Waislam Tuache Kumzulia Uongo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Waislam Tuache Kumzulia Uongo Nabiy

 

(Swalla Allaahu ‘Alayhi wa Aalihi Wa Sallam)

 

Abu Faatwimah

 

Alhidaaya.com

 

Assalamu 'alaykum,

 

Ndugu Waislam,

 

Barua pepe (Email) yoyote ile yenye kusema kama hivi ‘Read if you are muslim’ na namna hii ni vyema usiisome wala usiitume kwa mtu kwani yaliyomo ndani mara nyingi huwa ni mambo yenye kwenda kinyume na mafundisho ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au ni uzushi au uwongo unaotungwa na waongo kutaka kuwaharibia Waislamu Dini yao na kuwapoteza na mafundisho sahihi ya Dini yao, hivyo ni vyema ui-delete na umnasihi mwenye kawaida ya kukutumia email kama hizo kuwa ndoto ni jambo linalomuhusu mwenye kuota na sio mwengine katika sisi, na kama ndoto ni njema/nzuri basi anachotakiwa ni kumuomba Allaah Amuwafikishe akipate hicho alichokiota kama ni kizuri na kama kinyume chake basi amuombe Allaah Amuepushe na shari hiyo na amkinge.

 

Sasa na tuingie ndani ya habari inayotakiwa isomwe kama sisi ni Waislamu na itumwe kwa wengine ili mambo yetu yawe mazuri yatengenekee.

 

Dont Delete! If Yo Are A Muslim! Please Read This!

 

Wapi tunatakiwa au tunapendekezewa kutumia matamshi (tishio) kama,

 

If You Are A Muslim!

 

Ukiwa na urafiki/ushoga na Qur-aan itakushika mkono na kuudhibiti mdomo wako na kukupelekea kwa tawfiki yake Rabb kutumia matamshi kwa munasaba wake sio kuyatupa kama mtoto anayejifundisha kusema, matamshi kama haya If You Are A Muslim! pahala pake ni kama hapa:

 

Kama Wewe Muislamu Basi Mbona Huswali!

Kama Wewe Muislamu Basi Mbona Husomi Qur-aan!

Kama Wewe Muislamu Basi Mbona Huvai Hijabu Au Mkeo Mbona Havai!  Angalia kwa utulivu wapi Qur-aan imetumia tamshi If you are a Muslim!

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema katika Qur-aan:

 

فَإِلَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّمَا أُنزِلَ بِعِلْمِ اللَّـهِ وَأَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ

Wasipokujibuni, basi jueni kwamba hakika (hii Qur-aan) imeteremshwa kwa ujuzi wa Allaah, na kwamba hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye; basi je, nyinyi hamtokuwa Waislamu? [Huwd: 14]

 

Pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema katika Qur-aan:

 

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا قَوْمِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ فَعَلَيْهِ تَوَكَّلُوا إِن كُنتُم مُّسْلِمِينَ

Na Muwsaa akasema: Enyi kaumu yangu! Ikiwa mmemwamini Allaah; basi Kwake mtawakali, mkiwa ni Waislamu. [Yuwnus: 84] 

 

From Madina Sheikh Ahmed fell asleep reading the Quraan.

 

Tunatakiwa tuisome Qur-aan tukiwa na uchangamfu na ukihisi machofu au kama umechoka basi usiisome kwani hutokuwa unaisoma, na kama mpaka ikapelekea kufikia kusinzia wachilia mbali kulala mpaka ukaota basi ulikuwa huisomi Qur-aaan, ulikuwa unapoteza wakati au unapitisha wakati au unatafuta usingizi kwa matatizo yako ya kutopata usingizi, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘layhi wa aalihi wa sallam), hakupata kusoma Qur-aan mpaka akashikwa na usingizi au akaota, kwa hiyo sheikh huyu alikuwa hasomi Qur-aan alikuwa akitafuta usingizi. 

 

Then he dreamt the Prophet Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) standing in front of him

 

Tunataikiwa tuelewe kuwa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaonekanwa katika ndoto, lakini si kwa kila mtu hasa watu kama hawa wenye kutafuta usingizi kwa kuisoma Qur-aan, hawawezi kumuota al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam), wenye kujaaliwa kumuona Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa ‘aalihi wa sallam) ni wale wenye kushikamana na mafundisho yake na sio kusambaza na kueneza uwongo au uzushi au mambo kama haya yasiyo kuwa na asili katika Uislam.  Hivyo ndoto ya jisheikh letu ni ndoto ya ndaria na simulizi za watu wa kale na wenye kupenda kuonekanwa wanasikilizwa katika jamii. 

 

Ndoto huwa amri kwa Rusuli (‘Alayhimu-salaam) kama ilivyothibiti na kuja katika Qur-aan:

 

فَلَمَّا بَلَغَ مَعَهُ السَّعْيَ قَالَ يَا بُنَيَّ إِنِّي أَرَىٰ فِي الْمَنَامِ أَنِّي أَذْبَحُكَ فَانظُرْ مَاذَا تَرَىٰ ۚ قَالَ يَا أَبَتِ افْعَلْ مَا تُؤْمَرُ ۖ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ

 

اللَّـهُ مِنَ الصَّابِرِينَ ﴿١٠٢﴾ فَلَمَّا أَسْلَمَا وَتَلَّهُ لِلْجَبِينِ ﴿١٠٣﴾ وَنَادَيْنَاهُ أَن يَا إِبْرَاهِيمُ ﴿١٠٤﴾ قَدْ صَدَّقْتَ الرُّؤْيَا ۚإِنَّا كَذَٰلِكَ

 

نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ﴿١٠٥﴾ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْبَلَاءُ الْمُبِينُ ﴿١٠٦﴾ وَفَدَيْنَاهُ بِذِبْحٍ عَظِيمٍ ﴿١٠٧﴾ وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي

 

الْآخِرِينَ ﴿١٠٨﴾ سَلَامٌ عَلَىٰ إِبْرَاهِيمَ ﴿١٠٩﴾ كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿١١٠﴾ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ

Alipofikia makamo ya kwenda na kurudi pamoja naye; akasema: Ee mwanangu! Hakika mimi nimeona ndoto usingizini kwamba mimi nakunchinja, basi tazama unaonaje? (Ismaa’iyl) Akasema: Ee baba yangu! Fanya yale uliyoamrishwa, utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa wanaosubiriBasi wote wawili walipojisalimisha, na akamlaza kifudifudi juu ya kipaji. Na tukamwita: Ee Ibraahiym. Kwa yakini umesadikisha ndoto. Hakika Sisi hivyo ndivyo Tunavyolipa wafanyao ihsaan. Hakika hili bila shaka ni jaribio bayana. Na Tukamtolea fidia kwa dhabihu adhimu. Na Tukamuachia (sifa nzuri) kwa karne za baadaye. Salaamun! Amani iwe juu ya Ibraahiym. Hakika hivyo ndivyo Tunavyolipa wafanyao ihsaan. Hakika yeye ni miongoni mwa waja Wetu Waumini. [Asw-Swaaffaat: 102-111]

 

Pia Qur-aan inasema: 

 

لَّقَدْ صَدَقَ اللَّـهُ رَسُولَهُ الرُّؤْيَا بِالْحَقِّ ۖ لَتَدْخُلُنَّ الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ إِن شَاءَ اللَّـهُ آمِنِينَ مُحَلِّقِينَ رُءُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ لَا

 

تَخَافُونَ ۖ فَعَلِمَ مَا لَمْ تَعْلَمُوا فَجَعَلَ مِن دُونِ ذَٰلِكَ فَتْحًا قَرِيبًا

Kwa yakini Allaah Amemsadikisha Rasuli Wake ndoto kwa haki. Bila shaka mtaingia Al-Masjidal-Haraam In Shaa Allaah mkiwa katika amani, wenye kunyoa vichwa vyenu na wenye kupunguza, hamtakuwa na hofu.  Ameyajua ambayo hamkuyajua, Akajaalia kabla ya hayo ushindi wa karibu. [Al-Fat-h: 27]

 

Na si kila mwenye kuota ana uwezo wa kuaguwa ndoto yake na pia si kila mtu ana ujuzi huo, ndio Qur-aan ikatupa habari za ndoto na waaguzi wake huwa watu wa namna gani? Qur-aan inasema:

 

 وَدَخَلَ مَعَهُ السِّجْنَ فَتَيَانِ ۖ قَالَ أَحَدُهُمَا إِنِّي أَرَانِي أَعْصِرُ خَمْرًا ۖ وَقَالَ الْآخَرُ إِنِّي أَرَانِي أَحْ  مِلُ فَوْقَ رَأْسِي خُبْزًا تَأْكُلُ الطَّيْرُ

 

مِنْهُ ۖ نَبِّئْنَا بِتَأْوِيلِهِ ۖ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ﴿٣٦﴾ قَالَ لَا يَأْتِيكُمَا طَعَامٌ تُرْزَقَانِهِ إِلَّا نَبَّأْتُكُمَا بِتَأْوِيلِهِ قَبْلَ أَن يَأْتِيَكُمَا ۚ ذَٰلِكُمَا مِمَّا

 

عَلَّمَنِي رَبِّي ۚ إِنِّي تَرَكْتُ مِلَّةَ قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ

Wakaingia pamoja naye jela vijana wawili.  Mmoja wao akasema: Hakika mimi najiona ndotoni kuwa nakamua mvinyo. Na mwengine akasema: Hakika mimi najiona ndotoni nabeba juu ya kichwa changu mikate wanaila ndege humo. Tujulishe tafsiri yake, hakika sisi tunakuona ni miongoni mwa wafanyao ihsaan. (Yuwsuf) Akasema: Hakitokufikieni chakula chochote mtakachoruzukiwa isipokuwa nitakujulisheni tafsiri yake kabla hakijakufikieni. Haya ni katika Aliyonifunza Rabb wangu. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasiomwamini Allaah na wao ni wenye kuikanusha Aakhirah. [Yuwsuf: 36-37]  

 

Kila mtu huota lakini muaguzi wa ndoto ni lazima awe mtu mwenye sifa maalumu, awe mtu mwenye kushikamana na mafundisho aliyokuja nayo al-Habiyb Muhammad (Swalla Llaahu ‘Alayhi Wa ‘Alaa Aalihi Wa Sallam) ili aweze kufikishwa kwa tawfiki yake Rabb kuweza kuaguwa ndoto za waotaji, na sio biashara ya kujipatia fedha au umaarufu, ama aliye mbali na mafundisho kama mwenye kutafuta usingizi na njia aliyoiona ni kusoma akaamua kuisoma Qur-aan ili apate kulala huyo ndoto yake haina athari wala umuhimu wo wote ule katika Uislam na waislamu pia. 

 

The Prophet Said Whoever Reads This News To Someone Else, 'i Will On The Day Of Judgement Make Him A Place In Paradise, And If Someone Does Not Believe This News To Be True They Will Be Banished From Paradise!'if A Poor Person Gives Out This News To Other People His/her Good Wish Will Come True. 

 

Huku hasa ndiko kumzulia uongo al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa makusudi, na mwenye kumzulia uongo kama huyu anajipalilia na kujitengezea pahala pake Motoni sio kwengineko.  Wapi kumepokea habari hii katika vita vyote vya Hadiyth, wapi kumepatikanwa simulizi hii katika vitabu vyema kushikamana na mafundisho ya al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 

 

' I Will On The Day Of Judgement Make Him A Place In Paradise........

 

The Prophet Said 'keep Fast, Do Prayers, Give Zakaat And Give Kindness To The Poor' 

 

Al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haelewi nini atafanywa yeye! vipi atakuwa na uwezo wa kumpa mtu Jannah, yeye al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameletwa awe Muonyaji na Mtoa habari njema na sio kuwatengea watu sehemu katika Jannah, Jannah ni ya Allaah na Humtunuku Amtakae na wa mwanzo katika hao ni yule aliyeshikamana na mafundisho aliyokuja nayo al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu  ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na sio anayemzulia uongo na kutaka uongo huo utanganzwe na usambazwe kwa wenye kumpenda na kumfuata al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 

 And

 

If Someone Does Not Believe This News To Be True They Will Be Banished From Paradise! 

 

Habari hii ni uongo tena anayezuliwa uongo huu ni yule aliyeletwa watu wamfuate na sio vyengine, msambazaji anataka watu waamini, habari ambayo ni uongo na mwenye kukataa kuiamini basi hatopata Jannah.  Uhakika na ukweli ni kuwa huu ni uongo, na baada ya kuelewa kuwa ni uzushi na uongo anaozuliwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi mwenye kuueneza huenda akawa anajitengenezea pahala Motoni na mwenye kushikamana nao huenda akakosa hiyo Jannah yenyewe, hivyo kuamini yasiyothibiti katika Uislamu na unayoelewa kuwa ni uongo ni kujikosesha Jannah.

 

'If a poor person gives out this news to other people his/her good wish Will come true.  

 

Maskini amekosa nini hata awe ndiye msambazaji wa habari za uongo, masikini wengi ndio wakaazi wa Jannah na ndio wengi wasiokuwa hata na internet na e mail zenye kupelekea mtu kueneza uongo na uzushi kama huu. Tajiri hana haja ya kueneza uongo kwani yeye kwa mtazamo wa jisheikh letu ni kuwa anachokisema huwa ni kweli ndio akawa hana haja ya wish zake kuwa kweli kwani yeye anacho kila akitakacho, na maskini anahitaji awe na kitu na ni mwenye kuota na kutamani, hivyo akitaka apate anayoyatamani asambaze uongo na uzushi kwa lengo la kuwaharibia na kujiharibia yeye mwenyewe fursa yake ya kuingia Jannah.  Ukitaka wish zako ziwe true basi kuwa mcha wa Allaah, Qur aaan inasema:

 

وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يَجْعَل لَّهُ مَخْرَجًا﴿٢﴾ وَيَرْزُقْهُ مِنْ حَيْثُ لَا يَحْتَسِبُ ۚ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَهُوَ حَسْبُهُ

Na yeyote anayemcha Allaah; Atamjaalia njia ya kutoka (shidani). Na Atamruzuku kutoka njia ambayo hatizamii. Na yeyote anayetawakali kwa Allaah, basi Yeye Humtosheleza. [Atw-Twalaaq: 2-3]

 

 Pia Quraan Tukufu inasema:

ذَٰلِكَ أَمْرُ اللَّـهِ أَنزَلَهُ إِلَيْكُمْ ۚ وَمَن يَتَّقِ اللَّـهَ يُكَفِّرْ عَنْهُ سَيِّئَاتِهِ وَيُعْظِمْ لَهُ أَجْرًا

Hiyo ni amri ya Allaah Amekuteremshieni; na yeyote anayemcha Allaah, Atamfutia maovu yake na Atamuadhimishia ujira. [Atw-Twalaaq: 5]

 

Na mwisho inasema kuwa kama wewe kweli unataka wish zako ziwe true na ufanikiwe katika mambo yako yote, na kuwa wish kubwa anayotamani aipate Muislam ni Jannah, basi huna haja ya kuzua uongo wala kumzulia al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali kuwa hivi:

 

رَّسُولًا يَتْلُو عَلَيْكُمْ آيَاتِ اللَّـهِ مُبَيِّنَاتٍ لِّيُخْرِجَ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ ۚ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ وَيَعْمَلْ

 

صَالِحًا يُدْخِلْهُ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۖ قَدْ أَحْسَنَ اللَّـهُ لَهُ رِزْقًا

Ni Rasuli anakusomeeni Aayaat za Allaah zinazobainisha; ili kuwatoa wale walioamini na wakatenda mema kutoka kwenye viza kuingia katika Nuru. Na yeyote anayemwamini Allaah na akatenda mema, Atamuingiza Jannaat zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo abadi. Allaah Amekwishamfanyia rizki nzuri kabisa. [At-Twalaaq: 11]

 

Kupata Jannah ambayo inatafutwa na wenye hamu nayo katika mwezi huu wa Ramadhaan na hasa hasa katika siku kumi hizi za mwisho ndio wish kubwa kwa wenye akili, iman na kumtarajia Allaah na Siku ya Qiyaamah na wengi wao ni maskini Basi je! Nyinyi ni Waislamu?"  

 

Sheikh Ahmed said if this is not true then my death will Be off a Non-Muslim.  

 

Bila ya shaka wala wasi wasi wo wote ule hii habari sio kweli, haijathibiti kutoka kwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata kama kuna mambo ndani yake yenye kusisitizwa na Uislam, lakini habari hii ni uongo unaozuliwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na kwanini tutumie uongo na tuzuwe katika kuwapendelezea watu mambo ambayo yamethibiti katika Hadiyth tena kwa matamshi mazuri yenye nuru na mwangaza.

 

my death will Be off a Non-Muslim Person

 

Muislam hatakiwi aombe, ajiombe wala awaombee wenzake kuwa wafe hali ya kuwa sio Muislam, ukiwa rafiki/shoga wa Qur-aan utaona nini ushauri wake katika kutafuta ukiwa uwe nani, Qur-aan inasema: 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ حَقَّ تُقَاتِهِ وَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

Enyi walioamini! Mcheni Allaah kama ipasavyo kumcha na wala msife isipokuwa nyinyi (mmeshakuwa) ni Waislamu. [Al-'Imraan: 102]

 

Pia unatutaka katika mambo ya kuusia watoto wetu tuige watu wema na waja wema, sio tuusie mali tu na mambo ya kimaajabu bali tuwausie kuwa wafanye wafanyavyo lakini wahakikishe kuwa wanakufa hali ya kuwa ni Waislamu, na huu ndio wasii wa Rusuli kwa dhurriya wao, Qur-aan inasema:

 

وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٣٢﴾ أَمْ كُنتُمْ شُهَدَاءَ إِذْ

 

حَضَرَ يَعْقُوبَ الْمَوْتُ إِذْ قَالَ لِبَنِيهِ مَا تَعْبُدُونَ مِن بَعْدِي قَالُوا نَعْبُدُ إِلَـٰهَكَ وَإِلَـٰهَ آبَائِكَ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ إِلَـٰهًا وَاحِدًا

 

وَنَحْنُ لَهُ مُسْلِمُونَ

Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na (kadhalika) Ya’quwb (akawaambia): Enyi wanangu! Hakika Allaah Amekukhitarini nyinyi Dini; basi msife isipokuwa nyinyi ni Waislamu. Je, mlikuwa mashahidi wakati mauti yalipomfikia Ya’quwb alipowaambia wanawe: Mtaabudu nini baada yangu? Wakasema: Tutamwabudu Ilaaha wako (Allaah) na Ilaaha wa baba zako, Ibraahiym na Ismaa’iyl na Is-haaq; Ilaah Mmoja, nasi ni Waislamu (tunajisalimisha) Kwake. [Al-Baqarah: 132 -133]

 

Vipi utajiombea ufe kinyume na ushauri wa Qur-aan, na hata kama ikiwa habari ni ya kweli kama inavyodaiwa kuwa jisheikh letu la vitabuni alivyodai, basi hakuna haja ya kujiombea kufa hivyo, cha kufanya ni kumuomba Allaah Akuwafikishe kufuata yaliyothibiti na kuachana na uongo na uzushi tena uongo na uzushi unaozuliwa al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Forward it to 40 people he had 8,000 thousand, take prophet in his Business.

 

Mwenye kutaka faida na kumea biashara yake basi ushauri wa Qur-aan ni huu:

 

مَّثَلُ الَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنبَتَتْ سَبْعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنبُلَةٍ مِّائَةُ حَبَّةٍ ۗ وَاللَّـهُ يُضَاعِفُ لِمَن يَشَاءُ ۗ وَاللَّـهُ

 

وَاسِعٌ عَلِيمٌ

Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika njia ya Allaah ni kama mfano wa punje moja ya mbegu iliyotoa mashuke saba, katika kila shuke kuna punje mia. Na Allaah Humzidishia Amtakaye; na Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote. [Al-Baqarah: 261]

 

Pia Qur-aan inasema:

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ تِجَارَةٍ تُنجِيكُم مِّنْ عَذَابٍ أَلِيمٍ﴿١٠﴾ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتُجَاهِدُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِكُمْ

 

وَأَنفُسِكُمْ ۚ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿١١﴾ يَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ وَيُدْخِلْكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً

 

فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٢﴾ وَأُخْرَىٰ تُحِبُّونَهَا ۖ نَصْرٌ مِّنَ اللَّـهِ وَفَتْحٌ قَرِيبٌ ۗ وَبَشِّرِ الْمُؤْمِنِينَ

Enyi walioamini! Nikujulisheni biashara itakayokuokoeni na adhabu iumizayo? Mumuamini Allaah na Rasuli Wake, na mfanye jihaad katika njia ya Allaah kwa mali zenu, na nafsi zenu. Hivyo ndiyo bora kwenu mkiwa mnajua. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua. (Allaah) Atakughufurieni madhambi yenu, na Atakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito na masikani mazuri katika Jannaat za kudumu milele. Na jengine mlipendalo; nusura kutoka kwa Allaah na ushindi wa karibu. Na wabashirie Waumini. [Asw-Swaff: 10-13]

 

Whoever Forwards this will get his/her reward in three days.

 

Kuna Hadiyth nyingi kupita wingi wa habari wanazozisambaza wanomzulia al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zenye kuonyesha kuwa ukitenda jambo utalipwa hivi na hivi au utapata hivi na hivi au utakuwa hivi na hivi na sio utapata malipo yako katika kipndi cha siku tatu!  Waislamu wanapotekeleza jambo huwa na Iymaan na matarajio ya kutunukiwa Alichonacho Rabb na hicho sio baada ya siku tatu Allaahumma iwe shahada katika Jihaad ambayo yawezekana ikawa hata baada ya dakika tatu wachilia mbali siku tatu ama mengineyo ambayo Waislamu hujipendekeza kwa Rabb ni kwa ajili yake Rabb na ad-Daarul Aakhirah na sio vyengine. Hivyo malipo ya hapa dunia sio lengo kwa amali yoyote ile ya Muislam.

 

One Person did not believe this news and his son died. One kept Saying he will forward it today, tomorrow but never forward this News he died as well.  

 

Haya matamshi pekee yanathibisha na kubainisha kuwa muandishi au msambazaji hana 'Aqiydah /itikadi ya Kiislamu, sasa vipi mwenye 'Aqiydah sahihi asambaze jambo lenye kwenda kinyume na Dini yake na mafundisho ya al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)! Mwenye kuamini au kuitakidi kuwa kifo chake au cha mtoto wake kimetokea kwa sababu fulani na sio kuwa Allaah Ndiye Mwenye kufisha na kuhuisha basi Uislam wake una matatizo, na mwenye kuamini kuwa kama akifanya au kutofanya jambo fulani (kutosambaza uzushi na uongo kama huu) atapatwa na madhara ikiwemo kifo huyo si katika wenye kushikama na kufuata mafunzo na itikadi sahihi aliyokuja nayo al-Habiyb Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kitachokupata kimeshaandikwa kuwa kikupate na kisichokusibu hakiwezi kukusibu hata kama Majini na watu wote watashirikiana. Wino ushakauka na kalamu ishanyayuliwa. Hivyo ukifa ndio siku yako ishafika na sio jengine na akifa wako hali kadhalika.

 

Ndugu katika Iymaan, tuwe na tahadhari sana na kuanzia leo tuwekeni dhamira ya kupigana vita na e mails za namna hiyo zenye kumzulia Nabiy wetu mpenzi na zenye kuwapotezea Waislam wakati wao mkubwa. Tuhakikishe tunaacha kueneza mambo yasiyo na dalili wala ushahidi katika Dini, na pindi tunapopata e mails kama hizo, tujibu haraka na kuwakanya wanaozituma na kuwanasihi In Shaa Allaah.

 

Tunamuomba Allaah Awahifadhi katika ‘Aqiydah sahihi na kuwatakabalia ‘amali zenu. Aamiyn

Share