Ukweli Juu Ya Al-Kaafiy (Kitabu Cha Hadiyth Cha Kutegemewa Cha Mashia)
Ukweli Juu Ya Al-Kaafiy (Kitabu Cha Hadiyth Cha Kutegemewa Cha Mashia)
Imeandikwa Na Fayswal Nuur
Imetafsiriwa na Muhammad Faraj
Utangulizi
Hakika Shukrani zote anazistahiki Allaah, na sala na salaam zimfikie bwana wetu Muhammad pamoja na aali zake wema waliotahirika na Swahaba wake wote – Amma baad,
Nimegundua kuwa unapojadiliana na baadhi ya wenye kufuata madhehebu ya Kishia ukataka wakupe dalili juu ya itidaki zao, hukimbilia kukuletea dalili kutoka katika vitabu vya madhehebu ya Kisunni.
Watakuletea ama hadithi inayojulikana kuwa ni dhaifu au watakuletea hadiyth sahihi lakini wataigeuza maana yake ipate kunasibiana na hoja yake.
Wanajaribu kumpa fikra yule wanayejadiliana naye kuwa wana ushahidi kutoka katika vitabu vya Kisunni, lakini ukweli ni kuwa wao wanajaribu kumkimbiza mbali na vitabu vya Kishia. Na unapojaribu kutoka ushahidi katika vitabu vyao, watakwambia maneno yale yale wanayopenda kuyasema, nayo ni kuwa;
"Nani aliyekwambia kuwa sisi tunaziamini hadithi zote zilizomo ndani ya kitabu cha Al-Kulayniy kiitwacho Al-Kaafiy?"
Sisi tunawauliza; 'Kwa nini basi hamuzifanyii tahakiki hadithi hizo pamoja na wapokeaji wake? Kwa nini hamzikanushi wala kukanusha yale yaliyomo ndani ya kitabu hicho yenye kufundisha shirki pamoja na matusi kwa wake za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba wake (Radhwiya Allaahu 'anhum)?"
Hapo ndipo ukweli unapoonekana.
Daraja Ya Al-kulayniy Kwa Mashia
Al-Kulayniy anahesabiwa kuwa ni muandishi wa kitabu kitukufu kupita vyote katika madhehebu ya Kishia, na kitabu chake ndiyo chimbuko la mafundisho yote ya madhehebu yao, na wanaamini kuwa ni kitabu kinachoaminika kupita vitabu vyote, hata kupita [Al-Bukhaariy na Muslim].
Katika utangulizi wa kitabu chake kiitwacho 'Al-Kaafiy', na maana yake ni 'chenye kutosheleza', Al-Kulayniy mwenyewe akikisifia kitabu hicho ameandika yafuatayo;
‘’Nikasema kuwa utapenda uwe na kitabu kitakachokutosheleza, kitakachokusanya kila fani ya elimu ya dini, kitakachomtosheleza mwanafunzi, na anachoweza kukirudilia kila mwenye kutaka mwongozo, na atakachochukuwa ndani yake kila mwenye kutaka elimu ya dini na kukifanyia kazi kwa dalili zilizo sahihi zitokazo kwa wasemakweli.’’
Utangulizi wa kitabu cha Al-Kaafiy ukurasa wa 7
Anasema Ali Akbar al Ghafari aliyekifanyia tahakiki kitabu cha Al-Kaafiy;
‘‘Mashia wa Imamia wote wamekubaliana juu ya usahihi wa yaliyomo ndani ya Al-Kaafiy.’’
Anasema Abdul Hussein Sharafuddin;
‘‘Na bora kupita vyote ni hivi vitabu vine ambavyo ni marudio ya madhehebu ya Imamia (Ithnasheri) katika asili ya mafundisho yao na katika matawi yake, Mafundisho yaliyotokana na asili za mwanzo ya madhehebu mpaka kufikia wakati wetu huu. Na vitabu vyenyewe ni Al-Kaafiy na Attahadhiyb na Al Istibsar na Waman la yahadhuruhul faqiyh, na hadithi zake ni Mutawatir (zilizopokelewa kupitia njia nyingia sana kupitia tabaka mbali mbali na zama mbali mbali) na yaliyomo ndani yake vitabu hivi ni sahihi isiyo na shaka yoyote ndani yake, na Al-Kaafiy ni cha zamani kupita vyote na kitukufu kupita vyote na bora kupita vyote na kimeandikwa kwa ufundi kupita vyote.’’
Al Murajaat 335 na 110 – chapa ya Sadeq, Beirut.
Anasema pia Al Faidh al Kishani baada ya kuvisifia vitabu vine hivyo;
‘’Na Al-Kaafiy kinaheshima zaidi kupita vyote, na kitukufu kupita vyote, na kinachoaminika kupita vyote, na kilichokamilika kupita vyote, na ndicho kilichokusanya mengi kupita vitabu vyote.’’
Amesema haya katika Utangulizi wa tahakiki ya kitabu ya Al-Kaafiy ukurasa wa 9, juu ya kukubali kwake kuwa Al Majlisi amesema kuwa hadithi nyingi zilizomo ndani ya kitabu hicho si sahihi.
Anasema Attubrusiy;
"Al-Kaafiy baina ya vitabu vine ni mfano wa juwa baina ya nyota, na mtu anapotafakari akafanya insafu ataacha kutizama upande mmoja wa upokezi wa watu wake na matokeo yake atapata uhakika na matumaini juu ya ukweli wake na uthibitisho wake."
Mustadrak al Wasail 3/532
Ama Al Hur al Amiliy yeye anasema;
"Faida ya sita ni kuwa tumepata uhakika wa ukweli wa muandishi wa kitabu hiki, na ukweli uliomo ndani yake, pamoja na kuthibitisha kuwa yote yoliyomo yanatokana na Maimamu alayhimu ssalaam."
Khatimatu al Wasail,ukurasa – 61
Ama Agha Barzak yeye anasema;
"Hiki ni kitabu kinachoheshimika kupita vyote vine vya asili vinavyoaminika, hakijapata kuandikwa kitabu mfano wake kinachonukuu kutoka kwa watu wa nyumba ya Nabiy."
Ama Abbas Al Qummy yeye anasema;
"Ni kitabu kinachoheshimika kupita vyote katika vitabu vya kiislamu, na kitukufu kupita vyote katika vitabu vya Imamiya (Ithnasheri), na ambacho hakijapata kutunguwa mfano wake katika madhehebu ya Imamiya."
Anasema Muhammad Amin al Istrabadi;
"Tumesikia kutoka kwa mashekhe wetu na maulamaa wetu kuwa hakijapata kutungwa katika uislamu kitabu kinachoweza kufananasishwa au hata kukikaribia kitabu hiki."
Al Kunyiya wal Alqab 3/98
Anasema Muhammad Sadeq al Sadar katika kitabu chake kiitwacho 'Al Shia'. Ukurasa wa 122;
"Inasemekana kuwa Al Mahdi mwenyewe alipewa akisome kitabu cha Al-Kaafiy kisha akasema; "Hiki kitawatosheleza Mashia wetu."
Mlango;
Vipi kitabu hiki kitakuwa na isnadi sahihi au hadithi zake zitakuwa Mutawaatir (zilizopokelewa kupitia njia nyingi sana kupitia tabaka mbali mbali na zama mbali mbali) wakati inaelekea muandishi wake hajuwi hata isnadi. Mwenye kukisoma anaona kuwa Al-Kulayniy huyu katika hadithi zake nyingi anaanza bila kutaja majina ya watu alopokea hadithi kutoka kwao. Anaanza kwa kusema kwa mfano;
"Kutoka kwa sahibu zetu wingi…" kisha anaiandika hadithi.
Na hii ni dalili kuwa wapokezi wake hawajulikani hata majina yao, kwa sababu asili ya elimu ya hadithi ni kutaja majina ya wapokezi wapate kujulikana ni watu wa aina gani.
Hamna ndani ya vitabu vyao njia inayofahamika ya upokezi wa hadithi wala vidhibiti maalum, na utawaona wanasukuma tu.
Hebu tumsikilize Abdul Hussein anasema nini juu mmojawapo wa wapokezi wao anayeitwa Zurarah aliyepokea hadithi nyingi sana kutoka kwa Ja’afar asw-Swaadiq;
Anasema Abdul Hussein;
"Hatujaona chochote kibaya katika yale wanayomnasibisha nayo (Zurarah) wapinzani wetu na wanamsingizia uongo kwa ajili ya uadui tu na kuvuka kwao mipaka."
Al Murajaat ukurasa 110 – kimepigwa chapa na Al Aalamiy
Na katika vitabu vingine vya madhehebu yao utaona wanaleta hadithi zilizopokelewa kutoka kwa Ja’afar mwenyewe kuwa amesema;
"Zurarah ni muongo – Allaah amlaani Zurarah, Allaah amlaani Zirarah, Allaah amlaani Zurarah."
Na imepokelewa pia kuwa Ja’afar amesema;
"Akiumwa Zurarah usende kumtizama wala akifa usilishuhudie jeneza lake. Zirarah ni shari kupita Mayahudi na Wakristo."
Na akasema;
"Allaah ameupinda moyo wa Zurarah."
Yote haya yamo katika kitabu cha 'Rijaal al-Kushiy' ukurasa 160 na al Mamqani katika kitabu cha 'Tanqiyh al Maqaal' juz. 1 ukurasa 444
Zurarah huyu ni mpokezi wa hadithi nyingi zilizotoka kwa Ja’afar (Radhwiya Allaahu 'anhu), bali ni mpokezi wao maarufu kupita wote na hii ndiyo hali yake kama mlivyoona. Na juu ya yote hayo utawaona wanavishambulia vitabu vya Ahlus-Sunnah na kusema kuwa Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ni muongo.
Ikiwa wanamsingizia uongo Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyeombewa dua na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili aweze kuhifadhi, kwa nini basi wanazikubali hadithi zilizomo ndani ya Al-Kaafiy 1/385 zinazosema kuwa; Al-Hasan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akijuwa lugha milioni sabini.
Bali Al-Kulayniy huyu aliyeandika kitabu cha Al-Kaafiy anadai kuwa Allaah Anampa Imamu uwezo wa kujuwa lugha zote na kujuwa nasaba za watu wote na lini watakufa, na kwamba wamepewa uwezo wa kujuwa mambo mbali mbali, na kwamba Imamu wanayo elimu ya yaliyokwishatokea na yatakayotokea na kwamba hapana kinachoweza kufichika kwao na kwamba wanao uwezo wa kuhuisha na wa kuuwa."
Al-Kaafiy 1/426, na katika juzu hiyo hiyo pia ukurasa wa 204-217 na 225
Atakayejaribu kukipitia kitabu cha Al-Kaafiy ataona kuwa karibu kitabu chote kinazungumza juu ya yafuatayo:
1. Ushirikina; kutufu katika makaburi kuwa eti sawa na kutufu Al Kaaba (Al-Kaafiy – 1/287 Kitaabul Hujjah).
2. Allaah hata ndani ya Swalah. Imeandikwa katika Al-Kaafiy juz 2 ukurasa 406;
3. “Sema katika sajdah yako ya mwisho; 'Ewe Jibril, ewe Muhammad, Ewe Jibril, Ewe Muhammad, nitoshelezeni katika niliyonayo."
4. Imamu wamepewa majina ya Allaah. Kwa mfano; Jicho la Allaah, Uso wa Allaah, mkono wa Allaah, Nuru ya Allaah nk.
5. Imamu wao wanayo elimu ya ghaibu isiyo na upeo, na mmoja wao anajuwa lugha milioni sabini.
6. Itikadi kuwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ndiye atakayeamua nani atakayekwenda Peponi na nani atakayekwenda Jahannam.
7. Daraja ya Imamu na elimu yao ni kubwa kupita daraja na elimu ya Rusuli (‘Alayhis-salaam).
8. Kuwatukana wake za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwita Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa ni adui wa Allaah na wa Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
9. Kuwa Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhu) wamertaddi isipokuwa watatu tu.
10. Kumtukana Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuitakidi kuwa eti wamemletea udhia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kunasibiana nao. (Al-Kaafiy 1/241).
11. Kuwatukana ‘Ulamaa wa Kiislamu na kuwakufurisha hasa kumalaani Imam Abu Haniyfah.
12. Kuwatukana na kuwalaani watu wa Shaam na watu wa Makkah na watu wa Madiynah na kwamba eti watu wa Madiynah makhabithi kuliko wakristo.
13. Itikadi kuwa kila asiyekuwa Shia, ataingia Motoni na atakuwa humo milele na hakimfai chochote katika amali zake hata ziwe nyingi namna gani.
14. Amri ya kuosha mkono baada ya kusalimiana na 'An Naswibiy', na An Naswibiy kwano ni kila asiyeamini juu ya Imamu wao.
15. Nk.