Kufuturu Katika Mkahawa Unaouzwa Ulevi

SWALI:

 

Assalaam alaykum,

 

Napenda kuuliza, Kama mtu anafanya kazi nchi ambazo hakuna waisilamu wengi, na ana rafiki zake ambao wanafaya kazi sehemu tofauti tofauti, na wanafunga Ramadhaani na wakapata mama wa Kiislam, na kumuomba aweze kuwa anawapikia futari kila siku wakitoka kazini na ili waweze kukutana sehemu na kufuturu pamoja, na walipokuwa wanatafuta sehemu ya kukutana na kufuturu pamoja, kwa bahati wakapata sehemu ya kuweza kukutana na kufuturu pamoja, lakini sehemu hiyo ni restaurant pia huuza bia, lakini kuna sehemu wakapewa wawe wanafuturu. Je futari hii inasihi?  kwani hiyo restaurant ndio pekee wanaweza kupikiwa na huyo mama na kuweza kukutana na kufuturu pamoja. Ahsante.

 







JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Hakika ni kuwa si rahisi Muislamu akose sehemu nyingi za kula na kupikiwa futari isipokuwa katika hoteli ya asiyekuwa Muislamu. Je, kabla ya Ramadhaan ndugu hawa walikuwa wakila wapi? Je, hawa ndugu hawana nyumba zao? Ikiwa hawana, je, wanaishi sehemu gani ya mji huo? Je, huyo asiyekuwa Muislamu kwa kukubali kupikwa chakula kwake atakuwa na masharti aina yoyote au ni vipi?

 

Sehemu hiyo ina utata mwingi sana hasa ukizingatia kuwa kunauzwa pombe na Muislamu hafai kukaa sehemu kama hiyo hata kama hatakunywa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ashakataza kukaa kwenye sehemu inayotembezwa pombe. Na pia katika Hadiyth ya Abu ‘Abdillaah an-Nu‘maan bin Bashiyr (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) anasema kwamba amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Hakika halali iko wazi na haramu pia iko wazi, na baina ya vitu hivi viwili kuna mambo yenye shaka, ambayo watu wengi hawayajui. Basi mwenye kuepuka mambo yenye shaka, hakika amehifadhi Dini yake na heshima yake” (al-Bukhaariy na Muslim). Ikiwa uchaji Mungu ni kuepukana na jambo lenye shaka seuze kuepukana na jambo ambalo halina shaka kabisa kuwa limekatazwa.

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka” (at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy). Kuuliza kwako ni kuwa una shaka tele moyoni mwako hivyo tafuteni sehemu mbadala.

 

Ushauri wetu ni kuwa mtafute sehemu nyingine msiwe ni wenye kula futari yenu katika sehemu hiyo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share