Mas-ala Ya Alcohol Katika Chakula Na Nguo Na Hukmu Zake

 

SWALI:

Assalam aleikum warahamatullah,

Alhamdulillah, wasalatu wa salamu ala rasulillah.

Suala langu la khusu hukumu ya utumiaji "alcohol". Utumiaji hapa sikusudii kunywa. Kunywa ulevi twajua sote ni haram. Suala langu linaingia katika vyakula, madawa, marashi (perfumes), sabuni, n.k.

Mwanzo ningependa kueleza kidogo kuhusu "alcohol" ki-kemia (chemistry). Alcohol kwa jumla ni aina moja ya "organic compounds" ambazo asli yake hutokana na mafuta (petroleum refinery products). Alcohol ziko aina nyingi sana kuanzia zilo nyepesi kama vile "methanol", "ethanol"...halafu kuna zile ambazo ni za juu (higher alcohols kama "isopropanol, glycerols) na za juu zaidi (complex alcohols kama cortisol). Hizi aina tofauti zina "properties" tofauti na matumizi tofauti.

Ulevi (pombe za aina yote, mvinyo n.k) vyote huwa vina alcohol aina ya Ethanol. Alcohol aina nyeninge kama methanol ni sumu. Alcohol aina nyengine hutumiwa kama kwenye madawa kama viyayushaji (solvents) vya ule mchangyiko wa chemikali unaofanya dawa.

Ethanol ndio inayokuwa ndani ya ulevi kwa uafahamu wangu ndio inayosababisha mtu kuwa katika hali ya kulewa. Madaktari huweza kusema kiasi cha alcohol mwilini (blood alcohol level) kwa kupima ethanol iliyo kwenye damu. Na hichi ndicho kipimo wanachotumia polisi kushtaki watu wanaokamatwa wakiendesha magari na huku wamelewa.

Ethanol ina changanyika na maji sawa kwa sawa (100% soluble) na inachemka kwa joto la kiasi 78 degrees.

Masuala-

1. Nini hukumu ya chakula ambacho kimetiwa kwa mfano mvinyo? Kuna aina za keki, aina ya michuzi inayotiwa mvinyo, halafu vikapikwa kwa moto wenye joto kama 250 kwa kweki na zaidi ya hapo kwa vyakula. Kwa moto huu, ethanol yote itakuwa imetoweka (evaporated) na chakula hakitkuwa tena na ulevi. Chakula hiki ni vipi?

2. Matumizi mwenigne ya ethanol ni methylated spirit ma-hospitalini. Ulevi ni najis. Kutumiwa methylated spirit (~99% ethanol) kwa kusafisha sehemu ya mwili (disinfection) yakubalika? Mtume s.a.w amesema "anaetumia ulevi kama dawa, basi amelaanika na maradhi yake yasipowe" (Allahu a'alam).

Jee deodorants ambazo zina alcohol aina nyeninge ambayo sio ethanol, kutumiwa yaruhusiwa? 

3. Nguo zetu zikiingiwa na ethanol ambayo hukauka papo hapo twaweza kusalia?

Natumia masuala haya  yamefahamika na hayataleta utata kwa wasomaji wenginge. Na Inshallah mw. Mungu awape hikma katika kujibu masuala yote munayotumiwa.

Wabillahi taufiq.



JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri kuhusu alcohol ambayo kwa kiasi kikubwa kama tunavyofahamu ni pombe. Pia tunashukuru wka uchambuzi wako mzuri na pia kwa kuanza na kumhimidi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na ingekuwa vizuri zaidi pia kama ungerefusha kumswalia Mtume badala ya kutosheka na kuandika s.a.w halikadhalika ungempa heshima zaidi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa kuandika jina Lake kikamilifu badala ya kufupisha kwa kuandika mw. Mungu.

Hata hivyo kabla ya kuingia katika maswali yako tungependa kusema yafutayo:

  1. Mwanzo ile ibara uliyotumia kuwa asli ya alcohol ni mafuta (petroleum refinery products) ni sawa ingawa si njia pekee. Tunafahamu kuwa petrol haitoi alcohol bali alcohol kwa leo ipo ile yenye kutengenezwa viwandani kwa kutumia vifaa na vitu ambavyo vina carbohydrates. Kienyeji pia njia ni kama hiyo kwani majumbani huwa inatengenezwa ima kwa kutumia matunda kama zabibu, tende na kadhalika. Pia hufanywa kwa kutumia nafaka kama mahindi, ngano na kadhalika. Hata tembo hilo hugemwa kutoka kwenye miti kama mnazi, mkoma na kadhalika.

  2. Pia ibara ifuatayo: “halafu kuna zile ambazo ni za juu (higher alcohols kama isopropanol, glycerols) na za juu zaidi (complex alcohols kama cortisol)” si sahihi moja kwa moja kwani glycerol ni nyepesi sana nayo ni triol yenye formula C3H8O3.

Pia tufahamu kuwa neno khamr lililotumiwa katika Qur-aan limefasiriwa na ‘Umar bin al-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa juu ya minbari kuwa ni kitu chochote chenye kuharibu akili (al-Bukhaariy na Muslim). Na wafasiri wengine wamelifasiri neno hilo kumaanisha ulevi au kileo.

Ni vyema pia tuelewe kuwa wanazuoni wametofautiana kuhusu unajisi au utwahara wa pombe. Wapo wanaosema kuwa ni najisi na wengine wakasema ni twahara. Hata hivyo, usahihi ni kuwa pombe ni twahara mbali ya kuwa ni haramu kunywa. Soma maelezo kwa urefu kuhusu suala hilo hapa kwenye kitabu cha Fiqh ‘Swahiyh Fiqhus-Sunnah’ ambacho tunaamini utanufaika nacho sana, ingia katika kiungo hiki:

Je, (pombe) Pombe Ni Katika Vitu Najisi?

Ama tukija katika maswali yako, majibu yake ni kama yafuatayo:

  1. Pombe imeharamishwa kabisa kutumiwa kwa kunywa au kutiwa katika chakula hata ikiwa hizo keki ambazo zinatiwa pombe ina-evaporate (vukiza/toweka) kwa sababu ya daraja ya uharara iliyo kubwa. Ikiwa ni hivyo kwa nini ulevi utumiwe katika kufanyia chakula hicho ikiwa haitakuwa tena? Kama kusema inatia ladha, je, ladha haipatikani ila kwa njia hiyo ya matumizi machafu ya haraam ambayo tunatia katika matumbo yetu? Allaah Aliyetukuka Anatuambia wazi kabisa: “Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa” (5: 90). Hivyo, kutumiwa kama kinywaji au kutiwa katika chakula ni jambo ambalo halifai kabisa katika Uislamu kwani imeharamishwa kutumiwa katika njia hizo. Msingi wa Uislamu ni kuwa: “Kila kileweshacho ni ulevi, na kila ulevi ni haramu” (Muslim). Na, “Kileweshacho wingi wake basi na uchache wake ni haramu pia” (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ahmad).

  1. Kama tulivyosema hapo juu kuwa pombe si najisi kwa kauli ambayo ndio yenye nguvu zaidi kwa dalili zilizopo. Hakika hatujaiona Hadiyth kama ulivyoandika bali Hadiyth inayofahamika ni ile yenye maana: “Allaah Hakufanya kupona kwenu kutokane na Aliyokuharamishieni” (al-Bukhaariy). Na tena: “Ulevi si dawa bali ni maradhi” (Ahmad, Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy). Pia, “Allaah ameleta maradhi na dawa, na Akajaalia kila ugonjwa una matibabu yake basi jitibuni, wala msijitibu kwa kitu cha haramu” (Abu Daawuud). Ama kutumiwa nje ya mwili katika mahospitali kwa kusafisha, Wanachuoni wote wamesema haina tatizo lolote katika fatwa zao kwa sababu haikutumiwa kama inavyotumika kwa njia ya mdomo inayojulikana. Ama deodorants (kiondoa harufu) ikiwa zitakuwa na alcohol hiyo nyingine, je, hiyo ina ulevi au la? Ikiwa haina ulevi hakuna tatizo lolote. Ama ikiwa ina ulevi Mwanachuoni Faqiyh, Shaykh Ibn ‘Uthaymin anasema kuwa ikiwa kiasi kilichomo ni kidogo kuliko 5% basi itakuwa haina neno waweza kuitumia tu, na hiyo ndio kauli ya Wanachuoni wengi wa karibuni. Ama kiwango kikiwa kikubwa, kwa kiasi ambacho unaweza kutambua hilo basi itakuwa ni bora kuacha kutumiwa ila kwa mambo yasiyokuwa na budi kama kusafishia vidonda na mfano wake. Ikiwa si lazima kutumia itakuwa ni bora kutotumia japokuwa hatusemi kuwa ni haramu. Inajulikana kuwa matumizi kwa kunywa au kuliwa ni haramu lakini utumiaji kwa njia nyingine isiyokuwa hiyo inafaa. Hata hivyo, hili ni jambo la kujadiliwa, lakini kuwa katika hali ya salama ni kuacha kutumia. Wengine wanasema kuwa alcohol inayotumiwa katika manukato au deodorants hazikufanywa kwa ajili ya ulevi, wala haimpelekei mtu katika hilo, pia haitumiki kwa kunywa. Hakika ni kuwa hii kimsingi ni tofauti na khamr, hivyo msimamo wa kuiruhusu una nguvu zaidi.

  1. Kwa kuwa tayari tumesema kulingana na kauli yenye nguvu kuwa pombe ni twahara ingawa ni haraam (kwani si kila haraam ni najisi), hivyo ikiingia katika nguo unaweza kuswalia bila matatizo. Ama ikiwa imechukuliwa kuwa ni najisi kwa kauli ya Wanachuoni wengine utaosha sehemu ya nguo ambayo imeingia pombe kisha uswalie bila wasiwasi.

Ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:

Kutumia Lotion au Mafuta Ambayo Ingredient Yake Ina Alcholol

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share