Kuadhini Na Kukimu Kwa Mwanamke
Kuadhini Na Kukimu Kwa Mwanamke
SWALI:
Je inajuzu kwa mwanamke kuadhini na kukimu wakati wa kusali sala za fardhi au jambo hili ni kwa wanaume tu?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza ni vyema tufahamu lengo la Adhana ni kutoa taarifa ya kuingia kwa wakati wa Swalaah na lengo la Iqaamah ni kujulishwa kuanza kwa Swalaah.
Pili: Kila jambo ambalo ameamrishwa mwanamme katika Shariy’ah basi na mwanamke naye pia ameamrishwa kama ilivyo haramu ikiharamishwa kwa mwanamme basi ni pia kwa mwanamke isipokuwa kama kutakuwa na dalili iliyo wazi katika Qur-aan au Sunnah inayoelezea kinyume cha hayo.
Hivyo katika ufafanuzi wa kina katika suala hili tutaangalia kauli tofauti za ‘Ulamaa kama ifuatavyo.
-Ibn Hazm:
"Si lazima kwa mwenye kuswali peke yake kuadhini au kukimu lakini kama ataadhini na kukimu basi ni vizuri." [Al-Muhallaa 1/167]
-Ibn Qudaamah:
“Wala sijawahi kusikia mtu anaesema kinyume cha hayo.” (yaani si lazima) [Al- Mughniy 1/438]
-Ahmad bin Hanbal:
“Wakifanya hakuna kosa na wasipofanya pia inajuzu.”
Kwa upande wa madhehebu ya ki-Shaafi’iy wanasema: Kukimu kunapendeza kwa wanawake lakini si kuadhini.
-Fataawaa Al-Lajnatul Fataawah Daaimah 6/84:
"Mwanamke hajaamrishwa kuadhini au kukimu kwenye Swalaah ikiwa ataswali peke yake au hata wakiswali jama’ah."
-Imaam Ibn Baaz:
katika Majmu’ Fataawa wa Maqalaat Mutannawwi’ah 10/356, aliwahi kuulizwa suala hili na alisema:
"Wanawake hawajaamrishwa kuadhini au kukimu, jambo hili ni la wanaume hivyo ni bora waswali bila ya Adhana wala Iqaamah."
-Imaam Ibn ‘Uthaymiyn:
"Wakifanya hivyo hakuna ubaya na wasipofanya pia hakuna ubaya kwa sababu kuadhini na kukimu kumewajibishwa wanaume tu."
-Imaam Al-Albaaniy:
Amesema katika Al-Haawiy min Fataawaa ash-Shaykh al-Albaaniy/ 184:
"Hakuna tofauti katika hukumu za ki Shariy’ah katika Swalaah, Swawm wudhuu, Hijjah na kadhalika. Hivyo yale yote yaliyowajibishwa kwa mwanamme basi yamewajibishwa kwa mwanamke mpaka kupatikane dalili ya kinyume cha hivyo. Kwa kutumia msingi huu hukumu ya Adhana na Iqaamah itabaki kuwa wajibu kwa wote mpaka kuthibitike vyenginevyo."
Ulamaa katika kufanya utafiti wa kina wanasema katika suala hili lipo jambo linalolifanya hukmu hii isiwe wajibu kwa mwanamke. Kuadhini huwa kwa sauti kubwa na wanawake hawatakiwi kunyanyua sauti zao na pia Kuna Hadiyth iliyopokelewa na Asmaa bint Yaziyd inayosema:
ليس على النساء أذان ولا إقامة
“Wanawake hawana Adhana wala Iqaamah” [Al Mughniy 1/438]
Na kuna Riwaayah iliyosimuliwa na Al-Bayhaqiy inayosema hivyo hivyo kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa).
Tuziangalie hali zitazomkuta mwanamke:
|
Hali |
Hukmu |
1 |
Kuadhini na kukimu kwenye kundi la wanaume pekee |
Haijuzu |
2 |
Kuadhini na kukimu kwenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake
|
Haijuzu |
3 |
Kuadhini na kukimu kwenye kundi la wanawake tu |
Hakuna ubaya |
4 |
Kuadhini na kukimu akiswali peke yake |
Hakuna ubaya |
5 |
Kukimu tu bila ya kuadhini kwenye kundi la wanawake tu |
Mustahab (inapendeza) |
6 |
Kukimu tu bila ya kuadhini akisali peke yake |
Mustahab (inapendeza) |
Hata hivyo wanawake watakapoadhini watatakiwa waadhini kwa sauti itakayotosha kusikilikana kwa wale waliopo miongoni mwa wanawake tu.
Pia Swaalah yao itakuwa sahihi hata kama hapajaadhiniwa au kukimiwa kwa kufuata kauli za Maulamaa wengi kwamba jambo hili halijawajibika kwa mwanamke.
Na kama mume na mke wataswali jama’ah nyumbani, mwenye haki ya kuadhini na kukimu ni mume kwa sababu kwake hili jambo amewajibishwa na mwanamke hakuwajibishwa.
Na Allaah Anajua zaidi