Baba Ametukataza Tusiwasiliane Na Dada Yetu – Je Tumtii?

 

 

SWALI:

 

Mimi nina dadangu ambaye anaishi na mwanaume bila kuolewa na mbaya zaidi akapata ujauzito. Na wakati wote anakaa na mwanaume babangu hakuwa anajua hilo alikuwa anajua kuwa anaishi peke yake kwani ndiyo ilikuwa ahadi kuwa angeishi kwa misingi ya dini.

Sasa babangu alivyosikia kuwa ni mjazito alitoa maneno makali sana juu ya dadangu na kumtaka kama anataka msamaha arudi nyumbani na kadi la kliniki lifutwe jina la huyo mwanaume. Licha ya upenyo huo dada yangu akakataa kurudi nyumbani hivyo mpaka sasa amejifungua bado anakaa na huyo mwanaume wake ambaye ni mgalatia.

Sasa basi babangu amesema mtu yeyote atakayempa msaada dadangu iwe kwenda kumuona au kumpelekea zawadi   yeye hayuko pamoja naye. Hivyo mpaka sasa mimi sijaenda kumuona dada yangu huyo. Je kisheria babangu yuko sawa

 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu muulizaji swali. Hakika ukweli wa mambo ni ule msingi ambao ametuekea sisi kipenzi Mtume wetu, Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema: " Hakuna utiifu kwa kiumbe ikiwa itakwenda katika kumuasi Muumba". Lakini ikiwa mwenye kutoa amri ni katika wale walioelezwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi kutiiwa inakuwa ni lazima.

Miongoni mwa wale ambao tunafaa tuwatii ni wazazi wawili wakiamrisha jambo linalokwenda sambamba na sheria. Mas-ala ya kupigwa vita na kususiwa watu wa maasi ni jambo ambalo limehimizwa na sheria. Katika hilo ndio tunaona kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliamrisha Maswahaba watatu waliokosa kwenda katika Vita vya Taabuuk kupigwa vita na kusususiwa hata katika salamu. Maswahaba wenyewe walikuwa ni Ka'b bin Maalik, Muraarah bin ar-Rabii' al-'Amriy na Hilaal bin Umayyah al-Waaqifiy (Radhiya Allaahu 'anhum). Hawa watatu walianza kusemeshwa tu baada ya kupatiwa msamaha na Allaah Aliyetukuka (al-Bukhaariy na Muslim, waweza kuipata Hadiyth hiyo kwa urefu katika kitabu Riyaadh asw-Swaalihiyn, Hadiyth namba 21).

Ama Qur-aan imetuelezea yafuatayo kuhusu twaa kwa wazazi: "Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii, lakini kaa nao kwa wema duniani" (31: 15).

 

Kwa mujibu wa swali lako, fuata na tekeleza yafuatayo:

1.     Kwanza wasiliana na dada yako ukiweza na lengo lako la kufanya hivyo ni kumpatia nasaha kwamba maisha anayoishi hayo sio sawa, na dini yetu hairuhusu hivyo bali ni haraam.

 

2.     Jaribu kwa kila njia kumpatia makala, mawaidha atambue uharamu wa maisha anayoishi na matokeo yake kupata ghadhabu za Mola wake.

 

3.     Mjulishe kuwa unawasiliana naye kwa kuvunja amri ya mzazi wenu, na sababu ni kwamba unamtakia kheri ya maisha yake ya kidunia na Akhera. Kwani pindi atakapokatana na wazazi wake na ndugu zake ni hatari kubwa mno na jambo la kulaaniwa na Mola na pia ataharamishwa na Pepo. Mchapishie Swali katika kiungo kifuatacho:

 

Amezuiliwa Kuonana Na Mama Yake Afanyeje?

4.     Mtahadhirishe kuwa hayo ni maisha ya dunia ambayo yatakwisha – na pindi watakapoondoka mmoja wa mzazi wenu akiwa ameghadhibika naye basi atambue kuwa amekosa Pepo bali atapata ghadhabu za Mola wake na hatokuwa na kheri na Baraka katika maisha yake kwa kukosa radhi za wazazi wake, bali huenda akadhurika! Hivyo faida gani atakayopata au atafaidika vipi na huyo mume na watoto wake?

 

5.     Aachane na huyo mwanaume mara moja, na ikiwa huyo mwanaume anataka kuendelea kuishi naye, basi amjulishe kuwa anatakiwa kusilimu kwanza kwa khiyari yake na si kuitikia tu ili apate kukaa naye kama wanavyofanya wengi wenye kufuata mapenzi na si Dini! Mwambie afanye toba kwa yote hayo na Allaah Atamsamehe inshaAllaah na Kumpa bora kuliko huyo mwanaume aliyenaye hivi sasa.

 

6.      Atakapokupa jibu la kuwa na matumaini ya kukubali nasaha basi endelea kuwasiliana naye. Lakini pindi utakapoona kuwa kashikilia kuishi hivyo hivyo bila ya kutaka kujaribu kusawazisha maisha yake basi hapo ndipo itakapokubidi umjulishe kuwa hutoweza kuendelea kuwasiliana naye na kwamba itabidi ukate mawasiliano naye

 

Tunakuombea kila la kheri katika jitihada yako na nia yako njema ya kutaka kumuokoa dada yako kwenye haraam na madhara ya maisha yake.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share