Jinsi Ya Kuondosha Najisi Ya Mbwa Kwenye Nguo
Jinsi Ya Kuondosha Najisi Ya Mbwa Kwenye Nguo
SWALI:
Swali langu ni kwamba, Je hii najis inaondoshwa vipi ya mbwa? na je akininusa juu ya nguo sio kwenye ngozi inabidi nikoshe zile nguo tu au na mimi mwenyewe nijikoshe? na je inanuiwa vipi wakati wa kujikosha na kuiondosha hii najsi ya mbwa?
Natumai swali langu litawanufaisha waislamu wenzangu wengi hasa wanaoishi nchi za nje. Naomba tafadhalini munijibu haraka iwezekananyo kwani nategemea kuanza kazi pahala ambapo pana mbwa karibuni in shaa Allaah.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kuhusu najisi inayopatikana kwa kunuswa na mbwa basi maelezo ni kama yafuatayo.
Pahali paliponajisiwa kwa kurambwa na mbwa au kunuswa kama chombo na kadhalika mfano huo. Ili kitu hicho kutwaharika na kusafishika na kurudi katika hali yake ya kawaida na usafi kinatakiwa kioshwe mara saba mojawapo kwa mchanga. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Anaporamba mbwa kwenye chombo cha mmoja wenu, basi akioshe mara saba, mojawapo kwa mchanga" [Muslim, Ahmad na Abu Daawuwd].
Ikiwa amenusa kwenye nguo utaiosha nguo tu kwa mchanga na maji ikiwa hakuna taklifa, la sivyo unaweza kutumia sabuni na maji hususan ikiwa utafua nguo hiyo kwa mashine ya kufulia nguo, na akiwa amenusa ngozi yako basi utaiosha hiyo sehemu ya ngozi kwa maji na mchanga mara saba. Pia unaweza kutumia sabuni pamoja na maji.
Niyyah ya kila kitu iko moyoni, hivyo ukishanuia moyoni mwako kuondosha najisi inatosheleza kabisa, huna haja kutamka wala kusema maelezo au kuyahifadhi.
Bonyeza viungo vifuatavyo kupata faida zaidi:
Hukmu Ya Manyoa Ya Mbwa Anayefugwa Nyumbani
Jinsi Ya Kuondosha Najisi Ya Mbwa Kwenye Nguo
Na Allaah Anajua zaidi