Mume Wangu Hataki Kuswali Anasema Hakuna Allaah!
SWALI:
Asalama aleykum,
Je mume wangu hataki kuswali na kuna wakati kuligombana akasema kuwa hakuna mungu (Allaah) je mimi nifanyeje?
wasalam binti wa kislamu
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani dada yetu katika Imani. Huenda kuanzia mwanzo ulifanya makosa kwa kumkubali mume asiyetekeleza amali ya Swalah, kwani kuolewa na asiyeswali ni kujitakia maudhi kutoka kwake. Lakini hilo tuliache kwani ni kosa ambalo tayari limefanyika na hatuwezi tena kurudisha wakati nyuma ili tupate suluhisho.
Kwa maelezo yako hili lililokuja ni kubwa zaidi kuliko la mwanzo la kutoswali. Kukataa kuwa hakuna Allaah ni kujitoa katika Uislamu. Nasaha ambayo tunaweza kukupatia dada yetu ni wewe kama mke uzungumze naye kwa makini ujue alimaanisha nini kwa kusema hakuna Allaah (Mungu Apasaye kuabudiwa kwa haki). Ikiwa anasisitiza kuwa hivyo ndivyo alivyosema basi itisha kikao baina yako, wazazi wako, wazazi wake na mumeo ili mujadili suala hilo kwa uwazi kabisa. Ikiwa atakana basi itakuwa ni lazima muachane kwani mwanamke wa Kiislamu haolewi na mtu ambaye haamini Allaah au ikiwa atakiri makosa yake na akatubia basi inabidi arudi katika Uislamu. Jambo hilo la pili litakapotokea katika kikao hicho inabidi usikomee hapo bali mujadili suala la yeye kutotaka kuswali. Lau itakuwa kwamba yeye atashikilia uamuzi wake wa kutoswali basi itakuwa ni bora utake talaka mbele ya wazazi wake kwani kukaa naye ni kutaka kufikiwa na matatizo mengine. Mojawapo ya tatizo ni yeye pengine kukughuri wewe nawe pia uache Swalah ambayo ni amali kubwa sana.
Tunakutakia kila la kheri na mafanikio na kuondokewa na tatizo hilo.
Na Allaah Anajua zaidi