji wa elimu’ au ‘Nyumba ya Hekima’ na wao wote pia ni milango yake kama ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Vilevile, mtu yeyote aliyesoma Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anajua kwamba kuanzia alivyopewa Utume hadi kufariki kwake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akilingania watu katika Uislamu na kuifundisha yeye peke yake. Na mtu yeyote aliyetaka kujua jambo lolote la Uislamu alikuwa akimuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) moja kwa moja na kupata jibu. Je, ilishawahi kutokea kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipata mafunzo fulani ya Uislamu kutoka kwa Allaah kisha akawa amemfundisha ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘amhu) peke yake mafunzo hayo na kumuachia yeye peke yake jukumu la kuyafikisha kwa watu wengine? Au, mtu akaja kwa Nabiy (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza swali na yeye akamuambia aende kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) au aje kwake kwa kumpitia ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu)? Kama yote hayo hayakutokea katika muda wote wa miaka 23 wa Utume basi kauli hii kwamba mlango wa mji wa elimu ni mmoja tu una maana gani?

 

 

Al-Haakim mwenyewe ambaye anasisitiza usahihi wa Hadiyth hii amepokea Hadiyth nyingi sana kutoka kwa Swahaba wengine katika kitabu chake Al-Mustadrak na kuna Hadiyth nyingi tu katika Hadiyth hizo ambazo zina mafunzo na maana ambayo hajanukuu kabisa kutoka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Swali ni kwamba kama Hadiyth hii ilikuwa sahihi kweli kwa Al-Haakim na mlango wa mji wa elimu ulikuwa ni mmoja tu basi milango hii mingine ilitoka wapi na kwa nini aliiendea (milango hiyo)?

 

 

‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe alikuwa akikanusha madai ya kwamba kuna mambo alifundishwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakumfundisha mtu mwingine yeyote. Kuna Hadiyth sahihi katika Al-Bukhaariy, Muslim na Musnad Ahmad zinazosema kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) alikanusha mara nyingi madai ya watu waliokuwa na fikra kama hizo. alitoa karatasi moja na kuwaambia watu kuwa zaidi ya yaliyoandikwa katika karatasi hii Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakunifundisha mambo yoyote maalumu. Karatasi hiyo ilikuwa na hukmu nne au tano za ki-Fiqhi. Kauli hii ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) imenukuliwa kupitia sanad 13 tofauti katika Musnad Ahmad. Tukikusanya Hadiyth zote hizi tunaona kwamba ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe alikanusha mara nyingi na katika nyakati tofautitofauti kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimfundisha jambo lolote la Uislamu amba lo hakumfundisha mtu yeyote mwingine. Watu wengi sana walimsikia akikanusha madai haya na yamewafikia Wanachuoni kwa kupitia sanad nyingi tofauti kiasi kwamba inakuwa vigumu sana kutia shaka kuhusu usahihi wake. (Angalia Musnad Ahmad (Chapa ya Daar ul Ma’arif Misri) Hadiyth nambari 599, 615, 782, 798, 858, 874, 954, 959, 962, 993, 1037, 1297, 1306).

 

 

Baada ya yote hayo, tukiangalia Hadiyth zingine za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zinazozungumzia fadhila za Swahaba wengine tunaona ya kuwa Hadiyth hii inapingana nazo zote. Katika Musnad Ahmad na At-Tirmidhiy kuna Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba Zayd bin Thaabit (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mwenye elimu ya mirathi kuliko Swahaba wengine. Kuhusu Mu’adh bin Jabal (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Yeye ni mwenye kujua Halaal na Haraam kuliko Swahaba wote. Kuhusu Ubay bin Ka’ab (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Yeye ni msomaji bora wa Qur-aan katika Swahaba.

 

 

Katika Musnad Ahmad, ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe anasimulia kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Laiti ningetaka kumteua yeyote katika umma wangu kuwa kiongozi bila kumshauri mtu basi ningemteua Ibn Ummi A'bd (‘Abdullaah bin Mas’uwd).’

 

 

Katika At-Tirmidhiy kuna riwaya ya Hudhayfah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Sijui nitabaki nanyi hadi lini, kwa hiyo wafuateni Abu Bakr na ‘Umar baada yangu.’

 

 

Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasimulia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ‘Aliysema,”Kila nabiy alikuwa na mawaziri wawili mbinguni na wawili ardhini; Mawaziri wangu mbinguni ni Jibriyl na Miykaiyl na ardhini ni Abu Bakr na ‘Umar.”

 

 

At-Tirmidhiy amepokea kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema, “Kama kungekuwa na Nabiy baada yangu basi angekuwa ‘Umar’.

 

 

Al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Sa’ad bin Abi Waqqaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuambia ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu),”Ee Mwana wa Khatwaab! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, shetani akikutana nawe njiani basi hubadilisha njia na kupita njia usiyoipita wewe.”

 

 

Abu Daawuwd kapokea kutoka kwa Abu Dharr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema,”Allaah Ameiweka haki katika ulimi wa ‘Umar na yeye (‘Umar) huitamka.”

 

 

Al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: “Niliota jana watu wakiletwa mbele yangu wakiwa wamevaa makanzu makubwa na madogo. Wengine kanzu zao zilikuwa zimefika kifuani, wengine chini zaidi. ‘Umar alivyoletwa alikuwa akiburuza kanzu yake. Swahaba wakamuuliza Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu tafsiri ya ndoto hiyo. Akasema,”Kilichokusudiwa kuwa ni kanzu katika ndoto hiyo ni Dini.”

 

 

Hadiyth hizi zimepokewa na Swahaba wengine. Hebu tuangalie Hadiyth alizozipokea ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) mwenyewe na zilizopo katika vitabu vya Hadiyth vyenye kutegemewa:

 

 

Katika Al-Bukhaariy, mtoto wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) Muhammad bin Al-Hanafiyyah anasema: ‘Nilimuuliza baba yangu, ‘Ni nani bora baada ya Nabiy?’ Akajibu: ‘Abu Bakr.’ Nikasema, ‘Na baada yake?’ Akajibu, ‘Umar.’ Baada ya hapo nikawa na shaka kwamba nikimuuliza tena atasema ‘Uthman kwa hiyo nikasema, ‘Na baada ya ‘Umar ni wewe sio?’ Akajibu, ‘Mimi ni mtu tu wa kawaida katika Waislamu.’’ Jibu hili linafanana kabisa na Siyrah tukufu na safi ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Ilikuwa kawaida ya mtu mwenye makamu ya juu katika Uislamu kama yeye kuepuka kutaja fadhila zake na badala ya hiyo kujiweka tu katika safu ya Waislamu wa kawaida.

 

 

Katika Musnad Ahmad kuna riwaya ya Al-Hasan bin ‘Aliy Radhwiya Allaahu ‘anhu (na riwaya hii iko katika At-Tirmidhiy na Ibn Maajah pia) kwamba baba yake, ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema, ‘Nilikuwa na (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakaja Abu Bakr na ‘Umar. Nabiy akasema:”Ee ‘Aliy! Hawa wawili ni viongozi wa watu wazima peponi baada ya Rusuli.’’ [Musnad Ahmad Hadiyth nambari 602]

 

 

Katika Hadiyth nyingine iliyopokewa na Ahmad, Al-Bazzaar na At-Twabaraaniy kwa sanad sahihi, ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasema: ‘Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa nani atakuwa kiongozi wa Waislamu baada yake? Akajibu: ‘Mkimfanya Abu Bakr kiongozi basi mtamkuta ni muaminifu, mwenye kuupa mgongo pesa (dunia) na mwenye shauku ya Akhera. Mkimfanya ‘Umar kiongozi basi mtamkuta ni mwenye nguvu, muaminifu na haogopi lawama ya mwenye kulaumu kwa ajili ya Allaah na mkimfanya ‘Aliy kiongozi na siwaoni mkifanya hivyo basi mtamkuta mwenye kuongoa, aliyeongoka na atawapeleka katika njia iliyonyooka.’ [Musnad Ahmad Hadiyth nambari 859]

 

 

Katika Musnad hiyo hiyo ya Ahmad imesimuliwa, kupitia sanad 26 sahihi, kwamba siku moja ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema juu ya minbar katika khutbah yake moja kwamba baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) watu bora wa Ummah huu ni Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na baada yake ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Wapokezi wa Hadiyth zote hizi ni Thiqaat (wenye kuaminika) na hakuna aliyejeruhiwa (yaani aliyetolewa makosa). Hadiyth 23 ni sahihi kutokana na elimu ya Mustwalah ul Hadiyth, 2 ni Hasan na moja tu ndiyo Dhwa’iyf. Katika Hadiyth hizo, 12 zimesimuliwa na Abu Juhayfah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye ni Swahaba na alikuwa ofisa wa Baytul Maal wakati wa Ukhaliyfah wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasema, ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alituuliza katikati ya khutbah yake, mnajua mtu bora wa Ummah huu baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ’alyahi wa aalihi wa sallam)  ni nani? Mimi nikajibu, ‘Ni wewe ewe Amiyr ul Muuminiyn.’ Akasema, ‘Hapana! Baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu bora katika Ummah huu ni Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na baada yake ni ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Mpokezi mwingine ni ‘Abd Khayr Hamdaani ambaye riwaya 13 zinaishia kwake, alipoulizwa, ‘Je, kweli ulimsikia ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu )akitamka maneno hayo?’ alisema, ‘Niwe kiziwi kama sikuyasikia kutoka kwenye ulimi wake yeye mwenyewe.’

 

 

Mpokezi mwingine ni Ibraahiym An-Nakha’iy anayesema, ‘Alqamah aliupiga minbar wa Msikiti wa Kufah na mkono wake na kusema, ‘Nilimsikia ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akihutubu juu ya minbar hii na kusema, mtu bora baada ya Nabiy alikuwa Abu Bakr na baada yake ‘Umar.’’ (Kusoma Hadiyth hizi angalia Ahmad Hadiyth nambari, 833 – 837, 871 – 878, 880, 909, 922, 932 – 934, 1030 – 1032, 1040, 1051, 1052, 1054, 1055, 1059, 1060).

 

 

Al-Bayhaqiy na Ahmad wamepokea kauli ya ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ‘Tulikuwa hatuoni ajabu kwamba Sakina inatamka juu ya ulimi wa ‘Umar.’

 

 

Al-Bukhaariy, Muslim na Ahmad wamepokea Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alivyouawa na maiti yake ilivyoletwa na kuwekwa juu ya meza tayari kwa kuoshwa watu waliizingira pande zote na kuanza kumuombea du’aa za kheri. Mtu mmoja akaja kwa nyuma yangu, kaniegemea na akasema, ‘Allaah Akurehemu. Sijawahi kutamani ningekutana na Rabb wangu na Amali za mtu yoyote zaidi yako. Natarajia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   Atakuweka pamoja na Masahiba wako wawili (yaani Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalih wa sallam na Abu Bakr  Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwani nilikuwa nikimsikia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)mara nyingi akisema, Nilikuwepo mahala fulani pamoja na Abu Bakr na ‘Umar, Nilifanya kazi fulani na Abu Bakr na ‘Umar, Nilienda mahali fulani na Abu Bakr na ‘Umar.’’ Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anasema, ‘Nilivyogeuka kutazama ni nani anayesema maneno hayo nikakuta ni ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu.)’

 

 

Sasa jambo la kuzingatia ni kwamba kama kweli Hadiyth ‘Mimi ni mji wa elimu…’ ni sahihi na ina maana ileile ambayo huchukuliwa, basi tusemeje kuhusu Hadiyth zingine nyingi kuhusu fadhila za Swahaba wengine zilizowaridi na sanad sahihi zaidi kuliko ya Hadiyth hii? Tuzikatae vipi Hadiyth zote hizo kwa Hadiyth hii ambayo ina sanad dhaifu na yenye mashaka. Kama hatuwezi kuzikataa basi je, tunaweza kuipa Hadiyth hii tafsiri nyingine ili ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) abaki kuwa mlango wa mji wa elimu na pia kauli zingine zote za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) mwenyewe kuhusu Swahaba wengine yabaki kuwa ya kweli? Kwanza kabisa kuna Hadiyth nyingi sahihi kuhusu fadhila za ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na wala hakuna upungufu wa Hadiyth hizo katika vitabu vya Hadiyth na kwa hiyo hakuna haja kuleta Hadiyth kama hii ambayo sanad yake ni mbovu kuliko Dhaif kutokana na ‘Ilm ya Mustwalah ul Hadiyth. Kama kuna mtu ambaye atang'ang'ania kuwa hii Hadiyth ni sahihi basi sehemu hii, ‘kwa hiyo mwenye kuukusudia mji huo basi apitie mlango wake’ ya Hadiyth hii si sahihi kabisa kwa sababu inapingana na kauli za (Nabiy Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zingine na vilevile na vitendo vya maisha yake yote na pia na kauli zake ‘Aliy (Radhwiy Allaahu ‘anhu) mwenyewe. Sana sana tunaweza kukubali sehemu ya Hadiyth hii ya kwanza ambayo ni, ‘Mimi ni mji wa elimu na ‘Aliy ni mlango wake’ kuwa ni sahihi na hiyo pia si kwa maana ya kwamba mlango wa mji huo ni ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) peke yake bali kwa maana ya kwamba mji huo una milango mingi na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni mlango mmojawapo wa milango hiyo. Maana hii ni sahihi na inakubaliana na kauli na vitendo vya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.

 

 

Wa Allaahu A'lam

                                     

Share