Mume Ananitaka Tena Baada Ya Talaka Tatu

SWALI:

 

Natoa shukurani nyingi kwenu nimesikia sifa nyingi nzuri. Ningependa nipate maoni kwa wote ulamaa

kama isemekanavyo FAS’AL AHLADH DHIKR INKUNTUM LA TAALAMUN. nina watoto 6 na nishawachana na baba yao mara tatu nikaolewa akaoa mimi naishi na watoto sikupendezwa na mume nikajiachisha baba watoto akarudi akasema lakini iwe siri nikakubali maana ni baba yao el asaf mkeo akajua akaniwacha tena juzi akaja tena nirudi jee NIRUDI?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu kwa dada muulizaji swali kuhusu mahusiano yako na mumeo. Mwanzo wa yote ni kwamba yapo mambo mengine katika swali lako ambayo hayaeleweki vilivyo. Umetuambia kuwa ulirudiana na mumeo kwa siri, sasa hii ni siri ipi? Hakika ni kuwa katika Uislamu hakuna ndoa ya siri. Ndoa ya Kiislamu kusihi ni lazima kupatikane mashahidi wawili waadilifu pamoja na masharti mengine kutimia. Ikiwa mlichukuana tu mkaoana bila hayo masharti hakutakuwa na ndoa. Ama Ikiwa kwa neno siri unamaanisha kuwa mliifanya kwa kufuata taratibu za ndoa kikamilifu, lakini tu hamkutaka watu wengine wajue hasa watu wa mke mwenza na mke mwenyewe basi ndoa yenyewe itakuwa sahihi.

Ama kutaka ushauri kwetu ni kuwa ni lazima utahadhari na pengine kumwekea mtalaka wako masharti yatakayokuweka katika unyumba. Katika maelezo yako naona kama ndoa hiyo hata ukiikubali haitakuwa ni yenye kudumu kwa sababu mume anamuogopa mkewe. Huenda kuwa mke huyo akijua mahusiano yenu kwa mara nyingine atamuamuru huyo mume akuache, na bila shaka mume atatekeleza hayo kama alivyofanya mara iliyopita. Sasa jiulize mwenyewe utakubali kuwa katika hali ya wasiwasi kuwa nitaachwa leo au kesho. Ushauri ambao tunaweza kukupa ni uswali Swalah ya Istikhaarah umtake ushauri Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) ikiwa ni kheri Akusahilishie na ikiwa ni shari basi Akuepushie.

Tunakutakia na kukuombea kila la kheri katika suala hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share