Kumuoa Mwanamke Mwenye Hiv Bila Ya Kufanya Kitendo Cha Ndoa

SWALI

Assalaamu 'alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh,

Bismillahi Rahman rahiym.

Ndugu zangu katika imani naomba munifahamishe ikiwa inafaa kumuoa mwamke mwenye HIV kwa lengo la kumnusuru tu iwapo nimemuona ana imani mzuri. Nia ikiwa ni kumuondolea mawazo na kujaribu kumjenga kiimani bila kufanya tendo la ndoa. Kwani ameupata ugonjwa kwa njia tofauti na zinaa naomba ufafanuzi Tafadhali.




JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani kwa ndugu yetu kwa swali lako hilo kuhusu ndoa na mwenye ukimwi. Ni swali zuri hasa katika wakati huu ambao wenye ukimwi wanaume na wanawake huwa wanatengwa kwa njia moja au nyingine. Japokuwa ni maarufu kuwa kwa kutangamana nao, kula nao, kucheza nao, kuzungumza nao, ukimwi huwa haumuambukizi mwingine. Ni kwa sababu hii ya kutowajali waathiriwa hao ndio wanachukuliwa na Makanisa na hata wakati mwingine kubadili Dini yao ya asili kwa sababu ya kushughulikiwa huko na wasiokuwa Waislamu.

 

Hakika ni kuwa Uislamu umehimiza sana wagonjwa kutazamwa kwa roho safi na kuhudumiwa na watu wao. Kwa kufanya hivyo, wagonjwa huwa wanapata utulivu, moyo mkunjufu na kujiona ya kuwa bado watambulikana na jamii yao. Tufahamu kuwa ugonjwa wa ukimwi haupatikani tu kwa zinaa japokuwa hiyo ndio njia ya msingi, lakini hupatikana kwa kuwekewa damu ambayo labda haijapimwa, kwa kudungwa sindano ambayo si ima ya kutumiwa mara moja (disposable) au ya kuchemshwa, kutumia vifaa kama wembe ambao una mabaki ya damu na njia nyinginezo mbalimbali za kuambukiza.

 

Lakini katika swali hili, awali ya yote tutazame nini umuhimu wa ndoa katika Uislamu. Inaeleweka kuwa umuhimu mkubwa wa ndoa ni kujiepusha na machafu ya zinaa na kuendeleza kizazi cha binadamu katika huu ulimwengu. Swali ambalo linafaa tujiulize ni, kwa kumuoa msichana mwenye ukimwi ili kuongeza Imani yake malengo yanapatikana? Kuoa kunakuwa ni kuweza kwa wanandoa kuingiliana kimwili na tendo hilo la ndoa huwa haliwezi kufanyika kwa kumuoa mwenye ukimwi. Hili linaweza kukupelekea wewe kwa sababu ya kutaka kutimiza uchu wako wa kimaumbile uende kwa wanawake wengine na hivyo kuingia katika dhambi. Huenda pia msichana asikuelewe lau atawasikia wenziwe ile raha wanayoipata katika ndoa ilhali yeye haipati. Kwa minajili hiyo, huenda akakushurutisha ufanye naye tendo la ndoa kama wengineo na unapomueleza asiwe ni mwenye kukuelewa. Tatizo hili linaweza kusababisha ima ufanye naye tendo la ndoa au ukatae na hapo vurugu litokee mpaka atake kuachwa.

 

Katika Uislamu, haifai kwa mtu kujipeleka kwenye maangamivu kwa mikono yake mwenyewe. Vile vile, haifai kudhulumu wala kudhulumiwa kwa njia yoyote ile. Kwa kumuoa mke ana hiyo utakuwa inajidhulumu au utajiangamiza kwa mikono yako mwenyewe na hilo halifai kwa Muislamu.

 

Lau utakuwa na mke mwengine ambaye unaweza kutimiza haja zako za kimwili na ukawa ni mwenye kuzungumza na huyo msichana pamoja na wazazi wake mpaka wakakuelewa lengo hasa la wewe kutaka kumuoa basi itakuwa hakuna neno kwani utakuwa umesaidia kuondoa tatizo katika jamii. Nasiha yetu ni kuwa utahadhari sana usije ukaingia katika madhara, kudhulumu, kujidhulumu na maovu mengine.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share